Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KELELE MASOKONI: Mamlaka zinasubiri malalamiko ya wananchi na si sheria - 2

Muktasari:

  • Suala la kelele linagusa haki za msingi za binadamu, hususani haki ya kuishi katika mazingira tulivu na salama. Katika miji yenye msongamano kama Dar es Salaam, kelele hizi zimevuka mipaka ya shughuli za biashara na kuathiri maisha ya watu kwa ujumla.



Dar es Salaam. Tatizo la kelele zinazotokana na matumizi ya spika masokoni limeendelea kuwa kero kwa jamii na tishio kwa makundi nyeti, wakiwemo wagonjwa.

Kwa mtazamo mpana, kelele hizi si tu zinavuruga utulivu wa mazingira, bali pia zinagusa moja kwa moja afya ya jamii na ustawi wa maisha ya kila siku.

 Suala la kelele linagusa haki za msingi za binadamu, hususani haki ya kuishi katika mazingira tulivu na salama. Katika miji yenye msongamano kama Dar es Salaam, kelele hizi zimevuka mipaka ya shughuli za biashara na kuathiri maisha ya watu kwa ujumla.

Hata hivyo, mjadala unaendelea kujengeka kuwa biashara zinaweza kufanyika bila utegemezi wa kelele kupitiliza. Wadau wanasisitiza umuhimu wa mbinu mbadala za ushindani sokoni, zikiwemo ubunifu, huduma bora kwa wateja na ubora wa bidhaa.


Vikao na mamlaka

Makamu Mwenyekiti wa wamachinga, Stephen Lusinde, anakiri kuwa matumizi ya spika ni changamoto kubwa, hasa kutokana na ukweli kwamba masoko mengi yapo karibu na makazi ya watu, hivyo kuongeza athari kwa jamii.

“Kutokana na jiografia ya nchi, masoko mengi yapo karibu na makazi ya watu, hivyo kelele zinapotokea kuna watu wengi wanaathirika, wakiwemo wagonjwa,” anasema Lusinde.

Lusinde anasema taasisi yao inawaza namna ya kulitatua jambo hilo, lakini ni lazima kila taarifa na uamuzi uende kwenye mamlaka za Serikali kwa ajili ya utatuzi.

Kwa mujibu wa Lusinde, Februari 5, 2026 walifanya kikao na mamlaka za Serikali na wadau wengine kujadili namna ya kudhibiti kelele hizo, na makubaliano ni kwamba changamoto hiyo itatuliwe kwa ushirikiano wa wadau wote.

“Tulifikia makubaliano kwamba changamoto hii itatatuliwa kwa ushirikiano wa wadau wote, kwani si lazima kufanya biashara kwa kupiga kelele. Mtu anaweza kuuza bila kutumia kipaza sauti,” anasema Lusinde na kuongeza kuwa:

“Suluhisho si lazima ufanye biashara kwa kupiga kelele, maana mwisho ni kuita wateja. Kila mtu asimame kwenye eneo lake na kufanya biashara pasipo kutumia kipaza sauti,” anaeleza.


Kariakoo nayo yakumbwa

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), Severin Mushi, anasema tatizo hilo si la wamachinga pekee, bali linahusisha hata wafanyabiashara wenye maduka.

“Wapo wafanyabiashara wenye maduka wameweka spika na kutangaza gharama ya bidhaa zao, hili ni tatizo kubwa Kariakoo. Tumekubaliana spika ziondolewe kabisa,” anasema Mushi.

Mushi anasema wamekubaliana spika hizo ziondoke zote Kariakoo, na ikitokea mfanyabiashara anakutwa nazo apigwe faini kubwa, na utaratibu maalumu umewekwa wa kuziondoa kwa ushirikiano wa mamlaka za Serikali.

Kwa mujibu wa Mushi, uwepo wa kelele hizo zinazotokana na spika unasababisha athari za afya ya akili kwa wateja na wafanyabiashara husika.

“Huyu anatangaza anauza betri, yule sumu ya mende, kunguni na panya, mara yule anatangaza kitu kingine. Ni vurugu kubwa, hakuna maelewano.

“Mtu akipigiwa simu anashindwa kuzungumza kwa ufanisi, hadi ajifiche sehemu. Ni matatizo makubwa kwa kweli. Vinawachanganya wananchi, si lazima wafanyabiashara wavitumie, wanaweza kufanya shughuli zao bila kuwa navyo,” anasema Mushi.

Anaeleza kuwa kwa nyakati tofauti amekuwa akipokea malalamiko ya watu, ikiwemo wanaowasilisha kwa maandishi kuhusu kero za kelele za spika wakidai zinawasumbua.

“Uzuri malalamiko yao tumeyawasilisha kwa mamlaka, tupo kwenye vikao vinavyoelekea ukingoni kuhusu utatuzi wa jambo hili hasa kwa Kariakoo,” anasema Mushi.


Vispika vyakosesha ajira

Mfanyabiashara wa viatu katika Soko la Karume, Baraka Aloyce, anasema matumizi ya spika yamechukua nafasi ya wapiga debe waliokuwa wakivutia wateja kwa mbinu za ubunifu.

“Zamani kulikuwa na vijana wapiga debe waliokuwa wanaimba na kuvutia wateja. Wengine walilipwa hadi Sh15,000 kwa siku. Sasa spika zimechukua nafasi yao,” anasema.

Anasema licha ya kupunguza kazi ya kupiga debe na kumrahisishia muuzaji kuita wateja, matumizi yake yamegeuka kuwa kero kwa jamii.

