Wachina kuwasaidia madiwani wa Dar pikipiki

Pikipiki.
Muktasari:
”Pikipiki hizi tutakazopata zitawasaidia madiwani wa jiji hili katika kuwa karibu na wananchi,” alisema Dk Massaburi na kuongeza kuwa “Hivi sasa tupo katika mazungumzo ya kupatiwa kamera hizi, huu ni mwanzo.”
Tayari viongozi wa Majiji ya Dar es Salaam na Zhejiang, wameshatiliana saini mkataba wa makubaliano.
Dar es Salaam.Jiji la Dar es Salaam linatarajia kupokea pikipiki 200 baada ya kusaini mkataba wa makubaliano na Jiji la Zhejiang nchini China.
Majiji hayo pia yapo katika na mazungumzo ya kulipatia Jiji la Dar es Salaam kamera za CCTV zitakazofungwa katika mitaa mbalimbali kwa ajili ya usalama wa wananchi na mali zao.
Hali kadhalika, usalama wa barabarani.
Akisaini mkataba huo mwishoni mwa wiki iliyopita , Meya wa jiji, Dk Didas Massaburi, alisema pikipiki hizo zitawasaidia madiwani kufanya shughuli zao kwa uwepesi zaidi.
”Pikipiki hizi tutakazopata zitawasaidia madiwani wa jiji hili katika kuwa karibu na wananchi,” alisema Dk Massaburi na kuongeza kuwa “Hivi sasa tupo katika mazungumzo ya kupatiwa kamera hizi, huu ni mwanzo.”
Kwa mujibu wa Dk Massaburi, hilo ni Jiji la nne nchini China, kuingia mkataba na Jiji la Dar es Salaam.
Alimhakikisha Naibu Meya Jiji la Zhejiang, Eu Ming Quang, kuwa watandaa mazingira mazuri ya maendeleo ya biashara kati ya nchi hizo mbili.
Aliwaomba wananchi wa China wasisite kuja kuwekeza nchini, kwa sababu mkataba huo umeshafungua ukarasa mpya wa fursa nyingi za biashara.
“Tunawaomba wasisite kuja kuwekeza hapa nchini kwetu, naona hivi sasa uhusiano wetu unazidi kuwa mzuri , tumekifikisha idadi ya majiji manne tuliyoingia nayo mkataba kwa ajili ya kuleta maendeleo,” alisema Dk Massaburi.
Kwa upande wake, Quang alielezea kufurahishwa kwake kuhusu kuingia mkataba huo.