Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau washauri hatua mpya kudhibiti kelele masokoni -3

Muktasari:

  • Licha ya kelele hizo kuzoeleka kama sehemu ya uuzaji na ushindani wa kibiashara, zimeendelea kuibua malalamiko kutokana na athari zake kwa afya na mazingira ya biashara.



Dar es Salaam. Baada ya mfululizo wa makala kuhusu kelele za vipaza sauti masokoni, katika sehemu ya mwisho wa mjadala, wadau wanaelekeza hatua kwenye suluhisho.

Licha ya kelele hizo kuzoeleka kama sehemu ya uuzaji na ushindani wa kibiashara, zimeendelea kuibua malalamiko kutokana na athari zake kwa afya na mazingira ya biashara.

Wadau mbalimbali wanaeleza mitazamo yao kuhusu namna bora ya kudhibiti kero hiyo, huku wakipendekeza udhibiti wa matumizi ya spika kupitia sheria na viwango maalumu.

Pia, wanaeleza umuhimu wa utoaji wa elimu, mipango bora ya masoko na ushirikiano wa taasisi za Serikali kama suluhisho linalotekelezeka bila kuathiri shughuli za kiuchumi.

Mtaalamu wa sheria kutoka Taasisi ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Leat), Rajab Rajab, anasema kero za kelele si za Dar es Salaam pekee, bali zipo katika maeneo mbalimbali na si kwenye biashara pekee, bali hata kwenye makazi ya watu.

Rajab anasema, kikatiba, kelele ni kosa kwa sababu linahusisha suala la afya linalomuondolea mtu uhuru wa kuishi katika mazingira safi na salama.

“Sasa sokoni huyu ana kelele na yule ana kelele, zinaumiza. Hapa kuna sheria za kudhibiti kelele na zimeweka viwango vinavyotakiwa kufuatwa. Unajua hata kupiga honi hairuhusiwi kwenye maeneo ya hospitali, labda iwe kwa dharura, na kwenye masoko kuna kelele za muziki, vipaza sauti na matangazo, pia honi za bodaboda,” anasema Rajab.

Rajab anasema kuna viwango vya kelele vilivyowekwa kisheria ambavyo Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) wana chombo cha kupimia, akitolea mfano viwango vya kelele vya mchana na usiku katika maeneo ya biashara na makazi ya watu.

Mwanasheria huyo anasema wamiliki wa biashara katika maeneo ya masoko wana wajibu wa kutumia njia bora kupunguza changamoto za kelele na kuhakikisha hazizidi kiwango kilichowekwa.

“Suluhisho ni mamlaka kuchukua hatua, lakini pia mamlaka za mitaa zina jukumu la kulinda afya na usalama wa maeneo yao, hivyo mamlaka husika zinapaswa kuweka vidhibiti vya kelele ili kupima ubora wa sauti,” anasema Rajab.

Naye wakili, John Mallya, anasema moja ya suluhisho la kuondokana na changamoto hiyo ni kuiga mfano wa viwanda ambavyo, kabla ya kuanzishwa, lazima vipewe kibali kutoka NEMC kuhusu mazingira.

“Kinachotakiwa kufanyika kwa wafanyabiashara hawa ni kwamba wanapaswa, wakati wanaomba leseni zao za biashara, iwe manispaa au katika ofisi nyingine, kuwepo na kipengele cha kibali cha kupiga kelele kama ilivyo kwenye biashara zinazohusisha kelele,” anasema Mallya.

Anasema kuzuia kelele kwenye masoko ni jambo lisilowezekana kutokana na asili ya mazingira yenyewe, kwani ni lazima kukutana na kelele. Hivyo, ili kuruhusu jambo hilo, ni lazima mfanyabiashara awe na kibali cha kufanya hivyo, tofauti na hapo mkono wa sheria unamhusu.

Kutokana na kukithiri kwa kelele hizo katika masoko, daktari bingwa wa masikio, Salum Seif, anasema suluhisho lake si kuzuia shughuli za masoko, bali kuweka udhibiti wa viwango vya sauti, kupanga matumizi ya spika kwa usalama na kuzingatia muda sahihi.


NEMC

Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Hamad Taimulu, anasema kwa mwaka wa fedha 2025/26, baraza hilo linaendelea na mkakati wa udhibiti wa kelele na tayari wameandaa utaratibu mzuri wa dokezo, ili kupeleka kwenye taasisi zilizotajwa kwenye mwongozo kwa lengo la kushirikiana.

Anasema NEMC pekee haiwezi kudhibiti kelele bila kushirikiana na taasisi nyingine zilizoorodheshwa kwenye mwongozo wa udhibiti wa kelele.

Taimulu anasisitiza kuhusu utoaji wa elimu katika kudhibiti changamoto hiyo na pale inapobidi wanalazimika kutoza faini.

“Ukiona kelele unasema kazi ya NEMC, bodaboda inapiga kelele au kutoa moshi kazi inaelekezwa kwetu, lakini tukitoa elimu inawezekana kudhibiti,” anasema Taimulu.

Naye Katibu wa wafanyabiashara wa Soko la Tandika Usangi, Muhrami Simba, anasema ni vigumu kuziondoa zote kwa wakati mmoja, lakini Serikali inaweza kuweka utaratibu maalumu utakaohakikisha spika hizo haziwi kero kwa wengine.

“Wanaotumia spika au vipaza sauti wanatakiwa kukutana na watendaji wa Serikali ili kupewa elimu ya matumizi ya vifaa. Vifaa hivi vinaingia nchini na vinalipiwa kodi, hivyo sioni Serikali ikachukua uamuzi wa moja kwa moja wa kuviondoa,” anaeleza.

