Waeleza jinsi Nyerere alivyoshiriki ukombozi wa Afrika

Hayati Mwalimu Julius Nyerere
Muktasari:
Baadhi ya wanadiplomasia wameeeleza mchango wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, wakisema alichangia katika ukombozi wa Bara la Afrika katika kuziletea uhuru dhidi ya Wakoloni.
Dar es Salaam. Baadhi ya wanadiplomasia wameeeleza mchango wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, wakisema alichangia katika ukombozi wa Bara la Afrika katika kuziletea uhuru dhidi ya Wakoloni.
Hayo wameyasema leo Oktoba 12 katika kongamano la kujadili mchango wa Mwalimu Nyerere katika uga wa diplomasia, lililofanyika jijini hapa.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Chuo cha Diplomasia Dar es salaam Balozi Ramadhani Mwinyi, amesema Mwalimu Nyerere aliimarisha uhusiano wa kimataifa na kuleta ukombozi kwa nchi zilizokuwa katika utawala wa Wakoloni.
"Alitukomboa kutoka Ukoloni na ameshiriki katika ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, kwani hakupenda kuona Tanzania pekee inakuwa huru, huku nchi nyingine zikiwa bado kwenye ukoloni.
“Pia alitoa mchango mkubwa kwa nchi kwa nchi za Zambia na Zimbabwe," alisema.
Ameongeza kuwa Mwalimu Nyerere atakumbukwa kwa kuhimiza umoja na kuhamasiaha matumizi ya lugha moja ya Kiswahili.
Kwa upande wake Felix Wandwe Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia ameeleza jinsi Mwalimu Nyerere alivyoanzisha Sera ya Mambo ya Nje
"Mchango wa Mwalimu Nyerere ni mkubwa katika masuala ya diplomasia, kwani ndiye aliyeanzisha Sera ya Mambo ya Nje, japo imekuwa ikifanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara," amesema Wandwe.
Amesema kutokana na mchango wa Mwalimu Nyerere, diplomasia ya uchumi imeisaidia nchi kukua kiuchumi.
Akifafanua zaidi kuhusu diplomasia ya uchumi, Balozi Victoria Mwakasege amesema hayati Nyerere aliona suala hilo ni muhimu ndiyo maana alihimiza ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho, viwanda vya nguo na kuanzisha Shjirika la Kuhudumia viwanda vidogo (Sido) na diplomasia ya uchumi mapema na kujenga viwanda, kuanzia sido.
"Aliona ni namna gani tutakuwa kiuchumi na kuingia katika dunia pana na kujenga misingi, kwani diplomasia ya uchumi lazima ianzia nyumbani," amesema Mwakasege.
Naye mwalimu wa chuo cha diplomasia, Deus Kibamba amesema kutokana na umahiri wa Mwalimu Nyerere, maandiko ya ndani na kimataifa yamekuwa yakichambua kauli zake.
"Mwalimu alihakikisha imani yake inayosema, usalama wa nyumba yako haina maana kama majirani zako hawako salama, pia alitumia lugha inayofikirisha wakati wa kutoa ujumbe kiasi kwamba usingeweza kumwelewa wakati ule ule," amesema Kibamba.
Awalia kifungua kongamano hilo, Spika mstaafu, Anne Makinda amesema Mwalimu Nyerere alikuwa mtu mwenye hekima sana na anapenda kusikiliza watu bila kujali umri wala cheo.
Pia, amesema Mwalimu Nyerere alijali nafasi ya mwanamke katika uongozi, kwani hata viti maalum bungeni vilianzishwa kipindi cha mwalimu na mpaka sasa sera hiyo inaishi.