Waliofariki ajali ya basi, Noah Rombo wafikia 10

Basi la Ngasere na Noah baada ya kupata ajali katika eneo la Tarakea katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ajali ya basi na Noah Wilaya ya Rombo, imeongezeka na kufikia 10.
Rombo. Idadi ya watu waliofariki katika ajali ya basi na Noah katika eneo la Tarakea Rombo mkoani Kilimanjaro imefikia 10 baada ya majeruhi mmoja kufariki jana usiku.
Ajali hiyo ilitokea jana, Desemba 26, 2024 saa 9:40 alasiri katika Kijiji cha Kibaoni, Tarakea baada ya dereva wa gari aina ya Noah aliyekuwa anayapiota magari mengine bila tahadhari kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Ngasere na kusababisha vifo hivyo.
Akizungumza na Mwananchi leo, Desemba 27, 2024 Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mwangwala amesema mpaka sasa vifo vimefikia 10 na tayari miili tisa imeshatambuliwa.
"Majeruhi mmoja alifariki jana na idadi ya vifo kufikia 10, mpaka sasa miili tisa wameshatambuliwa na taratibu nyingine zinaendelea," amesema DC Mwangwala.
Jana Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema: "Leo majira ya saa 9:40 jioni huko Kijiji cha Kibaoni, Tarafa ya Tarakea, Wilaya ya Rombo barabara kuu ya Moshi-Tarakea gari kampuni ya Ngesere ikitokea Dodoma kwenda Tarakea iligongana na gari dogo la abiria likitokea Tarakea kwenda Moshi na kusababisha vifo vya watu tisa waliokuwa kwenye Noah," alisema Kamanda Maigwa.
Kamanda Maigwa aliwataja waliofariki katika ajali hiyo ni Mamasita Lowasa (27) mkazi wa Kamwanga, Damarisi Kanini Mwikau (22) mkazi wa Elasti Kenya, Peter Urio (38), Monica Mumbua (64) raia wa Kenya, Eligatanasi Kanje (30) mkazi wa Tarakea na Hilda Leberatus (24), mkazi wa Kikelelwa.
Kamanda Maigwa alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Noah akijaribu kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.
Kufuatia ajali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa salamu za pole kwa familia kutokana na ajali hiyo iliyosababisha vifo hivyo.
“Nimesikitishwa na taarifa ya vifo vya ndugu zetu tisa kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea katika barabara ya kutoka Tarakea, Wilaya ya Rombo kuelekea mji wa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro,” ameandika Rais Samia katika mitandao yake ya kijamii.
“Ninawaombea marehemu wapumzike kwa amani. Ninatoa salamu za pole kwa wafiwa, ndugu na jamaa na ninawaombea majeruhi wapate nafuu kwa haraka.”
Kadhalika, aliwataka madereva kuwa makini na waangalifu zaidi barabarani, huku akilitaka Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia sheria za usalama barabarani wakati huu wa mwisho wa mwaka.