Wahudumu wa mabasi wanolewa bongo wakilalamika kuhusishwa na kesi

Wahudumu wa kwenye mabasi mbalimbali ya masafa marefu na mijini wakisikiliza mafunzo ya namna ya kuboresha huduma zao yaliyotolewa na Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kushirikiana Latra kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Zaidi ya wahudumu 70 wa mabasi wamepatiwa mafunzo kupitia mradi wa Eastrip unaotekelezwa na NIT kwa ufadhili wa Benki ya Dunia
Morogoro. Baadhi ya wahudumu wa mabasi ya abiria ya masafa marefu na mijini wameeleza changamoto zinazowakabili, ikiwemo ya kuhusishwa kwenye kesi inapotokea mhalifu amepanda au kupakia mzigo kwenye chombo cha usafiri.
Vaileth Masawe, mmoja wa wahudumu hao amesema baadhi ya wahalifu wanaopanda kwenye mabasi bila wao kuwatambua ni wahamiaji haramu, majambazi na wanaosafirisha mizigo isiyo salama kama vile bangi na meno ya tembo.
Amesema wao hufanya kazi kwa uzoefu na hawana taaluma ya kumtambua mhalifu au mzigo wa hatari.
Kutokana na hilo, ameomba vyombo vya usalama viwapatie mafunzo ya kumtambua mhalifu na aina za uhalifu ili iwe rahisi kwao kutoa taarifa kwa wahusika.
"Abiria anaweza akaja na mzigo wa hatari, mfano meno ya tembo au bangi, au anaweza kuwapo mhamiaji haramu kwenye basi; kwa vile sina elimu ya kujua vitu hivyo nitashindwa kutoa taarifa, matokeo yake Polisi wanapokamata basi na mimi najikuta nahusishwa kwenye kesi na kuambiwa kuwa nafahamu au nashirikiana na wahalifu hao jambo ambalo si kweli," amesema Vaileth.
Kwa upande wake, Ally Kimweri ametaja changamoto nyingine ni kutokupewa mikataba ya kazi na kutoingizwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, jambo ambalo limekuwa likiwafanya wapoteze haki zao pale mmiliki wa basi anapoamua kupunguza wafanyakazi au anapofilisika.
"Hizi kazi zinategemea umri, itafika mahali sisi vijana tutashindwa kufanya, hivyo lazima katika kipindi hiki tujiwekee akiba kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya maisha yetu ya baadaye, isitoshe kazi hizi ni ya hatari, muda wowote unaweza ukapata ajali na ukapoteza maisha au kupata ulemavu, hivyo mikataba itaisaidia familia zetu kwa lolote litakalotokea," amesema Kimweri.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni kutukanwa na kudharauliwa na baadhi ya abiria kwa kuonekana kama ni kazi isiyofaa au isiyokuwa ya muhimu.
Hali hiyo amesema inasababisha baadhi ya wahudumu kushindwa kufanya kazi.
"Abiria anapanda kwenye basi unamwambia funga mkanda wa usalama hataki, anaanza kukutolea lugha chafu. Abiria mwingine unamuelekeza mahali pa kuweka mizigo yeye anang'ang'ania akae nayo kwenye siti, ukimuelekeza unazuka ugomvi, kwa kweli changamoto ni nyingi lakini tunajua namna ya kukabiliana nazo," amesema.
Ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kushirikiana Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kimeendesha mafunzo kwa wahudumu hao, lengo likiwa kuwawezesha kuboresha huduma wanazotoa na kuipa thamani kazi hiyo.
Akifungua mafunzo hayo jana Machi 18, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebecca Nsemwa amesema yatawawezesha kuonekana kuwa ni watu muhimu katika sekta ya usafirishaji.
"Ninyi ni watu muhimu sana, mmekuwa mkisimamia usalama wa abiria na mizigo yao kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari, mmekuwa mkikutana na watu mbalimbali wanaosafiri katika mabasi yenu. Mafunzo yatawasaidia kwa kuwa sasa mnaenda kutambulika na kurasimishiwa kazi yenu," amesema.
Nsemwa aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alisema, “nikiwaangalia wahudumu hawa wengi bado wana umri mdogo, hivyo wana ndoto zao, ili zitimie lazima kada hii ya uhudumu itambulike na ifanywe kuwa rasmi. Tunataka thamani anayopewa muhudumu wa kwenye ndege hiyohiyo apewe wa kwenye basi, lakini hatuwezi kufika huko bila ya kuwajengea uwezo wa kuboresha utendaji kazi wao," amesema.
Amewataka wahudumu kuwa wakarimu na wenye lugha nzuri kwa abiria, badala ya kubishana nao bila sababu za msingi.
Ofisa Mfawidhi wa Latra Mkoa wa Morogoro, Andrew Mlacha amesema baada ya mafunzo wanatarajia kuwa na kanzi data ya wahudumu wote wa mabasi ya masafa marefu na yale ya mijini, ili wawasajili na kuwapa vitambulisho vitakavyowasaidia kutambulika na kuifanya kazi hiyo kuwa rasmi.
Mlacha amesema baada ya kurasimishwa Latra kwa kushirikiana na mamlaka nyingine itawasaidia wahudumu hao kupata mikataba ya kazi na stahiki nyingine, zikiwamo za bima ya afya na mifuko ya hifadhi ya jamii.
"Latra imekuwa na miongozo inayowaelekeza namna wahudumu wa kwenye mabasi wanavyotakiwa kutoa huduma lakini kutokana na wahudumu wengi kukosa mafunzo wamejikuta wakitoa zisizo na viwango, hivyo kupitia mafunzo haya watapata weledi katika kuboresha huduma zao," amesema Mlacha.
Naibu Makamu Mkuu wa NIT, Zainabu Mshana amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa kanda.
Amesema mbali na kuboresha huduma wanazotoa, wahudumu watajengewa uwezo wa kumtambua abiria mwenye nia ovu au mizigo isiyo salama inayosafirishwa kwenye mabasi yao.
Mkuu wa kituo cha umahiri katika usafiri wa anga na oparesheni za usafirishaji kutoka NIT, Chacha Lyoba amesema mafunzo hayo yatafanya huduma za usafirishaji abiria kwa kutumia mabasi iwe bora na inayolingana na huduma zinazotolewa kwenye usafiri wa anga.
Amesema katika mafunzo, wahudumu watafundishwa elimu ya huduma kwa mteja, unadhifu, uaminifu na usalama wa abiria hasa katika kufunga mikanda kabla ya safari.