Wabunge waja juu kuhusu fidia athari za wanyama, wizara yataja mikakati
Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, akizungumza wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Ashatu Kijaji amewasilisha bajeti ambayo Sh62.3 bilioni zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo huku katika maeneo tisa ya kimkakati.
Dodoma. Kilio cha fidia kwa wananchi wanaopisha maeneo ya hifadhi kimeibua mjadala bungeni, huku wabunge wakitaka Serikali kueleza ni kwa nini imekuwa chanzo cha migogoro isiyokuwa na tija na kushindwa kuwalipa wananchi fidia stahiki, hali wanayodai inachangia kuwaingiza wananchi katika umasikini.
Mjadala huo umeibuka wakati wabunge wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, iliyowasilishwa jana bungeni ikiomba kuidhinishiwa Sh334.35 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, amewasilisha bajeti hiyo akieleza kuwa kati ya fedha hizo, Sh62.3 bilioni zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, yenye maeneo tisa ya kimkakati.
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), Joshua Nassari amesema Serikali imekuwa chanzo cha migogoro kati ya wananchi na hifadhi, huku ikitumia dhana ya uhifadhi kuwadhulumu wananchi na kuwaingiza kwenye umasikini.
Nassari ametoa mfano wa wananchi wa Bunda mkoani Mara, eneo alilowahi kulitumikia kama Mkuu wa Wilaya, akisema lilikumbwa na migogoro ya muda mrefu baada ya Serikali kuhamisha kata nzima kwa madai ya kupanua eneo la hifadhi.
“Nilipokuwa mkuu wa wilaya kule, nilisimamia kikamilifu na migogoro ikaisha baada ya wananchi kulipwa fidia. Lakini leo nasikia migogoro imeibuka tena. Hivi kuna nini serikalini? Maeneo mengine wananchi wanalipwa fidia ya Sh17, 000 hadi Sh3 milioni kisha wanaambiwa wahame. Je, hiyo si kuwaingiza Watanzania kwenye umasikini?” amehoji Nassari.
Amesema kwa upande wake hatakuwa tayari kuruhusu wananchi wahame kwa malipo ya kiwango hicho, akisisitiza kuwa wananchi hao walikuwa wakipigania ardhi yao hata kabla ya uhuru wa Tanganyika.
Mbunge wa Mbarali (CCM), Bahati Ndingo, alisema suala la fidia limekuwa donda ndugu ndani ya wizara hiyo, akidai kuwa chanzo kikubwa cha migogoro si wananchi bali ni Serikali yenyewe.
Ndingo amesema katika maeneo mengi, ikiwemo Mbarali, wananchi hawajawahi kuvamia hifadhi, bali Serikali ndiyo imekuwa ikitangaza upanuzi wa maeneo ya hifadhi na kuyafikisha kwa wananchi. Hata hivyo, amesema baada ya tathmini kufanyika, wananchi wameendelea kuahidiwa fidia bila kulipwa kwa muda mrefu.
Akitolea mfano Tangazo la Serikali (GN) Na. 754, alisema lilihusisha vijiji vingi, ikiwemo Masi na Mnonga, lakini hadi sasa miaka mitatu baadaye, wananchi hawajui hatima yao wala kuona dalili za kulipwa fidia.
“Ndani ya bajeti hii lazima patachimbika,” amesema Ndingo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Buchosa (CCM), Erick Shigongo ameeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la mashambulizi ya wanyama wakali, hususan mamba, akisema wamekuwa tishio kubwa kwa maisha ya wananchi.
Shigongo ameilaumu Serikali kwa kuonekana kujali zaidi ustawi wa wanyama kuliko maisha ya wananchi, akidai katika kipindi cha hivi karibuni watu 32 wamefariki dunia jimboni kwake kutokana na kushambuliwa na mamba.
Aidha, amegusia changamoto ya ukosefu wa weledi kwa baadhi ya watumishi wa wizara hiyo, akidai kuwa wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwapiga wananchi bila sababu za msingi. Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kilombero, Abubakar Asenga.
“Hawa askari wamekosa utu. Wanatumika kisiasa kwani hata kwangu waliwahi kunipiga virungu kwa kutumiwa na (anamtaja kiongozi). Sasa mmesababisha tembo wanaingia hadi mjini, lakini hamuwasaidii wananchi wetu. Hebu nendeni mkajenge uzio kule,” amesema Asenga.
Mapema, Waziri Dk Kijaji amesema katika hotuba yake kuwa moja ya vipaumbele vya wizara hiyo ni kuimarisha ulinzi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale kwa kuimarisha ushiriki wa jamii, kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori, kukabiliana na ujangili na kuzuia uharibifu wa mazingira.
Alisema katika juhudi za kutatua migongano kati ya binadamu na wanyamapori, wizara itaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kusimamia utatuzi wa migongano baina ya binadamu na wanyamapori wa mwaka 2025/26 hadi 2035/36.
Dk Kijaji amesema fedha pia zitatengwa kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa umeme wenye urefu wa kilomita 99 kutoka Kijiji cha Ming’ong’wa hadi Mto Guya katika Kijiji cha Ihusi (km 84) mpakani mwa Pori la Akiba la Maswa, pamoja na kutoka Loduare kuelekea Mbulumbulu (km 15) mpakani mwa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.