Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyumba ya wageni Mikumi iliyoteketea kwa moto yazinduliwa baada ya miaka 19

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba (mwenye tai) na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa hoteli ya Mikumi Wildlife Lodge iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi National Park mkoani Morogoro. Kushoto ni Mkurugenzi wa Wellworth Hotels and Lodges Limited, Gulam Ismail, na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima. Picha na Juma Mtanda


Muktasari:

  • Mikumi Wildlife Lodge iliyopo ndani ya Mikumi National Park imefunguliwa upya baada ya kukaa bila kufanya kazi kwa takribani miaka 19 tangu kuteketea kwa moto mwaka 2006, huku Serikali ikisema uwekezaji wa Sh26.8 bilioni uliowekwa katika ukarabati wake utaongeza ushindani wa utalii wa ukanda wa kusini na kuvutia watalii wa hadhi ya juu.

Morogoro. Baada ya kukaa kwa takribani miaka 19 tangu kuteketea kwa moto mkubwa mwaka 2006, Mikumi Wildlife Lodge iliyopo ndani ya Mikumi National Park imefunguliwa upya kufuatia uwekezaji wa Sh26.8 bilioni ulioweka sura mpya ya huduma za utalii katika ukanda wa kusini mwa Tanzania.

Uzinduzi wa Hoteli hiyo umezinduliwa jana na, Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba ambaye amesema maboresho ya miundombinu ya utalii pamoja na ongezeko la uwekezaji katika huduma za malazi yanaendelea kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi katika sekta ya utalii barani Afrika.

Dk Nchemba amesema Tanzania imepokea watalii zaidi ya milioni 5.9 mwaka 2025 huku mapato ya sekta hiyo yakifikia dola za Marekani bilioni 4.4, hali inayodhihirisha mchango mkubwa wa utalii katika kukuza uchumi wa Taifa.

“Uwekezaji huu utaongeza mvuto wa Hifadhi ya Mikumi kwa watalii wa hadhi ya juu na kuongeza muda wa wageni kukaa nchini, jambo litakalosaidia kukuza mapato ya sekta ya utalii,” amesema Dk Nchemba.

Amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) pamoja na kuimarisha miundombinu muhimu ya utalii ikiwemo viwanja vya ndege, malango ya kuingilia wageni, vituo vya taarifa na huduma za malazi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali imetoa zaidi ya Sh35 bilioni kwa ajili ya kuboresha huduma mbalimbali za utalii katika Mikumi National Park, fedha zilizotumika kujenga uwanja wa ndege unaoendelea, malango mapya mawili, nyumba za kulala wageni, maeneo ya kupiga mahema na sehemu za mapumziko ya watalii.

Dk Nchemba amesema pia mradi wa treni ya kisasa ya SGR umefungua fursa kubwa ya ukuaji wa utalii katika ukanda wa kusini kutokana na urahisi wa usafiri kupitia stesheni za Morogoro na Kilosa.

Kutokana na hali hiyo, ameiagiza TANAPA pamoja na wizara husika kuboresha miundombinu ya kuunganisha watalii kutoka stesheni hizo kwenda hifadhini ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea eneo hilo.

“Tanzania imejipanga kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030, hivyo wawekezaji waliopatiwa hoteli  zilizokuwa za Serikali wanapaswa kuhakikisha wanafanya maboresho yatakayokidhi ushindani wa kimataifa kuelekea AFCON 2027,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji amesema maendeleo ya sekta ya utalii duniani yanategemea ubora wa miundombinu pamoja na huduma za kisasa za malazi kwa watalii.

Dk Kijaji amesema idadi ya vyumba vya kulala wageni nchini imeongezeka kutoka 122,532 mwaka 2021 hadi 147,545 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 20.4 huku vitanda vikiongezeka kutoka 132,676 hadi 158,469 katika kipindi hicho.

“Mnamo mwaka 2025 Tanzania ilipokea watalii 5,905,455 sawa na ongezeko la asilimia 7.2 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Watalii wa ndani walifikia 3,610,960 kutoka 788,933 mwaka 2021,” amesema Dk Kijaji.

Amesema watalii wa kimataifa wameongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia 2,294,495 mwaka 2025 huku mapato ya utalii yakiongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi dola bilioni 4.4 mwaka 2025.

Dk Kijaji amesema Mikumi Wildlife Lodge ni moja ya hoteli zilizokuwa zikimilikiwa na Serikali tangu mwaka 1970 wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Julius Nyerere kabla ya kuathiriwa na moto mkubwa mwaka 2006 uliosababisha kusimama kwa huduma kwa muda mrefu.

Kupitia uwekezaji mpya wa kampuni ya Wellworth Hotels and Lodges Limited, loji hiyo sasa imekarabatiwa kwa kiwango cha kisasa na ina vyumba 48 vyenye uwezo wa kulaza wageni 96 kwa wakati mmoja.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Gulam Ismail amesema kampuni hiyo ya wazawa imewekeza zaidi ya Sh640 bilioni katika miradi ya hoteli   utalii nchini.

Gulam amesema uwekezaji huo haulengi watalii wa kutoka nje pekee bali pia kukuza utalii wa ndani kwa kuweka viwango rafiki vitakavyowawezesha Watanzania wengi kumudu gharama za kufanya utalii.

“Miradi yetu yote ikikamilika tutakuwa na zaidi ya vyumba 1,400 vyenye uwezo wa kulaza wageni zaidi ya 2,800 kwa wakati mmoja pamoja na kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 4,200,” amesema Gulam.

Amesema pamoja na mafanikio hayo, bado ukanda wa kusini unahitaji maboresho makubwa ya miundombinu ili kuongeza muda wa watalii kukaa katika hifadhi hizo.

Kwa mujibu wa Gulam, watalii wengi wanaotembelea Mikumi National Park hutokea Zanzibar lakini hukaa kwa muda mfupi kutokana na changamoto za miundombinu pamoja na eneo dogo la “game drive”.

Gulam ameshauri Serikali kuipa kipaumbele barabara inayounganisha Nyerere National Park na Mikumi ili watalii waweze kutembelea hifadhi zote mbili kwa urahisi na kuongeza muda wa kukaa katika ukanda wa kusini.

Amesema uwepo wa reli ya kisasa ya SGR umeifanya Mikumi kuwa lango muhimu la utalii wa ukanda wa kusini na kwamba maboresho zaidi ya miundombinu yataifanya Tanzania kuongeza ushindani wake katika soko la utalii duniani.