Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vyama vilivyojipambanua kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa

Muktasari:

  • Kadri siku zinavyokaribia ndivyo vyama vinavyoweka wazi misimamo yao kuelekea kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na mpaka sasa kwa sehemu kubwa vimeahidi kushiriki.

Dar es Salaam. Siku zinazidi kuyoyoma, ilikuwa miaka, ukawa mwaka na sasa ni miezi mitatu na siku kadhaa kuelekea kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa.

Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kama ilivyotangazwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), unahusisha kuwapata viongozi wa ngazi ya vijiji, mitaa na vitongoji.

Kwa kadri siku zinavyokaribia na ndivyo vyama mbalimbali vinavyoweka wazi misimamo yao kuelekea kushiriki uchaguzi huo na mpaka sasa kwa sehemu kubwa vimeahidi kushiriki.

Mbali na kushiriki, kila chama kinafanya linalowezekana kupata ushindi katika nafasi hizo, ikiwa ndiyo malengo ya kila chama cha siasa.

Licha ya upinzani juu ya Tamisemi kusimamia uchaguzi huo, vyama vyote vikiwemo vya upinzani vimepanga kushiriki kwa mbinu mbalimbali kuhakikisha vinapata ushindi katika nafasi zote.

Ahadi za vyama hivyo, zinakuja kipindi ambacho mapema baada ya uchaguzi kama huo wa mwaka 2019, vililalamikia kufanyiwa kile walichokiita mchezo mchafu wa kuenguliwa kwa wagombea wake.

Mazingira hayo yalivifanya baadhi ya vyama kuahidi kukoma kushiriki uchaguzi huo hadi pale Serikali itakapobadili sheria za uchaguzi huo na kuondoa jukumu la usimamizi wa uchaguzi huo kwa Tamisemi.

Mabadiliko ya sheria yamefanyika, lakini jukumu la usimamizi wa uchaguzi huo limebaki kwa Tamisemi, huku vyama vikionyesha msimamo wa kushiriki.

Tofauti na uchaguzi kama huo wa mwaka 2019 ambao vyama vya upinzani vya Chadema, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, NLD na Chauma vilijitoa na hivyo wagombea wengi wa CCM walipita bila kupingwa, uchaguzi wa mwaka huu hali inatarajiwa kuwa tofauti.

Hiyo inatokana na namna vyama vilivyojinasibu kushiriki uchaguzi huo, huku vikiahidi bila kujali mazingira yoyote vitashiriki kinyang’anyiro hicho.


ACT Wazalendo

Kuelekea uchaguzi huo, Chama cha ACT-Wazalendo kimeazimia kusimamisha wagombea kwenye mitaa, vijiji na vitongoji vyote nchini katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa serikali za mitaa.

Maazimio hayo ni kwa mujibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyoketi Agosti 25, 2024 ambayo pamoja na mambo mengine kimeazimia kulitekeleza hilo kama sehemu ya maandalizi yake kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Akieleza maazimio hayo baada ya kikao cha Halmashauri Kuu, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Shangwe Ayo amesema sekretarieti ya chama hicho imeelekezwa kuhakikisha inalitimiza hilo.

“Kikao hicho kimeielekeza Sekretarieti ya chama kutumia mtandao wetu mpana wa wanachama kuhakikisha tunasimamisha wagombea ngazi zote za serikali za mitaa bila kuacha hata kitongoji, kijiji na mtaa,” amesema.


Chadema

Ukiachana na maazimio hayo ya ACT-Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nacho kimeshatoa msimamo wake wa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Msimamo huo ulitolewa Julai 17, 2024 na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipokuwa katika mkutano wa hadhara jijini Arusha.

Katika mkutano huo, Mbowe alisema chama hicho hakitasusia uchaguzi wowote, badala yake kitashiriki kuhakikisha kinawaweka madarakani wagombea wake.

Kauli hiyo ilifuatiwa na uzinduzi wa oparesheni iliyopewa jina la kupinga uchafuzi katika uchaguzi wa serikali za mitaa ‘Kucha’ inayoendeshwa na chama hicho.

Msingi wa oparesheni hiyo ni kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema kuwa watalinda uchaguzi huo kuhakikisha wagombea wao hawaenguliwi.

“Hatutoki hapo tunasubiri matokeo, hakuna kitu kina nguvu kama kujiamini, hatutaibiwa kura hakuna mgombea wetu kuenguliwa. Mimi siwezi kuwa kwenye mitaa yote, hii kazi tunaweza kuifanya kwa pamoja,” alisema Lema.


CCM

Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla akiwa katika ziara yake kwenye wilaya mbalimbali za Dar es Salaam, alisisitiza ushiriki wa wananchi katika uchaguzi huo.

Ingawa alikipigia chapuo chama chake kupigiwa kura zaidi, alisema ni muhimu wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwanza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na pia wawanie nafasi katika uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa Makala, umuhimu wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaakisiwa na umuhimu wa viongozi wa ngazi hizo.

Aliijenga hoja hiyo akirejea alipokuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, akisema mafanikio yake ya kukabiliana na matukio ya uhalifu wa ‘Panyarodi’ yalitokana na ushirikiano wake na viongozi wa serikali za Mitaa.

“Nilipokuwa mkuu wa mkoa, moja ya mitihani migumu lilikuwa suala la panyarodi, nilipambana nao sana, lakini nilifanikiwa baada ya kushirikiana na viongozi wa ngazi ya serikali za mitaa, hivyo muhimu tuwachague ili watusaidie,” alisema Julai alipokuwa wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam.