Waelezea hasi, chanya sakata la VPN

Muktasari:
- Wadau mbalimbali wametoa mitazamo tofauti juu ya uamuzi wa Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhusu kudhibiti matumizi ya mtandao binafsi wa VPN. Wamesema hayo waliposhiriki mjadala wa X-Space ulioandalia na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) uliokuwa na mada ‘Kuna tija kwa Serikali kusimamia matumizi ya VPN.
Dar es Salaam. Baada ya vuta nikuvute juu ya sakata la Serikali kudhibiti matumizi ya mtandao binafsi wa VPN, wadau mbalimbali wametoa maoni yao juu ya tamko la Oktoba 13, 2023 lililotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhusu kutaka usajili kwa watumiaji wa huduma hiyo.
Maoni ya wadau hao yanakuja ikiwa ni siku chache baada ya kuibuka kwa mjadala baina ya wadau na Serikali kuhusu usajili wa watumiaji wa huduma hiyo suala ambalo limevuta hisia za wengi kiasi cha kusababisha suala hilo kutarajiwa kufikishwa mahakamani.
Wadau wametoa maoni hayo leo Jumatano, Oktoba 18, 2023 katika mjadala wa X-Space iliyoandalia na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) iliyokuwa na mada ‘Kuna tija kwa Serikali kusimamia matumizi ya VPN.’
Akitoa maoni yake, Msemaji wa sekta ya Habari na Tehama wa ACT Wazalendo, Philbert Macheyeki amesema kilichopo ni mwendelezo wa sheria kandamizi unaolenga kushughulika na wakosoaji wa Serikali na vyombo vya habari vinavyojaribu kutoa habari za uchunguzi zinazoilenga Serikali.
Mcheyeki amesema suala la usajili wa watumiaji wa VPN halina tija kwasababu linatoa mwanya kwa raia kuweza kudukuliwa mawasiliano yao.
Amesema vilevile suala hilo linaweza kusababisha kukosa uhuru wa kuwasiliana, Katiba na sheria zinaruhusu uhuru wa kuwasilana na kupata habari hivyo suala hili ni ukandamizaji.
“Tunayoyaona leo sisi ACT Wazalendo tunatafsiri kama kundamiza uhuru wa kupata taarifa. Tamko hili la TCRA ni batili na liko kinyume na katiba ibara ya 16(1) na ibara ya 18,” amesema
“Tamko la TCRA linakwenda kurahisisha udukuzi wa taarifa binafsi kitu ambacho ni kinyume na Katiba ibara ya 16 inayolinda haki ya faragha. Hivyo, mamlaka inapaswa kwanza iangalie Katiba inasema nini,” amesema.
“Tamko hili halina tija kwakuwa linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya Tehama na uchumi wa kidijitali kwa kiasi kikubwa. Unapokwenda kuingilia faragha za kampuni kama benki watu binafsi ambazo zinatumia VPN kulinda taarifa zao hivyo matumizi yatadorora hivyo unakwenda kuua uchumi wa kidijitali ambapo tunajinasibu kama nchi tumepiga hatua,” amesema
Akitoa ushauri amesema Serikali inapaswa kujikita kupambana na utapeli na uharifu wa mtandaoni badala ya kuweka vikwazo vya kuzuia wananchi kuwasiliana pia amesema Serikali ijikite katika kurahisisha huduma za mawasiliano ya intaneti maeneo mbalimbali hususani vijijini.
Wakati Macheyeki akiyasema hayo, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe amesema VPN inasaidia kurahisisha upatikanaji wa mtandao akitolea mfano mahali anapoishi hawawezi kupata mawasiliano bila VPN.
Amesema hivyo suala la kujisajili linasababisha kutolewa kwa taarifa binafsi za mtumiaji ambazo kwa baadaye ni rahisi kuweza kuzipata taarifa hizo.
Akizungumzia uamuzi wa kukataza matumizi ya huduma hiyo kwaajili ya tatizo la kimaadili amesema tatizo la kimaadili haliwezi kuzuiliwa kwa kutengeneza kanuni zinazotaka watu wasajili.
“Kimsingi mtu mwenye maadili vizuri hawezi kushinda kwenye tovuti za maudhui yasiyofaa,” amesema Wangwe.
Akitolea faida za huduma hiyo amesema matumizi ya VPN yanasaidia pia kwa watu wanaofanya tafiti. Amesema kuna takwimu huwezi kuzipata bila kuwezeshwa kwa VPN.
Ukiachana na Wangwe, yupo pia mdau mwingine aitwaye, Namanyisa Chris aliyesema jamii ikisema VPN inaruhusu mmomonyoko wa maadili inampa changamoto kwa sababu ukiangalia maudhui yanayowekwa na wasanii kupitia nyimbo zao hazifahi.
“Serikali ingeanzia upande huo wa nyimbo za wasanii kama kweli inajali maadili,” amesema Chris.
“Haya yanafanyika kwa kuwa wanajua uchaguzi umekaribia na nguvu ya mitandao ya kijamii katika kuwaunganisha watu inazidi kukua,” ameongeza Chris
Naye Regan Mosha amesema zuio hilo linaleta taswira huenda Serikali inataka kujua taaarifa za watumiaji wa mitandao.
Amesema ni ngumu kushindana na teknolojia hivyo wahusika wafikirie mbadala ili wajue vitu wanavyotaka kuvijua. Amesema hakuna sheria inayozuia matumizi ya VPN.
Hata hivyo, akizungumza leo Jumatano, Oktoba 18, 2023 na waandishi wa habari baada ya kufungua kongamano la saba la taifa la Tehama linalofanyika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kwa sasa utapeli unaendelea hivyo Serikali haina budi kuwatambua wale wote wanaotumia VPN.
Amesema zaidi ya nusu ya Watanzania wanatumia intaneti kwa sasa hivyo hata utapeli unaendelea ndio maana na Serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo kutunga sheria.
"Serikali imetunga sheria za kuwalinda watu wakiwa mtandaoni kama sheria ya (Data Protection), Miamala ya Kelektroniki, ni hatua moja wapo zilizokwisha chukuliwa," amesema Nape.
Amesema jambo la pili ni kutengeneza vyombo na mifumo itakayosaidia ulinzi huo ikiwemo Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Waziri Nape amesema kilichopo sasa waharifu wanabuni njia mbalimbali ndio maana, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imechukua hatua hiyo ya kutaka watu wajisajili wajulikane kwasababu kuna watu wanatumia mwanya huo kutekeleza uharifu kwa kujificha.