Prime
Viongozi TLS waachia ngazi, wanachama watishia kuandamana Mwanza

Baadhi ya mawakili ambao ni wanachama wa TLS Mkoa wa Mwanza wanaotishia kuandamana hadi ofisi ya Jaji Mfawidhi mkoa wa Mwanza endapo uchaguzi wa kujaza nafasi za viongozi walioachia ngazi hautaitishwa. Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
- Wakati wanachama wa TLS Mkoa wa Mwanza wakitishia kuandamana hadi Ofisi ya Jaji Mfawidhi kudai uchaguzi wa kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu. Rais wa chama hicho, Boniface Mwabukusi amesema anasubiria ripoti ya kamati iliyoundwa kufuatilia suala hilo.
Mwanza. Baadhi ya wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Mwanza wametishia kuandamana hadi Ofisi ya Jaji Mfawidhi Mkoa wa Mwanza iwapo ombi lao la kuitishwa kwa uchaguzi kujaza nafasi za viongozi wa mkoa huo walioandika barua ya kujiuzulu halitozingatiwa.
Mawakili hao 46, wamejaza majina na kusaini fomu maalumu ya kushinikiza uongozi wa TLS ngazi ya taifa kuitisha uchaguzi wa kujaza nafasi za viongozi walioandika barua ya kujiuzulu nafasi zao ngazi ya Mkoa wa Mwanza.
Viongozi wanaotajwa kuwasilisha barua ya kujiuzulu ni Mwenyekiti wa TLS Mwanza, Msafiri Henga, Makamu wake, Marina Mashimba na Mweka Hazina wa TLS Mkoa wa Mwanza, Angelo Nyaoro.
Alipopigiwa simu kujua sababu za kujiuzulu, aliyekuwa Mwenyekiti wa TLS Mwanza, Msafiri Henga amethibitisha kuchukua uamuzi huo huku akisema hawezi kutaja sababu kwa kile alichodai hayuko kwenye mazingira mazuri ya kuzungumzia suala hilo.
“Nikweli nilijiuzulu, ila siko mazingira mazuri kuzungumzia suala hilo,” amesema Henga.
Kwa upande wake, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Mwanza), Marina Mashimba amesema alijiuzulu wadhfa huo Agosti 21, mwaka huu na kuwasilisha barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TLS.
Kuhusu sababu ya uamuzi huo, Marina amesema ni binafsi na hawezi kuzianika hadharani, hata hivyo amesema anaamini mamlaka zitachukua hatua stahiki kujaza nafasi hiyo.
“Niliandika barua ya kujiuzulu tangu mwezi wanane kwenye barua inajieleza kwamba nimejiuzulu kwa sababu binafsi na nilijibiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TLS kwamba barua yangu itapelekwa kwenye kamati ya uchaguzi kwa ajili ya hatua zinazostahili,” amesema wakili huyo.
Kwa upande wake, Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi amekiri kuwa na taarifa ya viongozi hao kuachia ngazi, huku akisema tayari imeundwa kamati maalumu ya kufuatilia sababu zilizochangia viongozi wa Mwanza kuchukua uamuzi huo.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, bado kamati hiyo haijawasilisha majibu ya ilichobaini kuhusiana na suala hilo na ushauri wao ili kuuwezesha uongozi kuchukua hatua zinazostahiki.
“Ni kweli taarifa ya Mwanza tuliisikia, tuliunda kamati tumeituma Mwanza bado nasubiria taarifa yake. Ila TLS ina utaratibu wala siyo kulalamika ni kwamba nafasi inapokuwa wazi kuna utaratibu wa kuangalia na kufuata na kujaza nafasi wala haihitaji malalamiko.
“Kuna sekretarieti ipo hapo kwa hiyo mazingira muhimu yote ya mtu kufanya kazi yapo. Hiyo tume haiwezi kufanya kazi za kiutawala za taasisi yenyewe imeenda kushughulikia huo mgogoro na tukishapata taarifa ya tume tutakuwa kwenye nafasi ya kutoa maamuzi,” amesema Mwabukusi.
Kuhusu madai ya mawakili kuathiriwa na kujiuzulu kwa viongozi hao, Mwabukusi amesema siyo ya kweli kwa kile alichodai ofisi za TLS Mwanza ziko wazi muda wote na hivyo madai ya kwamba kujiuzulu kwa viongozi hao kumewaathiri hayana ukweli wowote.
“Hao viongozi (waliojiuzulu) wana wajibu wa kuendesha vikao tu vya kikatiba wala hawaendi mahakamani kupokea samansi, na kukaa vikao na hakuna mtu atakuambia kuna kikao cha kikatiba hawajakaa. Tunaisubiri taarifa ya tume ituambie kilichojiri, walichoona, maoni yao halafu tutachukua hatua,” amesema.
Kauli ya wanachama
Awali, Wakili Steven Kitale aliieleza Mwananchi kuwa tayari wamejaza majina na kusaini fomu maalumu (Petition) ya kushinikiza uongozi wa TLS ngazi ya taifa kuitisha uchaguzi wa kujaza nafasi za viongozi na isipofanyika hivyo wataandamana kwenda kwa Msajili wa Mahakama.
“Tangu wajiuzulu tumekuwa hatuna uongozi. Ombi letu kubwa tunahitaji uchaguzi ufanyike hapa Mwanza, tunahitaji tume ya uchaguzi itangaze kamba nafasi hizo ziko wazi ili watu wagombee na kuchaguliwa. Tunayo haki ya kuchagua mtu tunayemtaka baada ya hao kujiuzulu,” alisema Wakili Kitale.
Wakili Ester Tuvave, ambaye ni mwanachama wa TLS Kanda ya Mwanza wamevumilia kwa muda mrefu bila mafanikio bila uongozi kuitisha uchaguzi wa kujaza nafasi hizo ndiyo maana wamenuia iwapo suala hilo halitoshughulikiwa wanampango wa kuandamana hadi Ofisi ya Jaji Mfawidhi mkoa wa Mwanza.
“Kama tusipojibiwa tutaandika barua kwenda kwa Jaji Mfawidhi kwa sababu tuko chini ya mahakama, kulalamika kwa sababu kama hamna uongozi hata Mahakama haitajua inashughulika na watu walioko chini ya uongozi gani. Tunahitaji uchaguzi ufanyike,” alisema Wakili Ester.