Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijiji, vitongoji vilivyofutwa Ngorongoro sasa kushiriki uchaguzi serikali za mitaa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa,akitoa amri na notisi ya mgawanyo wa maeneo ya kiutawala katika Serikali za Mitaa, katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, leo Jumatatu Septemba 16, 2024 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, ametangaza amri na notisi ya mgawanyiko wa maeneo ya kiutawala katika serikali za mitaa, vijiji na vitongoji vilivyokuwa vimefutwa katika Tarafa ya Ngorongoro vitashiriki uchaguzi huo.

Arusha. Serikali imetangaza Vijiji 12,333, Vitongoji 64,274 na mitaa 4,269 vitakavyoshiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vikiwamo vijiji na vitongoji vilivyokuwa vimefutwa katika Tarafa ya Ngorongoro.

Tangazo hilo la amri na notisi ya mgawanyo wa maeneo ya kiutawala katika serikali za mitaa, limetolewa leo Jumatatu Septemba 16, 2024 jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa.

Waziri huyo amesema amri ya mgawanyo wa maeneo ya utawala katika serikali za mitaa (Mamlaka za Wilaya) (Tangazo la Serikali Na. 796 la mwaka 2024) imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287.

Kuhusu notisi ya mgawanyo wa maeneo ya utawala katika serikali za mitaa (Mamlaka za Miji) (Tangazo la Serikali Na. 797 la mwaka 2024) limetolewa kwa mujibu wa vifungu vya 16(1) na 18(1) vya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288.


Waziri Mchengerwa amesema matangazo hayo yanajumuisha maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa tangazo la Serikali Na. 673 na 674, ambayo ilihusisha pia Tarafa ya Ngorongoro.

“Uchaguzi huu ni muhimu kwa ustawi wa demokrasia yetu na maendeleo ya serikali za  mitaa, katika amri na notisi hizi jumla ya maeneo yafuatayo yameainishwa ambayo ni vijiji 12,333, mitaa 4,269 na vitongoji 64,274,” amesema.

Waziri huyo amesema lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha kuwa maeneo hayo yanapata uwakilishi mzuri wa kiutawala, pamoja na huduma za kijamii na kiuchumi zinazowiana na mahitaji ya wananchi wake.

Amesema mchakato huo ni fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu moja kwa moja katika kuamua mustakabali wa maendeleo ya maeneo yao na uongozi imara wa mitaa, vijiji na vitongoji unahitajika kuendeleza juhudi za Serikali kuleta maendeleo endelevu.

“Niendelee kuwasisitiza wananchi umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kwa wale wote wenye sifa ili kushiriki kikamilifu katika kuunda serikali ya wananchi kidemokrasia, kwa kuhakikisha wanajiandikisha pamoja na wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali kuanza kujiandaa,” amesema Mchengerwa.

Amewataka wananchi kote nchini kuheshimu taratibu zilizowekwa na kushiriki uchaguzi huo kwa amani, utulivu na umoja.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Marekani Bayo amesema wamepokea tangazo hilo kwa furaha na katika wilaya hiyo, vijiji vyote 65 na vitongoji 242 vitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

"Hii inaleta furaha kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro, tuko kwenye furaha kwa sababu kila mwananchi ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, kwa hiyo itakuwa haki yao kikatiba imetekelezwa,” amesema Bayo na kuongeza;

“Tunaamini tutashiriki kuandikisha na kupiga kura, miundombinu ipo shwari na tumejiandaa na tunaendelea kuhamasisha wananchi wajitokeze kujiandikisha ili wapata fursa ya kuja kuchagua viongozi wanaowataka.”


Zuio la mahakama

Awali, Agosti 22, 2024 Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilizuia tamko la Serikali namba 673 la Agosti 2, 2024 la kufuta kata, vijiji na vitongoji vikiwamo vya Wilaya ya Ngorongoro hadi amri ya Mahakama itakavyoelekeza vinginevyo.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji, Ayoub Mwenda aliyesikiliza maombi madogo ya zuio hilo yaliyowasilishwa na mmoja wa wananchi wa Ngorongoro, Isaya Ole Pose kupitia wakili Peter Njau.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mwenda aliridhia maombi hayo madogo na kukubali zuio la kusimamisha tamko hilo kupisha usikilizaji wa maombi ya msingi.

Katika maombi hayo madogo namba 6953 ya mwaka 2024, yalikuwa na hoja mbili ya kwanza ni kuomba zuio hilo na ya pili ambayo ni kuu katika shauri hilo,  ni kuiomba Mahakama itoe kibali cha mleta maombi kufungua maombi ya marejeo ya amri hiyo kama ilikuwa halali au si halali.

Jaji Mwenda aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 26, 2024 Mahakama itakaposikiliza maombi ya msingi.

Agosti 2, 2024 lilitolewa tangazo la Serikali chini ya kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) la  kufuta vijiji, kata na vitongoji kutoka wilaya za Ngorongoro, Bahi, Chemba, Kasulu, Kakonko, Hai na Rombo.

Hata hivyo, siku moja baada ya uamuzi huo wa Mahakama, Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kurejeshwa kwa huduma za kijamii na kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa.

Pia aliagiza kuondolewa kwa vikwazo vyote vilivyowekwa kwa wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro ambao kwa muda wa siku tano walikusanyika kwenye maeneo tofauti wakidai kupatiwa haki hiyo.

Miongoni mwa haki walizokuwa wakidai wananchi hao ni pamoja na kupinga kufutwa kwa vitongoji 96 , vijiji 25 na kata 11, amri ambayo kimsingi ilikuwa ikiwakosesha haki ya kupiga kura.

Zingine ni huduma za elimu, afya na maji pamoja na vikwazo vya muda wa kuingia na kutoka katika eneo hilo.

Maagizo hayo yalitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Willima Lukuvi, akizungumza na wananchi wa Kata 11, katika eneo la Oloirobi, Kata ya Ngorongoro walipoenda kusikiliza wananchi hao waliokusanyika kwa siku tano.

Lukuvi ambaye aliambatana na viongozi wengine, alisema wametumwa na Rais Samia kuzungumza nao na kutoa maagizo hayo ambayo ameelekeza mamlaka zote kuanzia mkuu wa mkoa hadi wilaya kuhakikisha yanatekelezwa.

Kuhusu huduma za jamii, alisema Rais anazo taarifa kuwa wananchi hao hawapati baadhi ya huduma ikiwemo kuharibika kwa miundombinu kama vyoo vya shule, hali inayosababisha wanafunzi kujisaidia vichakani.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngorongoro, Murtallah Mbilu alisema tayari  halmashauri hiyo ilikuwa imeanza kukagua na kubainisha vituo vya kupiga kura na kufanya maandalizi mengine kwa ajili ya uchaguzi huo.

“Tutakuwa na mhandisi na kuna Sh350 milioni zilizotolewa na mamlaka,  tutazitumia kwa ajili ya kukarabati miundombinu ambayo imeharibika ikiwemo vyoo katika shule,” alisema.