Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi wa dini wapewa kibarua kukabili wimbi la talaka nchini

Msajili wa asasi za kiraia nchini Emmanuel Robert akitembelea kazi za mikono zinazotengenezwa na wanafunzi wa kituo cha babtisti klasta ya namanga chini ya kituo cha compassion international Tanzania.

Muktasari:

  • Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2024 inaonyesha kuwa kiwango cha talaka nchini kiliongezeka kwa asilimia 93.7 mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2020, huku takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zikionyesha idadi ya talaka zilizosajiliwa mahakamani zikiongezeka kutoka kesi 711 mwaka 2022 hadi kesi 1,172 mwaka 2024 .

Arusha. Viongozi wa dini wametakiwa kuongeza juhudi katika kukabiliana na ongezeko la kuvunjika kwa ndoa na matukio ya talaka nchini kutokana na kuwa tishio kwa malezi ya watoto na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa leo Juni 2, 2026 na Msajili wa Asasi za Kiraia Tanzania, Emanuel Robert wakati akizungumza na viongozi wa makanisa wanaotekeleza programu ya malezi na makuzi ya watoto chini ya mwamvuli wa shirika la kimataifa la Compassion Tanzania, wakati wa ziara yake katika Kituo cha Huduma ya Maendeleo ya Mtoto na Kijana cha Baptist Longido.

Robert amesema familia ndiyo msingi wa Taifa imara, hivyo kuongezeka kwa migogoro ya kifamilia na talaka kunapaswa kutazamwa kama changamoto inayohitaji ushirikiano wa viongozi wa dini, Serikali na jamii kwa ujumla.

“Taifa bora hujengwa juu ya familia bora. Tunapaswa kutafakari kwa kina kuhusu ongezeko la talaka nchini kwa sababu linaathiri malezi na makuzi ya watoto ambao ndio viongozi tegemewa wa kesho, tukipuuza suala hili tunaweka hatarini mustakabali wa Taifa,” amesema.

Wito huo unakuja wakati takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa changamoto ya talaka nchini inaendelea kuongezeka kwa kasi na kuzua wasiwasi kuhusu ustawi wa familia na malezi ya watoto.

Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2024 inaonyesha kuwa kiwango cha talaka nchini kiliongezeka kwa asilimia 93.7 mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2020, huku takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zikionyesha idadi ya talaka zilizosajiliwa mahakamani zikiongezeka kutoka kesi 711 mwaka 2022 hadi kesi 1,172 mwaka 2024 .

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Dorothy Gwajima kwenye hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2025/2026, alisema sababu kuu zinazochangia kuvunjika kwa ndoa ni migogoro kuhusu majukumu ya kifamilia, uzinzi, kutelekezana, ukatili wa ndoa pamoja na changamoto za kiuchumi zinazozikabili familia nyingi.

Vilevile, takwimu za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) zinaonyesha kuwa idadi ya talaka 866 zilisajiliwa mwaka 2024 ikilinganishwa na talaka 447 zilizorekodiwa mwaka 2022.

Robert anaeleza kuwa watoto wengi wanaokulia katika mazingira yenye migogoro ya kifamilia hukumbana na changamoto za kisaikolojia, kielimu na kijamii ambazo huathiri ukuaji wao na uwezo wa kutimiza ndoto zao.

Katika risala iliyowasilishwa na Mchungaji Ndefiyo Skawa kwa niaba ya Klasta ya Namanga inayojumuisha makanisa matano yanayoshirikiana na Compassion International Tanzania, amesema huduma za maendeleo ya mtoto na kijana zimekuwa zikiwafikia watoto kutoka familia zenye uhitaji bila kujali dini, kabila au asili yao.

Tangu kuanza kwa programu hiyo mwaka 2001, watoto 1,169 wameandikishwa katika klasta hiyo na kunufaika na huduma mbalimbali za elimu, afya, malezi na maendeleo ya kiuchumi.

Skawa amesema kituo hicho hutumia zaidi ya Sh168 milioni kwa mwaka, kugharamia huduma za watoto na vijana ikiwemo elimu, bima za afya, lishe, mafunzo ya stadi za maisha na ulinzi wa mtoto.

Amesema kupitia programu hiyo, vijana wengi wamewezeshwa kupata elimu na ujuzi wa kujiajiri katika maeneo ya kompyuta, ushonaji, upishi, ususi, urembo pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.

“Aidha, kituo kimekuwa kikiwezesha wazazi na walezi kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali na mitaji ya biashara ambapo 117 wamepatiwa mitaji ya biashara yenye thamani ya Sh1.5 milioni kila mmoja huku vikundi vya kuweka na kukopa vya wazazi vikifikisha mtaji wa zaidi ya Sh32 milioni,” amesema.

Amesema Wilaya ya Longido bado inakabiliwa na changamoto zinazowaathiri watoto na vijana, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, ndoa za utotoni, ukeketaji, utoro shuleni pamoja na changamoto za malezi kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kupata muda wa kutosha wa kuwalea watoto wao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Compassion International Tanzania, Merry Lema amesema lengo kuu la shirika hilo ni kumkomboa mtoto na kijana kutoka katika mzunguko wa umaskini kwa kuwapatia fursa za elimu, afya na maendeleo ya kiuchumi.

“Tunataka kuona watoto wakikua katika mazingira salama, wakipata elimu bora na hatimaye kuwa watu wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa hili baadaye,” amesema.