Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakurugenzi wa H’shauri Lindi watakiwa kutenga bajeti za vifaa vya michezo

Muktasari:

  • Aga Khan imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya michezo shule za msingi na sekondari mkoani Lindi

Lindi. Wakurugenzi wa halmahauri mkoani Lindi wametakiwa kutenga bajeti ya ndani ili kununua vifaa vya michezo na kutengeneza vilivyoharibika vinavyotolewa na wadau wa maendeleo.

Wito huo umetolewa leo Ijumaa Juni 14, 2024 na Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk Bora Haule wakati akipokea vifaa vya michezo kutoka Shirika la Aga Khan mkoani Lindi katika Shule ya Msingi Wiles.

Dk Haule amesema vifaa vinavyotolewa na wadau wa maendeleo vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akiwataka wakurugenzi kutenga bajeti ya mapato ya ndani ili kuongezwa vifaa vya michezo kwa watoto wa shule ya msingi na sekondari kwa kuwa kucheza vizuri kunakuza akili zao pamoja na kujenga afya bora.

“Niwaombe wakurugenzi wote wa mkoa wa Lindi wahakikishe vifaa vya michezo kwa shule za msingi na sekondari vinaongezwa pamoja na kuvifanyia ukarabati vinapoharibika. Vifaa hivi vinatakiwa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” amesema Dk Haule.

Meneja wa Shirika la Aga Khan Mkoa wa Lindi, Kawanga Mapunda amesema wametoa vifaa vya michezo na kufundishia vyenye thamani ya Sh268 milioni katika shule za msingi na sekondari.

Mapunda amesema Aga Khan inatekeleza miradi ya elimu Wilaya ya Ruangwa, Manispaa ya Lindi pamoja na Halmashauri ya Matama.

“Tumekabidhi vifaa kwa Shule ya Msingi Wiles, huu ni mwendelezo kwa kuwa tulishatoa vifaa mbalimbali kwa shule za sekondari zikiwamo kompyuta mpakato, vifaa mbalimbali vya stationary, vishikwambi kwa walimu pamoja na projector.

“Leo tumeleta vifaa vya michezo kwa watoto wa awali na msingi ikiwamo mipira, bao, mikeka kwa ajili ya kukalia wakati wa kucheza mdako, draft na vifaa vya kuhesabu jumla vyote vina thamani ya Sh268 milioni,” amesema Mapunda.

Akizungumzia msaada huo, mwanafunzi wa darasa la nne, Waziri Mohamed ameishukuru Aga Khan kwa kuwapatia vifaa vya michezo.

“Tunashukuru sana Aga Khan kwa kutuletea vifaa vya kuchezea, awali tulikiwa tunacheza kwa mipira tunayotengeneza wenyewe, sasa ile mipira inaumiza sana, lakini kwa sasa tutacheza vizuri sana kwa kuwa tumepata mipira ya kisasa,” amesema Waziri.

Aisha Seif, mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo, amesema vifaa walivyoletewa vitawasaidia kujenga mwili pamoja na akili kwa kuwa michezo inaleta afya nzuri na kuwafanya kuwa na nguvu.

“Michezo hujenga mwili na afya bora, hivi vifaa tulivyoletewa vitatusaidia sana katika kuendeleza somo la michezo pamoja na sisi wenyewe kucheza vizuri pindi tunapokuwa shuleni,” amesema Aisha.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Wiles, Fatuma Mkatwa amesema vifaa walivyopewa vitawasaidia katika kufundisha na somo la hesabu.

“Hivi vifaa vya michezo vitatusaidia sana kufundisha na somo la hesabu katika madarasa ya awali, tunawashukuru sana la Aga Khan kwa kuiona shule yetu na kutuletea vifaa hivi,” amesema Mwalimu Mkatwa.