Wabunge wamtaka Majaliwa arudi tena bungeni, suala la vyeo Mungu anapanga

Muktasari:
- Oktoba 2025, Tanzania inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na urais. Wabunge wamemwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kugombea na kurejea tena bungeni.
Dodoma. Mbunge wa Bunda (CCM), Mwita Getere amemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kugombea na kurudi tena bungeni bila kujali kama atapewa nafasi ya Waziri Mkuu au hatapewa.
Majaliwa ni Mbunge wa Ruangwa Mkoa wa Lindi na amekuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2015 na baada ya kuvunjwa kwa Bunge Juni 27, 2025, Majaliwa atakuwa ametumikia nafasi hiyo kwa miaka 10.
Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa ofisi ya Waziri Mkuu katika mwaka wa fedha 2025/26 bungeni jijini Dodoma, leo Alhamisi, Aprili 10, 2025, Mwita amesema Majaliwa anaweza kufuata nyayo za mawaziri wakuu, John Malecela na Edward Lowassa.
Malecela na Lowassa licha ya kuwa mawaziri wakuu na baada ya kuachia nafasi hizo, walirejea bungeni na kuwa wabunge wa kawaida.
“Tunamtaka Waziri Mkuu arudi bungeni, suala la vyeo Mungu anapanga, mbona tulikuwa na Waziri Mkuu mstaafu hapa Malecela na marehemu Lowasa lakini walikuwa wakikaa hapa,” amesema Getere.
Mbunge huyo amemzungumzia Waziri Mkuu kuwa amekuwa mtulivu kiasi ambacho hawezi kumlinganisha na mtu mwingine ndani ya Bunge.
Miongoni mwa sifa alizozitaja ni namna ambavyo amekuwa mtu wa kuwasikiliza wabunge na kuwasaidia kutatua matatizo yao bila kulinganisha na mtu mwingine.
Katika mchango wake, Mbunge wa Viti Maalumu Nusrat Hanje, amemtaja Waziri Mkuu kama mtu mwema na msikivu anayeweza kuwasikiliza watu wote bila kubagua.
Amesema hata yeye alipoingia kwa mara ya kwanza bungeni alikwenda kuzungumza naye na alimsikiliza vizuri na kumshauri namna gani afanye, hivyo anamuombea Mungu ambariki.
Mbali na Mwita, leo ikiwa ni siku ya kwanza ya kuchangia kwenye bajeti hiyo, wabunge wengi wakiwemo kutoka upinzani Salome Makamba na Aida Khenan walimwagia sifa Majaliwa wakisema amekuwa mtu mtulivu zaidi na msikilizaji kwa watu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Sumve (CCM), Masalali Mageni amesema ni bahati kwake kuwa na mtu kama Waziri Mkuu Majaliwa ambaye tangu kipindi cha kampeni ndiye alikwenda kumnadi kwa wapiga kura wake, hivyo anamuombea mema kwa mwenyezi Mungu.
Septemba 2024, Majaliwa akizungumza na wanachama wa CCM Jimbo la Ruangwa, baada ya kusema Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya anastahiki ‘mitano tena’ kisha akasema: “Na mimi nauhitaji tena ubunge. Nataka niendelee kuwawakilisha kwenye Bunge, nataka niendelee kuwasemea popote pale mnapotaka nikaseme.”