Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unafahamu hili kuhusu talaka? msikie Sheikh Walid

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Kawambwa

Muktasari:

  • Asema baadhi ya sababu zinazotolewa na wanandoa wanaotaka kuachana zinaonyesha kuwa watu wengi wanaingia kwenye ndoa bila kuelewa wajibu, malengo na misingi yake.



Dar es Salaam. Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Kawambwa amesema ongezeko la talaka zinazotolewa kwa sababu zisizo na msingi ni ishara ya kuporomoka kwa maadili na uelewa wa dhana halisi ya ndoa katika jamii ya sasa.

Amesema baadhi ya sababu zinazotolewa na wanandoa wanaotaka kuachana zinaonyesha kuwa watu wengi wanaingia kwenye ndoa bila kuelewa wajibu, malengo na misingi yake.

Sheikh Walid ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanya na kituo cha redio cha Clouds FM ambapo ameeleza masuala mbalimbali ikiwemo changamoto za ndoa zinazofikishwa ofisini kwake.

“Mimi nakutana na kesi kila siku. Mtu anasema anataka kumpa talaka mke wake kwa sababu hajampikia, mwingine analalamika hafunikwi blanketi akiwa amelala. Hayo siyo malengo ya ndoa,” amesema.

Amesema ndoa haiwezi kujengwa katika misingi ya huduma ndogo ndogo au matarajio ya upande mmoja pekee, bali inahitaji uvumilivu, maadili na uelewa wa pamoja.

“Unamuoa mwanamke kwa sababu akupikie tu? Hakuna hilo. Ndoa ina maana kubwa zaidi ya hayo,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Sheikh huyo, tatizo kubwa lililopo sasa ni vijana wengi kuingia kwenye ndoa kwa kufuata hisia za muda mfupi na mvuto wa nje badala ya kuzingatia maadili na msingi wa familia.

“Zamani kulikuwa na mifumo ya malezi kama jando na unyago ambayo iliwafundisha vijana wajibu wao ndani ya familia. Leo watu wanaingia kwenye ndoa bila kuelewa kwa nini wanaoa au kuolewa.

“Hata wazazi wa zamani ambao hawakuwa na elimu kubwa rasmi waliweza kuwalea watoto wao katika misingi ya heshima, uvumilivu na uwajibikaji ndani ya ndoa, hali iliyosaidia ndoa nyingi kudumu kwa miaka mingi.

“Watu wanaoa kwa mihemko. Anaangalia uzuri, weupe au umbo, lakini vitu hivyo havidumu. Baadaye yale yaliyokuvutia yakibadilika ndiyo mnaanza kutafutiana sababu,” amesema.


Aonya mizaha ya talaka


Sheikh Walid pia ameonya kuhusu tabia ya baadhi ya wanandoa kuchezea maneno ya talaka katika migogoro ya ndoa, akisema hatua hiyo imechangia baadhi ya watu kuishi pamoja bila kujua kuwa ndoa zao tayari zimevunjika kidini.

Amesema talaka katika dini ya Kiislamu si jambo la mzaha na kwamba neno hilo likitamkwa, hata kwa hasira au masihara, lina uzito mkubwa wa kisheria na kidini.

Sheikh Walid ameongeza kuwa baadhi ya wanandoa wanaendelea kuishi pamoja bila kutambua kuwa walishavunja ndoa zao kutokana na kutamka talaka kwa wepesi wakati wa ugomvi.

Amesema badala ya mwanaume kukimbilia kutoa talaka, anaweza kutumia njia za usuluhishi ikiwemo kumrudisha mke kwa wazazi au walezi wake kwa muda ili kutoa nafasi ya kutafuta suluhu ya tatizo lililopo.

“Wakati mwingine ni vizuri kupeana muda wa kutulia na kutafuta suluhu kupitia familia au wazee wa pande zote kuliko kukimbilia kuvunja ndoa,” amesema.

