Wagombea chama mbadala cha walimu watamani kurudi CWT

Muktasari:
- Tumaini Nyagawa na wenzake wamepeleka malalamiko kwa msajili wa vyama na wanapanga kwenda mahakamani. Mwenyekiti Emmanuel Herman amesema uchaguzi ulifanyika kwa kufuata Katiba na rufaa zao zinashughulikiwa.
Dodoma. Mgogoro umeibuka katika Chama cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu Tanzania (Chakuhawata) baada ya kuibuka kundi la waliokuwa wagombea kuupinga uchaguzi huo kwa madai umekiuka Katiba ya chama hicho.
Uchaguzi huo uliofanyika Juni 26, 2024 mkoani Tanga umechagua viongozi wa ngazi ya Taifa, baada ya kushindikana kufanyika tangu mwaka jana kutokana na kukosekana kwa vibali vya mikutano.
Mgogoro huo umeibuka baada ya wagombea wa nafasi ya Katibu Mkuu (Tumaini Nyagawa) na Naibu Katibu Mkuu (Nyavidunda David Mhule) kudai kukiukwa kwa Katiba ya chama.
Akizungumza kwa niaba ya wagombea wengine, leo Jumatatu Julai, 8 2024, Tumaini Nyagawa amesema wameshapeleka taarifa zao kwa msajili wa vyama vya wafanyakazi kuhusu kukiukwa kwa Katiba kwenye uchaguzi huo.
Amesema wanasubiri uamuzi wa msajili wa vyama na kwamba wasiporidhika watakwenda mahakamani kupata tafsiri ya kisheria, ili kudai haki yao na wapiga kura wao.
Nyagawa amesema uchaguzi huo haukuwa wa kidemokrasia na kwamba walianza kuulalamikia tangu siku ya kwanza.
“Katibu yetu hii ya mwaka 2015 iko wazi na inataja mambo mengine ya haki, lakini tunaposema tunatetea walimu, halafu tunasigina Katiba haina maana kabisa, ni bora hata kama tungerudi CWT (Chama Cha Walimu Tanzania) tulikokimbia,” amesema Nyagawa.
Kwa upande wake, Hilary Mwingira amesema yeye na wenzake wengine wamekosa imani na chama hicho, hivyo kama wasiposikilizwa watafanya uamuzi wa kurudi CWT.
Amesema hata kama CWT itawakatalia kurudi kwenye chama chao cha zamani, watakaa bila chama cha kuwatetea kwa kipindi chote cha utumishi wao.
Akijibu tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Emmanuel Herman amesema uchaguzi huo ulifanyika kwa kufuata Katiba na kwamba kulikuwa na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyohakikisha kuna kuwa na usalama.
“Uchaguzi wetu umewahi kuzuiliwa mkoani Kigoma mwaka jana na Tanga pia. Kwa namna Serikali ya Rais Samia inavyopenda walimu tumepambana tukawa tumepata hicho kibali, kwa hiyo uchaguzi ulikuwa huru na salama na hakuna aliyepata dosari, aliyeumia wala kulalamika pale ukumbini,” amesema.
Herman amesema kuwa wagombea waliolalamika, wapo waliweka mawakala wao na wengine walikwenda kusimamia uhesabuji kura.
Amesema wagombea hao tayari wameshakata rufaa katika Kamati Tendaji ya Taifa ya chama hicho ambacho kikatiba ndicho kinashughulikia masuala ya rufani za uchaguzi.
“Muda si mrefu watasikiliza rufaa yao ndiyo maana hatujaona sababu ya kutoka hadharani kuanza kulalamika katika vyombo vya habari,” amesema na kuongeza waliokata rufaa ni wanachama wanne walikuwa wakiwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Chakuhuwata kilianzishwa mwaka 2015 ambapo makao makuu yake yako mkoani Kigoma na hadi sasa kina wanachama 29,500 nchini.