Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajawazito, watoto wakiona cha moto Katoro

Mkazi wa Katoro, Juma Nyahinga, akizungumza katika mkutano huo kuhusu kero za wananchi. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

Wananchi wa Kata ya Ludete, Mji Mdogo wa Katoro, mkoani Geita wamemweleza Mkuu wa Mkoa huo, Martin Shigella juu ya adha wanayokutana nayo katika Kituo cha Afya Katoro.

Geita. Wananchi wa Kata ya Ludete, Mji Mdogo wa Katoro, mkoani Geita wamemweleza Mkuu wa Mkoa huo, Martin Shigella juu ya adha wanayokutana nayo katika Kituo cha Afya Katoro.

Wamemweleza RC Shigela jinsi wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanavyotozwa fedha kwa ajili ya kumuona daktari na wakitakiwa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya dawa kinyume na sera ya afya.

Wametoa kilio hicho leo Jumatano, Machi 6, 2024 katika mkutano wa RC Shigella  anayefanya mikutano ya hadhara ya kusikiliza kero za wananchi kwenye ngazi za kata.

Juma Nyahinga, Mkazi wa Ludete amedai mwishoni mwa mwezi uliopita alimzika mtoto wake mdogo, baada ya kuugua ghafla na kumkimbiza kituoni hapo akiwa mahututi na alipofika alimuomba daktari aliyekua akimhudumia mgonjwa mwingine kumsaidia mwanaye kwa kuwa ana hali mbaya lakini alikataa na baada ya muda mwanawe alifariki dunia.

“Juzi nimezika mtoto nilimleta hapa akiwa mahututi, nilipofika nilimkuta daktari anamhudumia mtu mwingine ambaye hakuwa amezidiwa. Nikamuomba anisaidie maana hali ya mwanangu ilikuwa mbaya alinijibu usinipelekeshe nikiwa nimekaa nasubiri nifikiwe mwanangu alifariki akiwa mikononi mwangu,  yumkini angemhudumia labda angemuokoa, inaumiza sana,” amedai Nyahinga

Naye Asha Hussen na Hadija Mlekwa kwa nyakati tofauti,  wamedai wanapofika kituoni hapo hutakiwa kulipa Sh5000 kumuona daktari na baadaye kutakiwa kwenda kununua dawa kwenye duka la dawa lililopo kituoni hapo kinyume na kauli zinazotolewa na viongozi wa Serikali kuwa huduma kwa mjamzito na mtoto ni bure.

“Mkuu wa Mkoa mnasema huduma kwa mama mjamzito na mtoto ni bure, lakini ukifika hapa hata kama ni usiku una mtoto mgonjwa utaambiwa ulipe Sh5000.

Ukilipa utaambiwa mwache mgonjwa hapa ukanunue dawa, ukiomba hata paracetamol wanasema hakuna sasa nimefika usiku hospitali hata paracetamol hakuna hela zetu wanachukua za nini,” ameuliza Asha

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita, Modest Burchard amekiri kuwepo kwa changamoto katika kuwahudumia wajawazito na watoto na kusema wakati mwingine daktari humuandikia mgonjwa dawa ya kununua kutokana na kituo cha afya au zahanati kutokuwa na dawa hizo.

“Kweli kuna kero lakini kwenye zahanati kuna dawa ambazo hazipo kutokana na uwezo vivyo hivyo kwenye vituo vya afya na anapofika mjamzito akiambiwa dawa hii haipo analazimika kwenda kuinunua.

Kuhusu kituo cha afya kutokuwa na dawa hata Paracetamol, Burchard ameomba kufuatilia ili kujua sababu kwa kuwa zipo dawa muhimu ambazo hazipaswi kukosekana kwenye vituo vyovyote vya kutolea huduma.

Akizungumza na wananchi hao, RC Shigella amesema changamoto ya kina mama wajawazito kutakiwa kulipa sio kwenye Kituo cha afya Katoro pekee na kumtaka mganga mkuu wa wilaya hiyo, kuandika matangazo ya kuwataka watumishi kwenye vituo vya kutolea huduma kutowatoza fedha na kuyaweka kwenye mbao za hospitali.

“Hayo matangazo yawe na namba za simu ili mjamzito anapofika hapa na kutakiwa kulipia aweze kupiga simu na hatua zichukuliwe haraka,” amesema Shigella.

Kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ni miongoni mwa vipaumbele vya Wizara ya Afya kwa mwaka 2023/24, lengo likiwa ni kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

Hata hivyo bado kumekuwa na utata juu ya matibabu bure kwa makundi maalum wakiwemo wajawazito, watoto na wazee wakidai kuendelea kutozwa fedha.