Wakulima watakiwa kuzingatia kilimo bora kabla ya kudai bei ya mazao

Mkuu wa Idara ya kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Makambako, Beatrice Tarimo akizungumza na wakulima katika uzinduzi wa duka la pembejeo Halmashauri ya Mji wa Makambako wilayani Njombe.
Muktasari:
Wito huo umetolewa leo Jumamosi Aprili 6, 2024 na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya mji wa Makambako, Beatrice Tarimo wakati wa uzinduzi wa duka la pembejeo za kilimo lililopo Halmashauri ya Mji wa Makambako hapa wilayani Njombe.
Njombe. Wakulima wametakiwa kuachana na malalamiko ya kuhusu bei ya mazao na badala yake wazingatie maelekezo ya wataalamu wa kilimo ili kupata mazao bora.
Kauli hiyo imekuja baada ya wakulima kuendelea kulalamika kuhusu bei ndogo ya mazao wakati wanachozalisha kuonekana hakina tija kutokana na kutumia eneo kubwa la shamba kuzalisha kiasi kidogo cha mazao, hivyo kushindwa kumudu gharama za uendeshaji
Wito huo umetolewa leo Jumamosi Aprili 6, 2024 na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya mji wa Makambako, Beatrice Tarimo wakati wa uzinduzi wa duka la pembejeo za kilimo lililopo Halmashauri ya Mji wa Makambako hapa wilayani Njombe.
Amesema wakulima wengi wamekuwa wakilalamikia bei ya mazao, lakini changamoto kubwa iliyopo kwa Watanzania katika kilimo sio bei bali ni tija katika kile kinachozalishwa.
"Uzalishaji kwa eneo mkulima anasema bei ya mazao ni ndogo kwa sababu kama kwenye ekari moja amevuna gunia nne akienda kuziuza Sh30, 000 maana yake atapata Sh120,000 akilinganisha gharama za uzalishaji na alichokipata hakiendani.
“Kwa hiyo kwa haraka haraka mkulima atakwambia shida yetu kubwa ni bei ya mazao," amesema Tarimo.
Amesema wakulima wanatakiwa kuondokana na tatizo la bei kwa kuanza kupambana na tatizo la tija katika kile kinachozalishwa na wakulima.
Amesema katika kupambana na tatizo la tija wakulima wanatakiwa kupata pembejeo kwa wakati ikiwamo mbolea, mbegu na viuatilifu.
Amewataka wakulima kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo kutoka kwa wataalamu kwa kuwa wengi hawafanyi hivyo na ndiyo sababu wanashindwa kunufaika na kilimo chao.
Tarimo amesema ili kilimo kiwe endelevu wakulima wanatakiwa kuchukua hatua kulima kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.
Ofisa Kilimo Kitengo cha Pembejeo Halmashauri ya Mji wa Makambako, Peter Emmanuel amesema ili wakulima wapate tija ya kile wanachozalisha wanatakiwa kufuata kanuni za kilimo ikiwamo kuandaa shamba mapema kabla ya msimu wa kilimo kuanza.
Amesema wakulima wanatakiwa kutumia mbegu bora zitakazowaletea kipato na zinazostahimili ukame.
"Tunatakiwa kudhibiti magugu kwa njia ya parizi au njia ya viuagugu lakini pia kudhibiti wadudu na magonjwa yanaoshambulia mazao yetu ili mazao yawe bora na tupate kwa wingi," amesema Emmanuel.
Ofisa Uhusiano na Serikali kutoka One Acre Limited Tanzania, Enhart Israel amesema uzinduzi wa duka hilo la pembejeo za kilimo utaleta chachu na kuongeza upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa urahisi.
"Hata hivyo, kampuni bado inaangalia fursa zilizopo na zinazojitokeza ili kufungua maduka mengine kwenye mikoa yetu hii ya nyanda za juu kusini," amesema Israel.
Diwani wa Kata ya Kitisi, Navy Sanga amesema uzinduzi wa duka hilo la pembejeo mjini Makambako utawasaidia wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo ya pembejeo za kilimo.
"Sasa huduma hii itakuwa jirani kabisa na makao yao niseme tu One acre Fund wamebuni kitu kizuri kufungua hili duka litawasaidia wananchi," amesema Sanga.
Baadhi ya wakulima Njombe akiwamo Ezekia Chongolo amesema changamoto kubwa waliyokuwa wanakumbana nayo ni kupata pembejeo feki, hivyo uwepo wa duka hilo unakwenda kumaliza changamoto hiyo.
"Changamoto ilikuwa ni kuuziwa mbegu feki halafu ujazo ulikuwa na shida unapoambiwa mfuko huu ni kilo 50 lakini ukienda kupima kule unakuta arobaini na tatu," amesema Chongolo.