Waliounguliwa maduka Mlango Mmoja walia kutoswa, Serikali yawajibu

Wafanyabiashara 13 kati ya 92 waliounguliwa meza na bidhaa zao kwenye tukio la moto ulioibuka na kuteketeza soko la Mlango Mmoja Kata ya Mbugani jijini Mwanza, wamelalamikia kutojumuishwa kwenye mpango wa kupatiwa fremu kwenye mradi wa jengo la maduka katika soko hilo.
Muktasari:
- Ingawa Serikali iliahidi kutoa kipaumbele kwa waathirika, baadhi yao wamekosa vyumba. Halmashauri ya Jiji la Mwanza imekiri malalamiko na inaendelea kufanya uhakiki.
Mwanza. Wafanyabiashara 13 kati ya 92 waliounguliwa meza na bidhaa zao kwenye tukio la moto ulioibuka na kuteketeza soko la Mlango Mmoja Kata ya Mbugani jijini Mwanza, wamelalamikia kutojumuishwa kwenye mpango wa kupatiwa fremu kwenye mradi wa jengo la maduka katika soko hilo.
Tukio la moto huo lilitokea Septemba 28, 2018, ambapo baadhi ya bidhaa ya meza na maduka yaliyokuwa na mali za wafanyabiashara hao ziliteketea.
Hata hivyo, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagama (wakati huo), Dk Philis Nyimbi alifika eneo hilo na kutoa ahadi kuwa Serikali itajenga upya sehemu ya soko hilo, huku akiahidi waathiriwa kupewa kipaumbele kwenye zabuni za kutumia maduka yatakayojengwa ndani ya soko hilo.
Utekelezaji wa mradi wa majengo yenye maduka 45 umekamilika na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza lilipo soko hilo kutangaza zabuni kwa wanaohitaji kuingia katika maduka hayo. Hata hivyo, baadhi ya waathiriwa walipatiwa vyumba, huku 13 wakikosa fursa hiyo.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 9, 2024, mwathiriwa wa moto huo, Makanga Maage amewataja waathiriwa wenzake waliokosa maduka hayo kuwa ni Elizabeth Lazima, Hezron Sigwa, Dotto Mohamed, Hassan Makanga, Makanga Maage, Amina Hamad, Hashim Ally, Vanensia Masau, Marry John, Saidi Hemed, Winfrida Mganda na Moksi Baraka.
“Baada ya soko kuungua na meza zake Serikali ilianza ujenzi wa meza, tukaambiwa ujenzi wa mara ya pili utafanyika na kweli ulifanyika yakajengwa maduka ambayo yapo hapa sokoni wa maduka 45 na waathiriwa tulikuwa 32 tukaambiwa tusubirie tutapewa.
“Wafanyabiashara tuliounguliwa meza na maduka yetu kwenye soko hili tunaona kama haki yetu inaporwa, badala yake wamepewa maduka watu ambao si waathiriwa,”amesema na kuongeza;
“Nimeathirika sana kifamilia na kiuchumi kwa sababu sifanyi biashara kwa sababu sina eneo,” amesema Makanga.
Mwathirika mwingine, Mbaraka Karibuami amesema kutokana na kutopewa fremu katika majengo hayo amelazimika kuning’iniza bidhaa zake, ikiwemo nguo na viatu kwenye mbao na milango ya wafanyabiashara wengine, huku akiiomba Serikali na uongozi wa jiji hilo kuwafikiria upya.
“Tumefilisika mitaji kwa sababu ya ule moto, tulitarajia tungefutwa machozi angalau kwa kupewa kipaumbele kwenye maduka yanayojengwa, lakini tunashangaa kuona wakipatiwa watu ambao hawakuwepo wakati soko linateketea,” amesema Mbaraka.
Akijibu kuhusu malalamiko hayo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Jiji la Mwanza, Martine Sawema amekiri kuwepo malalamiko hayo na kusema ni kweli wapo baadhi ya wafanyabiashara waliokosa vyumba kwenye maduka 45 yaliyojengwa katika soko hilo.
Hata hivyo, Sawema amesema uhakiki bado unaendelea kuhusu ukweli wa wafanyabiashara wanaodai kutoswa katika zabuni hizo, huku akidokeza kuwa taarifa za awali za uhakiki unaofanywa na idara ya biashara ya jiji hilo zinaonyesha kati ya 13, ni wafanyabiashara wanane pekee ndio wanakidhi sifa hiyo.
“Tulitoa tangazo la zabuni na likitolewa linakuwa na muda, sasa kuna watu ambao hawakuomba, tuliposikia malalamiko hayo ya watu 13 tulipofuatilia tulibaini majina halali ni manane waliokuwepo kwenye soko wakati linateketea. Majina matano hayapo, idara ya biashara inaendelea kuhakiki,” amesema Sawema.
Ofisa huyo amewataka wafanyabishara hao kuwa na uvumilivu wakati Serikali inasaka mwarobaini wa malalamiko yao, huku akitoa ahadi kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi ndani ya kipindi cha wiki nne kuanzia leo Septemba 9, 2024.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Masoko ya Mkoa wa Mwanza, Hamad Nchola ameiomba halmashauri ya jiji hilo kutumia hekima kutafuta suluhu ya suala hilo kwa kile alichodai wafanyabiashara hao wana haki ya kupatiwa maduka katika soko hilo pamoja na kuwa huenda hawakuomba zabuni.