Mbali na hilo, Sheikh huyo alizungumzia changamoto ya wanandoa kutarajia kumfahamu mwenza wao kwa muda mfupi, akisema tabia za binadamu hujitokeza hatua kwa hatua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa maelezo yake, mwanaume anaweza kuchukua hadi miaka minane kuonyesha tabia zake zote kwa mkewe, huku mwanamke akitajwa kuweza kutumia hadi miaka 16 kuonyesha kikamilifu tabia zake zote ndani ya ndoa.

“Binadamu haonyeshi tabia zake zote kwa wakati mmoja. Ndiyo maana wakati mwingine watu wanaweza kuishi miaka mingi pamoja lakini bado wakaendelea kugundua mambo mapya kuhusu wenza wao.

“Kwa wanawake hii ni zaidi, anaweza kutumia hadi miaka 16 kukuonyesha tabia zake zote. Kila siku utaona jipya, muhimu kinachotakiwa ni uvumilivu.”


Wataalamu wasemaje

Kauli hizo zimeungwa mkono na baadhi ya washauri wa mahusiano na wanasaikolojia waliozungumza na Mwananchi, wakisema changamoto kubwa iliyopo sasa ni watu kuingia kwenye ndoa wakiwa na matarajio yasiyoendana na uhalisia wa maisha.

Mshauri wa masuala ya familia, Happiness Mrema amesema vijana wengi wa sasa huingia kwenye ndoa wakiamini mapenzi pekee yanatosha kujenga familia.

“Watu wengi wanaingia kwenye ndoa wakiwa na picha ya maisha ya mitandaoni. Wanategemea furaha muda wote na wakikutana na changamoto ndogo wanaona ndoa imefeli,” amesema Happiness.

Amesema elimu ya ndoa na mawasiliano ni muhimu ili kuwasaidia wanandoa kutatua migogoro kabla haijafikia hatua ya talaka.

Kwa upande wake, mwanasaikolojia Neema Mwakalukwa amesema baadhi ya migogoro ya ndoa hutokana na watu kutokuwa tayari kiakili kubeba majukumu ya maisha ya pamoja.

“Wapo wanaoingia kwenye ndoa kwa presha ya umri, familia au jamii bila kuwa tayari ‘emotionally’. Baadaye changamoto ndogo zinapokuja wanaona hawawezi kuendelea,” amesema Neema.

Amesema pia matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yameongeza matarajio yasiyo halisi kwa wanandoa wengi.

“Mitandaoni watu wanaona picha za furaha pekee. Hawazioni changamoto zinazopitiwa ndani ya ndoa hizo. Matokeo yake wanandoa wanaanza kujilinganisha na wengine,” amesema.

Baadhi ya wanandoa nao wameeleza kuwa uvumilivu na mawasiliano ndiyo msingi mkubwa wa kudumu kwa ndoa.

Mkazi wa Kisemvule, Mariam Suleiman ambaye ameolewa kwa miaka 12 amesema changamoto ndani ya ndoa hazikosekani, lakini maamuzi ya haraka yanaweza kuvunja familia.

“Kuna wakati mnakwazana lakini mkikaa chini mkizungumza mambo yanaisha. Wengi sasa hawataki kuvumiliana hata kidogo,” amesema Mariam.

Naye Hamis Omary, mkazi wa Temeke amesema wanandoa wengi wa sasa wanakosa muda wa kujenga urafiki ndani ya ndoa kutokana na presha za maisha.

“Watu wanachoka na majukumu ya kila siku mpaka mawasiliano yanapungua. Hapo ndipo migogoro inaanza kuongezeka,” amesema Omary.

Kwa upande wake, Zuhura Bakari amesema jamii inapaswa kuacha kuwahukumu wanandoa wanaopitia changamoto na badala yake kuwapa ushauri na msaada.

“Ndoa si maisha ya filamu. Kuna nyakati nzuri na ngumu. Muhimu ni watu kujifunza kuvumiliana na kusaidiana,” amesema Zuhura.