Wadau wataka ruzuku isiishie kwenye mitungi ya gesi

Muktasari:
- Wadau wa nishati safi ya kupikia wamesisitiza umuhimu wa elimu ili kufikiwa kwa lengo la matumizi ya nishati hiyo.
Wadau wameitaka Serikali isiishie kutoa ruzuku ya mitungi ya gesi pekee, bali ione namna ya kusaidia ujazaji wa nishati hiyo itakapoisha hasa kwa wananchi wa kipato cha chini.
Kwa mujibu wadau hao, hatua hiyo itawezesha hata wananchi wenye kipato cha chini kuwa na matumizi endelevu ya gesi, badala ya kubaki na mitungi ndani pale nishati hiyo inapoisha.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Meneja Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Oryx Gas, Shaban Fundi alipokuwa akishiriki katika mjadala wa jopo kuhusu mipango na mikakati ya nishati safi ya kupikia wakati wa Kongamano la 11 la Petroli la Afrika Mashariki na Maonyesho.

Amesema juhudi za kufikiwa kwa lengo la asilimia 80 ya Watanzania watakaotumia nishati safi ya kupikia, zitafanikiwa kwa kutolewa elimu kwa wananchi.
Ameeleza elimu hiyo, inapaswa kuhusisha uelewa kuwa, matumizi ya gesi ni nafuu ukilinganisha na nishati nyingine katika mapishi.
Sambamba n hilo, amesema juhudi zinafanywa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) hazipaswi kuishia kutoa ruzuku ya mitungi ya gesi pekee, badala yake wawajazie nishati hiyo wananchi, hasa wa kipato cha chini.
“Pamoja na changamoto katika usambazaji wa nishati safi, hususan LPG, kuna hitaji kubwa la elimu juu ya mpito wa nishati ili kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kuhamia nishati safi ifikapo mwaka 2034," amesema.
Amesema licha ya juhudi zinazoendelea, bado kuna wananchi wanaoamini kupika kwa gesi kuna madhara, hivyo ni muhimu kutoa elimu na hatimaye wananchi waone nishati safi ya kupikia ndio suluhisho sahihi katika kupika.
Pia amesema kwa sasa hali ilivyo watumiaji wengi wa mkaa wako mijini sio vijijini, hivyo juhudi za Serikali lazima pia zizingatie eneo hilo katika mpito wa nishati.
“LPG ni nafuu kuliko mkaa kwa kiwango sawa cha matumizi.Kwa kutambua juhudi na msaada wa serikali kupitia REA na wadau wengine, tufikirie kutoa ruzuku sio tu mitungi ya gesi bali pia kujaza gesi kwa watu wa kipato cha chini hasa vijijini,” amesema Fundi.

Amesema kwa nafasi yao wametoa elimu kwa wananchi kufahamu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia kwa kuwa mbali ya kutunza mazingira pia inasaidia kujikinga na madhara ya kiafya yanayotokana na chembechembe za moshi wa kuni au mkaa.
Pia, amesema katika kufikisha gesi ya kupikia maeneo ya vijijini wameendelea kuongeza vituo vya kusambaza gesi kupitia mawakala wao walioko katika Wilaya na Vijiji huku akitoa rai kwa wadau wengine kupeleka gesi vijijini kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wake.