Lakini mfanyabiashara wa Kariakoo, Andrea John, alikuwa na mawazo tofauti akisema njia pekee ya kuondokana na changamoto hiyo ni Serikali kupiga marufuku matumizi ya spika hizo, na si vinginevyo.

“Mbona zamani hazikuwepo na watu walikuwa wanauza kama kawaida? Hali si nzuri, mtu una ‘stress’ (mawazo) za maisha, ukija sokoni unakutana na kelele. Viongozi wa Serikali, itusaidieni,” anaeleza.

“Baadhi ya wafanyabiashara hapa wanaumwa vichwa kwa nyakati tofauti. Tunaposema hali ni mbaya hatutanii, tunamaanisha Serikali iingilie kati,” anasema John.


Mabadiliko ya kisaikolojia

Mwanasaikolojia, Yisambi Mbuwi, anasema katika ulimwengu huu watu wanatofautiana, wapo wanaopata faraja na msisimko wanapokuwa kwenye mazingira yenye kelele, huku wengine wakipata usumbufu mkubwa unaoweza hata kuathiri hali yao ya kisaikolojia.

Mbuwi anasema tofauti hizo zinatokana na namna ubongo wa mtu unavyochakata sauti pamoja na uzoefu na mazoea ya maisha ya kila siku.

Kwa mujibu wa Mbuwi, mtu anayekumbana na kelele zisizomfaa anaweza kupata madhara kama msongo wa mawazo, kukosa umakini na hata kuchoka haraka, hali inayoweza kuathiri uzalishaji na ustawi wake kwa ujumla.

Kutokana na hali hiyo, anashauri kuwa ni muhimu kwa mtu binafsi kujitambua na kuchukua hatua stahiki za kujilinda kiafya, ikiwemo kujiepusha na mazingira yenye kelele nyingi pale inapowezekana.

“Kuna kitu wewe hutaki, lakini mwenzako anakitaka. Ni jambo ambalo huwezi kulibadilisha. Kikubwa ni yule asiyependa hizo kelele ndiye anayetakiwa kubadilika na si kumbadilisha mtu mwingine,” anasema Mbuwi.

Hata hivyo, anasema pamoja na umuhimu wa mtu binafsi kujilinda, jamii na mamlaka pia zina wajibu wa kuweka mazingira rafiki kwa wote kwa kuweka mipaka ya matumizi ya sauti ili kupunguza migongano kati ya wanaopendelea utulivu na wale wanaopendelea kelele.


Hatua zinazochukuliwa

Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Jomary Satura, anasema wanaotumia spika hizo mara nyingi ni wamachinga, hivyo mipango iliyopo katika halmashauri hiyo ni ujenzi wa masoko matatu ya kisasa katika maeneo ya Keko, Mbagala na Tandika.

“Wafanyabiashara wakishaingia kwenye vizimba vyao rasmi na kufanya biashara zao vizuri, kelele hizo hazitakuwepo. Mtindo wangu ni tofauti kidogo na wengine kwa sababu sipo kwa ajili ya kupambana na wafanyabiashara,” anasema Satura.

Anasema utaratibu wake ni kusoma tatizo, kujua chanzo chake na kisha kufanyia kazi, kwani kugombana na watu ni ngumu kupata suluhisho la tatizo husika. Anaamini watu wakikaa maeneo maalumu ya biashara, haitawezekana kupiga kelele.

Satura anasema anaamini katika mwelekeo wa ujenzi wa masoko hayo na kwamba yakikamilika watu watapima kuhusu changamoto hizo, ambapo tayari soko la Mbagala limeshatangazwa na karibuni masoko ya Tandika na Keko yatatangazwa.

“Tofauti na kwenda kuwanyang’anya spika, huwezi kufanikiwa, bali masoko haya yatasaidia kuondokana na kelele. Masoko ya Tandika na Keko tutatumia mfumo wa ushirikiano wa sekta binafsi, tunaamini ujenzi wake utakwenda kwa kasi,” anasema.

Ushauri wa Kamati ya Bunge

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeshauri Serikali kuharakisha muswada wa marekebisho ya sheria bungeni utakaowezesha NEMC kuwa na mamlaka kamili.

Mbali na NEMC kuwa na mamlaka kamili, hatua hiyo itawezesha pia taasisi hiyo kuwa na uwezo ulioimarishwa wa kusimamia kwa ufanisi masuala ya mazingira.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jackson Kiswaga, alieleza hayo Aprili 21, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya maoni ya kamati kuhusu bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), iliyoomba Bunge kuidhinishia Sh76.68 bilioni.

Kwa mujibu wa Kiswaga, moja ya changamoto inayoikabili NEMC ni kutokuwa na nguvu kamili ya kimamlaka katika suala la uendeshaji na usimamizi wa shughuli za mazingira nchini.

“Jambo hili linapunguza kasi ya uratibu bora katika usimamizi wa mazingira, hivyo kamati inaishauri Serikali kuharakisha mchakato wa kuleta bungeni muswada utakaowezesha marekebisho ya sheria ya NEMC kuwa na mamlaka kamili,” alisema Kiswaga.

Mbali na hilo, Kiswaga amesema kamati hiyo inaishauri Serikali kuchukua hatua stahiki ili kuwezesha ushirikiano wa wadau wote wanaohusika kwa karibu na shughuli za mazingira.

Hatua hiyo imetokana na changamoto inayoikabili NEMC ya kutokuwa na ushirikiano wa karibu na wadau wanaohusika na shughuli za mazingira, jambo linalosababisha kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.