Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kikao cha wanaume chazua mjadala, wataja kiini cha tatizo

Wanaume wakiwa wameketi katika moja ya ukumbi. Picha na AI

Muktasari:

  • Kimefanyika Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam kikiwakutanisha wanaume kutoka sekta mbalimbali kujadili masuala yanayowahusu, ikiwamo nafasi ya mwanaume katika familia, majukumu ya kifamilia, tatizo la afya ya akili na changamoto wanazokutana nazo katika maisha ya kila siku.



Dar es Salaam. Picha na video zilianza kusambaa taratibu katika mitandao ya kijamii zikionyesha ukumbi uliojaa wanaume wa rika na taaluma tofauti wakisikiliza kwa makini, wengine wakitikisa vichwa kuonyesha kukubaliana na hoja zilizokuwa zikitolewa.

Ndani ya muda mfupi, kile kilichoitwa ‘kikao cha wanaume’ kiligeuka gumzo mitandaoni, kikizua mjadala mpana kuhusu nafasi ya mwanaume katika jamii ya sasa na ama anavyopaswa kuhimili au kueleza yanayomsibu.

Kikao hicho kilichofanyika Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam kiliwakutanisha wanaume kutoka sekta mbalimbali kujadili masuala yanayowahusu ikiwamo nafasi ya mwanaume katika familia, majukumu ya kifamilia, afya ya akili na changamoto wanazokutana nazo katika maisha ya kila siku.

Lakini mara mijadala mikali iliyoibuka mitandaoni iliibua ajenda na mambo mengine mapya. Wapo waliolipongeza kama jukwaa muhimu kwa wanaume kujitafakari, wapo pia waliolikosoa wakidai linaweza kuonekana kama jukwaa la kupinga juhudi za usawa wa kijinsia na wqengine wakibeza kuwa wanaume hawapaswi ‘kulialia’.

Kwa baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kijamii, mjadala unaoendelea unaonyesha jambo moja muhimu kuwa wanaume nao wanahitaji majukwaa ya wazi ya kujadili changamoto zao.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Levocatus Ndaro, amesema kwa muda mrefu jamii imejenga taswira ya mwanaume kuwa mtu imara asiyeonyesha udhaifu.

Amesema kwa mtazamo huo, wanaume wengi hujikuta wakibeba matatizo yao kimya kimya.

“Kwa miaka mingi mwanaume ameonekana kama mtu anayepaswa kustahimili kila kitu. Lakini ukweli ni kwamba wao pia wanapitia changamoto nyingi na wanahitaji nafasi ya kuzungumza na kupata ushauri,” amesema Ndaro.

Kwa mujibu wa Ndaro, matarajio makubwa ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuwa tegemeo la familia, kufanikiwa kiuchumi na kuwa kiongozi ndani ya nyumba, wakati mwingine huweka shinikizo kubwa kwa wanaume.

Amesema shinikizo hilo linaweza kusababisha msongo wa mawazo, hasa pale ambapo mwanaume anahisi hawezi kufikia matarajio hayo.

Mtazamo huo unaungwa mkono na mtaalamu wa saikolojia ya jamii, Asha Kileo, ambaye amesema changamoto nyingi za wanaume zinahusiana moja kwa moja na afya ya akili.

Kileo anasema wanaume wengi hupitia msongo wa mawazo, lakini hushindwa kuzungumzia matatizo yao kwa hofu ya kuonekana dhaifu.

“Katika jamii nyingi bado kuna imani kuwa mwanaume hapaswi kulalamika. Hivyo matatizo yake hubaki moyoni na wakati mwingine husababisha migogoro ya kifamilia au matatizo ya kisaikolojia,” amesema.

Anasema majukwaa ya majadiliano yanaweza kusaidia wanaume kujifunza namna ya kukabiliana na changamoto hizo kwa njia chanya.

Maoni ya wachambuzi hao yanaakisi sura tofauti za mjadala zilizotokea mitandaoni kuhusu kikao hicho; wale wanaopongeza hatua hiyo wakisema ni jukwaa ambalo limekuja wakati muafaka, hasa wakati ambapo migogoro ya ndoa na talaka inaongezeka;  na wale waoadai kikao kinaenda kuongeza shida zaidi.

Akitoa maoni yake kupitia mtandao wa Instagram, Rashid Shelukindo, amesema wanaume wengi wamekuwa wakikosa nafasi ya kujadili matatizo yao.

“Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuwa wanaume hawapati majukwaa ya kuzungumzia changamoto zao. Kwa hiyo mijadala kama hii inaweza kusaidia kutafuta suluhisho,” amesema.

Shelukindo anaamini kuwa majadiliano ya wazi kuhusu majukumu ya kifamilia na changamoto za maisha, yanaweza kusaidia kupunguza migogoro katika familia.

Hata hivyo, si wote waliolipokea tukio hilo kwa mtazamo chanya.

Baadhi ya wanaharakati wa masuala ya jinsia wameonya kuwa majadiliano hayo yanapaswa kufanyika kwa uangalifu, ili yasije yakatafsiriwa kama juhudi za kupinga harakati za usawa wa kijinsia.

