Wahalifu wavamia kijiji na kupora kisha kubaka wanawake

Muktasari:

  • Watu wanaodaiwa kuwa wahalifu wameuawa na wananchi baada ya kuvamia nyumba za watu katika Kijiji cha Bukungu, Kata ya Kharumwa wilayani Nyanghwale mkoani Geita na kupora kisha kubaka wanawake wawili.

Geita. Watu wawili wanaodaiwa kuwa wezi wameuawa na wananchi wenye hasira katika Kijiji cha Bukungu, Kata ya Kharumwa wilayani Nyang’hwale mkoani Geita baada ya watu hao kuvamia nyumba za watu usiku kisha kupora na kubaka baaadhi ya wanawake.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Jamhuri Wiliam amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea usiku wa Januari 17 ambapo kundi la watu nane hadi 10 walivamia vibanda vya biashara na nyumba za watu na kufanya uhalifu huo.

William amesema watu hao walipora baadhi ya vitu ambavyo thamani yake haijajulikana pamoja na kuwabaka wanawake wawili ambao tayari wameelekezwa kwenda hospitali kwa matibabu.
“Ni kweli tukio limetokea jana Kijiji cha Bukungu majira ya usiku wahalifu walivamia maeneo ya biashara na wananchi walipiga yowe kati ya watu 8 hadi 10 wengine walikimbia wawili walijeruhiwa na kabla ya kupelekwa hospitali walifariki,” amesema.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na taarifa zaidi itatolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi, Safia Jongo hazikuzaa matunda baada ya kutokuwa ofisini na hata simu yake ya mkononi ilipopigwa iliita bila majibu.
Serafine Richard mkazi wa Kharumwa amesema matukio ya uhalifu kwenye eneo hilo ni mengi na kuwa siku moja kabla ya makazi ya watu kuvamiwa watu wasiofahamika walivamia kituo cha mafuta Kharumwa na kuiba kisha kumjeruhi mhudumu.

“Matukio yanatokea hatuoni ufuatiliaji hata vyie vyombo vya habari hamripoti hali ni mbaya na huelewi kwanini yanakaliwa kimya mtu unavamiwa mke wako anabakwa mbele yako ni ukatili wa ajabu alisema,” Richard.

Taarifa za awali zinaeleza mmoja wa aliyeuawa anadaiwa kuwa mchimbaji mdogo wa dhahabu katika maeneo hayo na waliokuwa na silaha za jadi kama mapanga na rungu.