Viongozi wajitokeza mazishi ya Balozi Mwapachu Tanga

Muktasari:
- Mwili wa mwanadiplomasia Balozi Juma Mwapachu utazikwa mchana wa leo Jumapili, Machi 30, 2025 kijijini kwake Pande wilayani Tanga.
Tanga. Shughuli za mazishi ya Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Juma Mwapachu, zimeanza nyumbani kwa baba yake, maeneo ya Chumbageni jijini Tanga, huku viongozi mbalimbali wakiwasili na kutoa salamu za pole kwa familia.
Shughuli za safari ya mwisho ya mwanadiplomasia huyo zimeanza asubuhi ya leo, Jumapili, Machi 30, 2025, ambapo maziko yatafanyika mchana kijijini kwake Pande wilayani Tanga.

Balozi Mwapachu (82) alifariki dunia Machi 28, 2025, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Miongoni mwa viongozi waliofika ni Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, na mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Masinde Bwire.
Dk Bwire amesema jumuiya hiyo imepoteza muasisi mahiri na watamuenzi kwa yote aliyoyaasisi.
Zitto amemwelezea Balozi Mwapachu kama mwalimu wake katika masuala mbalimbali, ikiwemo ya kisiasa, na kusema amekuwa akimshauri kwenye shughuli zake za kisiasa.
Kisomo cha kumuomba kimeongozwa na Mufili wa Taasisi ya Kiislamu ya Maawal, Mohamed Halili, akishirikiana na masheikh mbalimbali wa Mkoa wa Tanga.

Balozi Juma Mwapachu alizaliwa Septemba 27, 1942, jijini Mwanza, Tanzania.
Alikuwa mwanasiasa na Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), nafasi aliyoirithi kutoka kwa Amanya Mushega wa Uganda, aliyemaliza kipindi chake cha miaka mitano Machi 24, 2006.
Balozi Mwapachu alipendekezwa kwa nafasi hiyo na Rais wa Tanzania wa wakati huo, Jakaya Kikwete. Alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa EAC na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC Aprili 4, 2006.
Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Balozi wa Tanzania mwenye mamlaka kamili na mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).
Balozi Mwapachu alikuwa mhitimu wa Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliyohitimu mwaka 1969.
Pia alikuwa na Diploma ya Uzamili katika Sheria za Kimataifa, Taasisi za Kimataifa, na Diplomasia kutoka Chuo cha India cha Sheria za Kimataifa na Diplomasia kilichopo New Delhi.
UDSM ilimtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi mwaka 2005. Pia alipata Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda.
Balozi Mwapachu alikuwa mwanasheria kitaaluma na alipitia taaluma mbalimbali zikiwamo za benki, maendeleo ya vijijini, diplomasia, na sekta binafsi.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa EAC, aliwahi kufanya kazi na Wizara ya Serikali za Mitaa na Utawala wa Mikoa katika miaka ya 1970.
Alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa kati ya mwaka 2002 hadi 2006.
Balozi Mwapachu aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi za wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na za mashirika ya umma, ikiwemo Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB).
Alishika wadhifa wa Kamishna wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC). Alikuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki.
Aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Biashara ya Nje na Baraza la Uongozi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Balozi Mwapachu aliwahi kuhudumu kama Mjumbe wa Baraza la Uongozi la Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo.
Alihudumu kama mjumbe wa tume mbalimbali zilizoundwa na Rais na alishiriki katika kuandaa Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025.
Balozi Mwapachu aliwahi kujitoa CCM Oktoba 2015 na alijiunga na upinzani kabla ya kurejea kwenye chama hicho mwaka 2016, ikiwa ni miezi mitano baada ya kujiondoa.