Wadau wataka uchumi wa buluu ulinde wavuvi wadogo

Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko akipata maelezo kutoka kwa mwakili wa banda la benki ya NMB katika mkutano wa Afrika wa wavuvi uliofanyika Dar es Salaam.
Muktasari:
- Waeleza kutokana na mipango ya Serikali ya uchumi, baadhi ya jamii zimefukuzwa kwenye maeneo yao.
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuweka mkakati wa kuwaendeleza wavuvi nchini, wadau wametaka juhudi hizo zilenge kuwalinda wadogo na jamii zinazozunguka maeneo ya uvuvi.
Akifungua mkutano wa Afrika wa wavuvi wadogo uliokusanya washiriki zaidi ya 400 kutoka nchi 32 za Afrika Juni 5, 2024 Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko alisema asilimia 95 ya wavuvi wa Tanzania ni wadogo, hivyo wanapaswa kuwezeshwa.
Amesema Serikali itaendelea kuanzisha viwanda kwa ajili ya uchakataji wa samaki, mahali pa kuhifadhia au kugawa boti za uvuvi za kisasa, vizimba vya kufugia samaki na zana zinazohusika.
Dk Biteko amesema pia kutoa pembejeo za kufugia samaki kama chakula na vifaranga, misamaha ya kodi kwa uagizaji wa bidhaa za samaki.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu mada aliyotoa katika mkutano huo, Profesa Maemba Isaacs wa Chuo Kikuu cha Western Cape cha Afrika Kusini, amesema wakati Serikali inapigia debe uchumi wa buluu, kuna haja ya kuziangalia jamii za wenyeji ili zifaidi matunda yake.
“Ninachozungumzia ni haki za buluu ambazo zinahusiana na uchumi wa buluu. Ni kwa kiasi gani umewafukuza wavuvi katika maeneo yao ya rasilimali na ya asili na kwa utamaduni wao kwa kisingizio tu cha uchumi na utunzaji wa mazingira,” alisema.
Amesema kutokana na mipango ya Serikali ya uchumi, baadhi ya jamii zimefukuzwa kwenye maeneo yao.
“Kulikuwa na mwanafunzi wangu aliyefanya utafiti Mtwara, alieleza jinsi uwekezaji wa gesi ulivyosababisha wananchi kufukuzwa kwenye maeneo yao, kule Mafia pia wananchi waliondolewa kwenye maeneo yao kwa sababu ya utalii, pia kuna kazi tulifanya Mwanza katika Ziwa Victoria ambako wanawake wengi wamejiajiri kwenye uchakataji wa samaki.”
“Serikali inapopanga mipango inapaswa kuwaangalia wavuvi wadogo wapate masoko na wapate haki zao,” alisema.
Dk Almas Mazigo wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce) alisema licha ya Serikali kuwasaidia wavuvi kwa vifaa, bado kuna haja ya kuwekeza vyenye uwezo wa kwenda mbali na kufanya uvuvi wa kibiashara.
Kuhusu fursa za vijana katika uchumi wa buluu, Shamimu Nyanda kutoka Taasisi ya Tanzania Ocean Climate Innovation Hub inayofanya kazi chini ya Umoja wa Mataifa, alisema bado vijana hawajapata elimu ya kutosha kuhusu uchumi wa buluu.
“Naishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha mpango wa 'Jenga kesho iliyo njema' (BBT), hii ndiyo kesho yetu. Nimezungumza na baadhi ya vijana kuhusu uchumi wa buluu, wengi wanasema uko Zanzibar, hiyo siyo kweli, uchumi wa buluu upo kote Tanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Serikali, Tanzania huzalisha tani 472,579 za samaki kwa mwaka na kati ya hizo, tani 429,168 zinatokana na uvuvi katika maji ya asili.
Sekta hiyo pia huzalisha Sh3.4 trilioni kwa mwaka na inakua kwa asilimia 1.9 kwa mwaka, ikikadiriwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 230,000.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) nchini, Dk Nyabenyi Tipo, alisema wavuvi wadogo wanazalisha tani 9.2 za samaki kati ya tani milioni 20 kwa mwaka.
Alibainisha kuwa wanawake watatu kati ya 10 wanashiriki katika uvuvi, wakichangia uchumi na lishe.