Aloyce anasema chanzo kikubwa cha tatizo ni wafanyabiashara wenyewe, kwani kuna kipindi vilipigwa marufuku na hali ikawa shwari, lakini baadhi ya viongozi wakafanya ushawishi vikarejeshwa.

Anasema uondoaji wa kelele hizo upo mikononi mwa wafanyabiashara wenyewe kabla ya kuingiliwa na viongozi endapo watakuwa na kauli moja.

“Nakupa mfano, kuna wakati hapa Karume vilipigwa marufuku kabisa kukawa shwari, lakini kuna viongozi wachache wenye ushawishi wakaenda kuonana na wabunge, ambao walifanya utaratibu vikarudi,”

“Hivi kweli hapo utailaumu Serikali au mamlaka za usimamizi wa mazingira? Kama sisi wenyewe tulikubaliana, lakini wachache wetu wakafanya ushawishi wa kuvirudisha,” anasema Aloyce.


Uzito wa tatizo kwa mamlaka

Wakati Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004 na marekebisho yake ya 2025 pamoja na vifungu vyake ikikataza upigaji kelele uliopitiliza, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, anasema hajawahi kupelekewa malalamiko ya kelele, iwe kutoka kwa wananchi, mbunge wala diwani, huku akiomba ushirikiano ili kupata uhalisia wa suala hilo.

“Katika masoko kuna uongozi, kuna wenyeviti na makatibu. Nisiwe muongo, sijapokewa malalamiko ya namna hiyo. Inawezekana ni kero kwa baadhi ya watu. Kama itakupendeza tuifanyie kazi kwa pamoja, tukianza kwa kutambua wananchi wana maoni gani kuhusu hili.

“Sio kila anayelalamika anapaza sauti, bali kuna wengine wanaugulia moyoni au chinichini, lakini kuna watu wanaona ni kawaida,” anasema Msando.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, anasema hata yeye linamkera suala hilo, si Karume pekee hadi Kariakoo, lakini ni wafanyabiashara wenyewe ndio wanaofanya bila uongozi wao kuchukua hatua.

“Changamoto iliyopo ni nani mlalamikaji, wananchi au wafanyabiashara? Kama wananchi sawa, lakini wafanyabiashara wao kwa wao wanaoneana aibu na mara nyingine hawaoneshi kama wanalalamika,” anaeleza Mpogolo.

Mpogolo anafafanua kuwa ndio maana wakati Soko la kisasa la Kariakoo linafunguliwa katika hotuba yake alisema kama mtu anauza dawa, panya au mende au soksi si muhimu kufunga spika akihoji ya nini.

Hata hivyo, Mpogolo anasema uongozi wa Ilala utalishughulikia suala hilo ili kupata ufumbuzi wa kudumu na wananchi wafurahie wanapokwenda kufanya manunuzi.

“Kikubwa kinachotakiwa tukae tuelewane, kitu ambacho ninaamini kila binadamu ana utashi. Moja ya sehemu ya utashi inatambua jema na baya. Hili tunaamini linatukera sote, ila nitalifanyia kazi nikishirikiana na viongozi wenzangu,” anasema.

Mpogolo ameahidi kulishughulikia kwa ushirikiano wa karibu na viongozi wote wa masoko, kwa kutoa elimu, akieleza kuwa jiji limeweka masharti ya marufuku ya kelele kwenye maeneo ya biashara.

Mkuu wa wilaya huyo anasema moja ya agizo la mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, ni marufuku kupiga matangazo ya namna hiyo, akihimiza ushirikiano wa uongozi wa masoko na wafanyabiashara wenyewe.

“Hakuna sauti ndogo wala kubwa, hairuhusiwi. Nakubaliana na wewe (mwandishi), tukemee tabia hii. Nitalishughulikia suala hili hadi lipate ufumbuzi,” anasema Mpogolo.


Kauli ya NEMC

Wakati wananchi na wafanyabiashara wakilizungumzia suala hilo, wasimamizi wa mazingira wanaeleza kuwa si kila sauti ni kelele.

Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Hamad Taimulu, anaeleza kuwa si NEMC pekee wenye jukumu la kudhibiti kelele, bali kuna taasisi nyingine za Serikali zinazopaswa kushiriki, kulingana na mwongozo wa udhibiti wa kelele wa mwaka 2021.

Aidha, Taimulu anasema NEMC huongeza weledi kwa kufanya vipimo katika maeneo ya biashara ili kubaini kiwango cha kelele.

Hata hivyo, anafafanua kuwa si kila sauti ni kelele hadi ipimwe kwa vifaa maalumu ili kubaini kama imezidi kiwango kilichowekwa kisheria.

“Ukiona viwango vimezidi hiyo ni kelele na hatua zinachukuliwa. Kwa maeneo ya sokoni, vipaza sauti ni vingi, hivyo unapopima kubaini chanzo cha kelele inakupasa uvizime vyote,” anasema Taimulu.

Anasema kwa viwango vya mchana katika maeneo ya biashara ni desibeli 55.

Anasema hata kama ni kimoja hakiwezi kutoa majibu sahihi, na ukiviwasha vyote huwezi kushtakiwa kwamba kila mtu anapiga kelele kwa pamoja bila kipimo.

Taimulu anasema kwa nyakati tofauti baraza hilo limekuwa likifanya mikutano na vyombo vya habari kutoa elimu kuhusu athari za kelele.


Itaendelea kesho…