Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau sekta ya madini washauri ya kufanya kukuza sekta hiyo

Wadau wa sekta ya madini wakiwa katika mkutano wa kimataifa wa madini Jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Wameitaka Serikali kuangalia namna ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ikiwemo kuwapatia ruzuku, nyenzo za kisasa na kuwekeza kwenye afya zao.

Dar es Salaam. Wachimbaji na wadau sekta ya madini nchini wametoa mapendekezo yao kwa Serikali yatakayofanikisha uboreshaji wa sekta ili kufikia malengo ya kuongeza mchango katika pato la taifa na maendeleo kwa ujumla.

Wamesema Serikali lazima iangalie namna ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ikiwemo kuwapatia ruzuku, nyenzo za kisasa na kuwekeza kwenye afya zao.

Hayo yamebainishwa kwenye mkutano wa sita wa kimataifa wa madini na uwekezaji Tanzania uliofikia kilele Novemba 21, 2024, mkutano huo wa siku tatu umewaleta pamoja washiriki zaidi ya 1,500 kutoka ndani na nje ya nchi.

Mchimbaji wa madini kutoka Chunya Benson Mwakilembe, amesema wachimbaji wadogo wanapaswa kufikiwa na ruzuku, vifaa vya kuchimbia pamoja na kupewa kipaumbele katika shughuli zao za uchimbaji.

“Changamoto nyingine inayohusu mikutano ya kimataifa kama hii ni kwamba wanashindwa kufikiwa kwa sababu hawana nauli ya kuja Dar. Mikutano kama hii inawakutanisha wachimbaji na kampuni na kuna fursa nyingi endapo wakiwepo watazipata, hivyo naomba Serikali ifanyie mikutano kama hii mikoani,” amesema.

Kuluthum Lunje kutoka Nachingewa, Lindi amesema changamoto inayokabili wachimbaji hususani wanawake wanapaswa kujengewa uwezo waweze kujiamini ili waendelee zaidi.

Abdi Yahya amesema uongezaji thamani madini uendane na kupunguza umasikini kwa jamii za Kitanzania kwa kampuni zilizotoka nje ya nchi kuwaajiri Watanzania kwa wingi.

Mdau mwingine wa sekta hiyo, Dk Dalali Kafumu amesema ushirikiano kama nchi unahitajika kwa ajili ya kuongeza uwezekaji zaidi ili kuongeza mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Aidha, wadau hao wamesema Serikali inapaswa isaidie vyuo vya kati na ufundi kuwa na maabara kwa ajili ya kuwandaa wanafunzi kuwa na ujuzi kwenye sekta ya madini ambayo watakuja kuifanyia kazi wakimaliza vyuo.

Wameitaka Serikali kuja na Sera rafiki kwa watu wa chini kwa ajili ya kuongeza mnyororo wa thamani wa shughuli zao, jambo ambalo hata mapato yataongezeka.

Kwa upande wake, mdau sekta ya madini, Peter Masika ametoa pendekezo la uwepo wa benki maalumu ya madini ambayo itatumia leseni kama dhamana kwenye mitaji na mikopo kwa wachibaji hao.

Amesema benki hiyo iwe na wataalamu wa madini watakaokuwa wanatambua mfumo mzima wa sekta, hivyo itakuwa rahisi katika kuwahudumia wachimbaji wadogo.

Naye Aron Mpole amesema ameona umuhimu wa mipango na taarifa za maazimio ya mikutano ya kimataifa ya madini ya kila mwaka kuwekwa bayana ili waweze kuunganishwa na wadau wa wadau na wawekezaji kirahisi kwaajjili ya kupata mafanikio.

“Wachimbaji wadogo wanapaswa kuwezeshwa kiteknolojia ambayo inahitajika sana tunataka Serikali iwasaidie ili wasiweze kufanya kazi zao ikiwemo kutafuta maeneo ya madini kienyeji,” amesema Mpole.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Tanzania inatarajia kuwa na maeneo maalumu ya kufanyia mikutano ya madini ili kuwawezesha kukutana na wageni, amewaomba wakuu wa mikoa nchini kutenga maeneo makubwa ya mikutano ya kimadini.

Mgeni rasmi wa mkutano huo, Naibu Spika Baraza la wawakilishi Serikali ya Mapindunzi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, amezungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali imeyapokea mapendezo na maazimio yote na inaahidi kuyafanyia kazi.

“Umetolewa ushauri na mapendekezo, nipende kuwahakikishia kuwa Serikali itazingatia yote ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji na kufikia lengo la kuzalisha ajira na pato la taifa,” amesema.

Pia, amesema: “Ili nchi inufaike ipasavyo na uwepo wa rasilimali hizi kama madini ya kinywe, shaba, nickel, basi lazima tuhakikishe tunajenga viwanda vitakavyoongeza thamani hadi kufikia uzalishaji wa bidhaa zikiwemo betri za magari ya umeme.”