Wachina wawili wadakwa wakitorosha dhahabu

Madini ya Dhahabu kilogramu mbili zilizokamatwa wilaya ya Ulanga
Muktasari:
- Wachina wawili na Mtanzania mmoja aliyewekeza katika machimbo ya madini wilayani Ulanga mkoani Morogoro wamekamatwa wakitorosha dhahabu kilo mbili zenye thamani ya Sh337 milioni
Morogoro. Wachina wawili na Mtanzania mmoja aliyewekeza katika machimbo ya madini wilayani Ulanga mkoani Morogoro wamekamatwa wakitorosha dhahabu kilo mbili zenye thamani ya Sh337 milioni
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Fotunatus Muslimu amethibitisha kukamatwa kwa watu hao na wanaendelea kuhojiwa na kuchunguzwa zaidi.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Ngolo Malenya, amesema walipata taarifa za utoroshaji wa madini hayo yaliyochimbwa katika mgodi uliopo kijiji cha Isyanga na walipofuatilia waliwakamata watuhumiwa hao.
“Ulanga inafahamika kwa madini, lakini kuna baadhi ya wachimbaji hawazingatii kanuni, sheria na taratibu za nchi zinazoongoza sekta ya madini na matokeo yake wanaishia kwenye mikono ya sheria wanapojaribu kufanya udanganyifu” amesema Malenya.
Malenya amesema ni vema wachimbaji wanapopata madini wayafikishe kwenye ofisi za madini kwaajili ya uhakiki na baadaye taratibu nyingine zifuatwe.
“Serikali tuko macho, hatuwezi kuruhusu ubadhirifu wa aina hii, hizi ni mali za watanzania, mnapopewa leseni muwe waaminifuna ndivyo Rais Samia Suluhu Hassan anasisitiza ili kuondokana na kero zisizo za lazima”Amesema Malenya.
Kiongozi huyo amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kuhakikisha wanakuwa waaminifu kwa kulipa kodi na kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Ole wao wanaotaka kutumia Ulanga kama kichochoro cha kukwepa kodi na kufanya biashara kwa njia ya magendo, wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria” amesema Malenya