Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge waibana Serikali tozo kwa wajawazito wanapojifungua

Muktasari:

  • Mbunge huyo ameuliza swali la nyongeza akihoji vifaa vinavyoagizwa na kununuliwa, lakini vinabaki baada ya wanawake kujifungua, vinapelekwa wapi?

Dodoma. Sakata la wanawake wajawazito kutozwa fedha wakati wa kujifungua limeibua mjadala bungeni leo na kusababisha baadhi ya wabunge kuomba mwongozo wa Spika ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusu utekelezaji wa sera ya matibabu bure kwa wajawazito.

Mapema leo Ijumaa, Mei 16, 2025, Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole (CCM), amehoji bungeni iwapo bado inatekelezwa Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007, inayotamka kuwa huduma za kujifungua kwa kina mama wajawazito zinapaswa kutolewa bure.

Katika swali lake la nyongeza, Mwenisongole pia ameuliza kuhusu hatma ya vifaa tiba vinavyoagizwa au kununuliwa kwa ajili ya huduma hizo, akitaka kujua vinakwenda wapi baada ya wanawake kujifungua.

Swali hilo liliibua mjadala mkali ndani ya Bunge, na kusababisha wabunge wengi kusimama wakitaka kuuliza maswali ya nyongeza kuhusu uhalali wa tozo hizo.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alitaka kujua sababu ya wananchi kutozwa fedha ilhali Serikali hutenga bajeti maalum kwa ajili ya huduma hizo. "Fedha hizo zinaenda wapi hadi wananchi walipe?" alihoji kwa msisitizo.

Mbunge wa Viti Maalum, Ferister Njau, alihoji kwa nini Serikali isitoe tamko la kuifuta Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 iwapo haitekelezwi ipasavyo, akidai hali ya sasa inaonesha kuwa utekelezaji wake umedorora.

Kwa upande wake, Mbunge wa Momba, Condester Sichalwe (CCM), alitaka kujua ni kwa nini Serikali imeshindwa kuutekeleza na kuusimamia kikamilifu mpango huo muhimu, ambao unalenga kupunguza vifo vya wajawazito nchini.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, alieleza kuwa Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 bado ipo na inaendelea kutumika kama mwongozo wa utoaji wa huduma za afya nchini.

Dk Mollel amesema kwa sasa Wizara ya Afya iko katika hatua za mwisho za kupitia upya sera hiyo kwa lengo la kufanya maboresho yatakayoiwezesha kuendana na mahitaji ya sasa na changamoto zilizopo katika sekta ya afya.

"Hata hivyo, kuanza kutumika kwa Bima ya Afya kwa Wote itakuwa suluhisho la kudumu la tatizo hili na kumaliza malalamiko ya wananchi," amesema Dk Mollel.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri amesema kiasi cha Sh200 bilioni zinazotengwa kwa ajili ya huduma ya wajawazito kujifungua hazitoshi kwani ili ziweze kutosheleza inapaswa zitengwe jumla ya Sh227 bilioni.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Wabunge Esther Matiko na George Mwenisongole wameomba mwongozo wa Spika wakihoji majibu ya Serikali kwa changamoto hiyo kubwa wananchi lakini majibu wamesema hayajitoshelezi.

Kwa upande wake Matiko amehoji fedha zinazotozwa kwa wajawazito zinapelekwa wapi kwani Bunge haliwezi kuzihoji.

Spika Dk Tulia Ackson ametoa mwongozo akiomba kulipitia upya swali hilo pamoja na majibu yake ndipo atatoa mwongozo wake kama litapaswa kujibiwa upya ama vinginevyo.