Prime
Vispika vimerudi tena Kariakoo, DC Ilala atoa msimamo
Muktasari:
- Kurejea kwa matumizi ya vifaa hivyo kunakuja wiki kadhaa tangu Serikali ya Wilaya ya Ilala ifanye operesheni ya kuviondoa na kutangaza marufuku ya matumizi ya spika hizo.
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kufanya operesheni na kuzuia matumizi ya spika katika maeneo mbalimbali ya Soko la Kariakoo, baadhi ya wafanyabiashara wameanza upya kutumia vifaa hivyo kutangazia biashara.
Kurejea kwa matumizi ya vifaa hivyo kunakuja wiki kadhaa tangu Serikali ya Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, ifanye operesheni ya kuviondoa na kutangaza marufuku ya matumizi ya spika hizo.
Kwa mujibu wa Serikali, uamuzi wake wa kuzuia matumizi ya spika hizo unatokana na malalamiko ya wananchi kwamba kelele za spika hizo zinashusha hadhi ya Soko la Kariakoo.
Uamuzi huo wa Serikali kufanya operesheni na kuzuia matumizi ya spika hizo ulitokana na ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kuhusu athari zake katika mwili wa binadamu kwa mujibu wa madaktari.
Katika ripoti hiyo, ilibainika kuwa masoko ya Kariakoo, Tandika na Karume (Mchikichini) yana matumizi makubwa ya spika hizo na kusababisha usumbufu kwa baadhi ya wateja, wafanyabiashara na wapita njia.
Vimerudi tena bwana
Jana, Jumanne Juni 23, 2026, Mwananchi ilitembelea Soko la Kariakoo na kushuhudia wafanyabiashara wakitumia spika hizo baada ya kuviacha kwa siku kadhaa kufuatia Jiji la Dar es Salaam kufanya operesheni.
Katika mitaa ya Aggrey, Kongo, Msimbazi na Mchikichi ya Kariakoo, kumeshuhudiwa kelele zinazotokana na spika na vipaza sauti vinavyotumiwa na wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
Wakati huo huo, Mtendaji wa Kata ya Kariakoo, Tatu Nyamoga, amesema, “Kwa lugha fupi, suala hilo lisiwatishe. Operesheni haiwezi kufanywa kwa siku moja kwa sababu jiji ni kubwa na mchakato unaendelea. Hata wale ambao hawajafikiwa watafikiwa.”
Spika hizo, zikiwemo za kutumia flashi na vipaza sauti vinavyotumiwa na wafanyabiashara wakubwa na wadogo kutangaza bidhaa zao kupitia matangazo yaliyorekodiwa, zimekuwa zikisababisha kelele kubwa katika maeneo ya biashara.
Juni 2, 2026, Jiji la Dar es Salaam lilianza operesheni endelevu ya kuziondoa spika hizo katika mitaa ya Kariakoo ya Msimbazi, Narung’ombe, Mchikichi, Kongo na Aggrey.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara waliorejea matumizi ya spika hizo kwa staili tofauti, ikiwemo kuzificha kiasi kwamba ni nadra kuziona, badala yake sauti pekee ndiyo inasikika.
Mwananchi imebaini spika hizo zikifichwa katikati ya nguo au viatu kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa hizo kwa kuzipanga katika meza pembezoni au katikati ya barabara za mitaa mbalimbali ya Kariakoo ukiwamo wa Kongo.
Baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia vipaza sauti huvificha katika mifuko mbadala na kuvichomoza katika nguo au viatu vilivyowekwa kwenye meza kwa ajili ya mauzo.
Lakini kwa wafanyabiashara wenye fremu, hasa wa ghorofani, wao wanajiachia kwa kuzining’iniza juu au mbele ya maduka yao wakitangaza bidhaa mbalimbali, ikiwemo pochi, ili kuwavutia wateja kuzinunua.
Mmoja wa wafanyabiashara wa Mtaa wa Mchikichi, John Daudi, amesema baadhi yao wamekuwa wakikaidi na kutotekeleza maagizo ya jiji ya kutotumia spika hizo kwa sababu zimekuwa kero kwa wanunuzi na wapita njia.
“Hali ni kama unavyoiona. Sisi tumetii, lakini wenzetu bora liende, hawana cha kupoteza. Ni kelele mwanzo mwisho kuanzia asubuhi hadi jioni. Tunapata kero kubwa sisi. Serikali iangalie namna ya kutusaidia,” amesema Daudi.
Hata hivyo, Daudi anasema kuna muda mwingine anawaelewa wafanyabiashara wanaotumia spika hizo, hasa wale wanaomiliki fremu za juu, akisema ni njia pekee ya kuvuta wateja.
“Jiografia ya Kariakoo, mteja ni rahisi kununua bidhaa kwenye fremu za chini, lakini zile za juu bila kumtangazia hapandi ng’o. Sasa hapo ndipo tatizo linapoanzia, ndiyo maana hawa wakikatazwa wanarejea kuzitumia upya,” ameeleza Daudi.
Naye mfanyabiashara wa Mtaa wa Aggrey, Yasin Abdulswamadu, amesema mara kwa mara maofisa wa jiji wanafanya operesheni lakini ni kama vile wafanyabiashara wameweka pamba masikioni mwao.
“Ni juzi tu hapa walipita na kuzikamata hasa zile spika za vipaza sauti, lakini jamaa wamezinunua na kuanza upya. Tunapata shida sisi wenye fremu; kwanza wanazuia barabara, pili wanatusababishia kelele kwa spika zao,” amesema.
Mmoja wa wateja waliozungumza na Mwananchi, Aisha Juma, amelitaka Jiji la Dar es Salaam kuongeza kasi katika utekelezaji wa operesheni ya kuziondoa spika hizo ili Kariakoo iwe mfano wa kuondokana na kelele zinazotokana na spika.
“Mwanzoni mwa operesheni hii kulikuwa na utulivu katika baadhi ya mitaa ya Kariakoo, sasa hali inarejea kama zamani. Jiji lisichoke wala kukata tamaa; walianza vizuri, sasa waongeze kasi,” amesema Juma.
Kauli ya DC
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameliambia Mwananchi jana Jumanne Juni 23, 2026 kuwa hali inajitokeza, lakini akisisitiza operesheni ya kuwaondoa ni endelevu.
Alipoulizwa wanachukua hatua gani kuhusu hatua hiyo, “Tutafanya tathimini, tutakuja na nini kifanyike,” ameeleza Mpogolo.