Mtetezi wa haki za wanawake na watoto kutoka Women Dignity Forum, Saidati Ngajiro amesema ni muhimu wanaume kujadili changamoto zao, lakini majadiliano hayo yanapaswa kujenga ushirikiano kati ya wanaume na wanawake.

“Tunatambua kuwa wanaume pia wanakabiliwa na changamoto mbalimbali. Lakini, ni muhimu mijadala hiyo ifanyike kwa mtazamo wa kushirikiana, siyo kwa namna itakayojenga mashindano ya kijinsia,” amesema Ngajiro.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kariakoo, Haji Manara, amesema haoni sababu ya wanaume kuwa na mikutano ya aina hiyo.

“Wapi tumeachwa mpaka tuanze kuwa na mikutano? Kama tunafanya uzembe au tunashindwa kuongoza familia zetu ni sisi wenyewe. Mwanaume anayejielewa hapaswi kulalamika,” amesema Manara.


Kiini cha mjadala


Wachambuzi wanasema mjadala unaoibuka kuhusu kikao hicho unahusu mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi yanayotokea katika jamii.

Kwa miaka mingi, mwanaume alionekana kama kichwa cha familia na mtoa mahitaji mkuu wa kiuchumi, huku mwanamke akionekana zaidi kama mlezi wa familia.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni hali hiyo imeanza kubadilika.

Kuongezeka kwa elimu kwa wanawake, ushiriki wao katika ajira na biashara pamoja na harakati za usawa wa kijinsia, kumebadilisha namna majukumu ndani ya familia yanavyotazamwa.

Mwanasaikolojia Deo Sukambi amesema mabadiliko hayo yamewafanya baadhi ya wanaume kujikuta katika hali ya sintofahamu kuhusu nafasi yao katika familia na jamii.

“Shida ilianzia kwenye uwezeshaji wa mwanamke ambao haukumuhusisha mwanaume. Unapokuwa na mwanamke mwenye nguvu, sauti ya mwanaume inashuka na inapofikia anaona anatakiwa apambane kupata mamlaka, uamuzi wa haraka kwake ni kuachia majukumu,” amesema.

Kwa mujibu wa Sukambi, hali hiyo imechangia kuzalisha kizazi cha wanaume ambao wakati mwingine hawako tayari kuwajibika kikamilifu katika majukumu ya kifamilia.

“Hiki ndicho kinachoendelea sasa. Tunatengeneza kizazi cha wanaume ambao hawataki kuwajibika kwa sababu wanaona wanawake wakiwajibika na kuwa na nguvu zaidi,” amesema.

Amesema baadhi ya majukwaa yanayojaribu kumsaidia mwanaume bado hayajaelewa kwa kina chanzo cha changamoto hizo.

“Tunarudi kwenye majukwaa ya kumwambia mwanaume apambane awe na hela na mamlaka, lakini hatuelezi kiini cha tatizo na namna ya kulitatua. Hili linahitaji uwekezaji wa muda mrefu, labda miaka 30 hadi 40 ijayo,” amesema.


Nini kifanyike

Kwa mujibu wa Sukambi, suluhisho la kudumu linahitaji kuanza na malezi ya watoto wa kiume.

Amesema ni vigumu sana kubadilisha mtazamo wa mtu ambaye tayari amekomaa, hivyo ni muhimu kuanza mapema kwa kuwalea watoto wa kiume katika misingi imara ya uwajibikaji.

“Tunatakiwa tuanze na hawa watoto wadogo wa kiume. Tuwajenge katika misingi itakayowafanya wakue wakiwa wanaume wanaojielewa na wanaosimama katika nafasi zao,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanawake katika mchakato wa kutafuta suluhisho.

“Tusifanye makosa yaleyale yaliyofanyika zamani wakati wa harakati za kumuinua mwanamke ambapo mwanaume aliachwa nyuma. Lazima wanaume na wanawake washirikiane,” amesema.

Mbali na hilo, Sukambi amesema wanaume wanapaswa kukumbushwa wajibu wao wa msingi katika familia.

Amesema jukumu la mwanaume halipaswi kuishia katika kutafuta kipato pekee, bali pia kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto.

“Isitoshe kuwaambia watafute hela au wawe na mamlaka, ni muhimu pia kusisitiza wajibu wao wa kulea familia. Hata kama una ugomvi na mwenza wako, hakikisha unabaki kwenye nafasi yako kama baba,” amesema.

Sukambi amesema uwepo wa baba katika maisha ya watoto ni jambo muhimu katika kujenga kizazi chenye maadili kwa kuwa mama hawezi kumfundisha mtoto wa kiume kuwa mwanaume.

“Watoto wanaolelewa na mama pekee mara nyingi hawapati fursa ya kuona mfano wa mwanaume katika familia. Kwenye maisha yake anakosa mwanaume ambaye anaweza kumtazama na akajifunza kuwa mwanaume, mume na baba. Hii inaweza kuwa changamoto kubwa kwa mtoto wa kiume anapokua,” amesema Sukambi.