Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KESI YA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA: Mahakama itakavyoamua leo

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Dk Ananilea Nkya (wa pili kulia) akiteta jambo na Mchungaji, Mwana Mapinduzi (kushoto), katika chumba cha Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam Agosti 28,2024 kabla ya kuanza kusikiliza kwa kesi waliyoifungua ya kupinga Tamisemi kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa (Jukata), Bob Wangwe. Picha na Sunday George

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, leo Jumatatu Septemba 9, 2024 inatarajiwa kutoa uamuzi utakaotoa hatima ya shauri la kupinga uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.

Hatima hiyo itatokana na uamuzi wa Mahakama hiyo kuhusiana na pingamizi la awali dhidi ya shauri la maombi ya ridhaa ya kufungua shauri hilo la kupinga uchaguzi huo pamoja na maombi hayo ya ridhaa ya kufungua shauri hilo.

Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 umepangwa kufanyika Novemba 27, 2024. Agosti 15, mwaka huu, Waziri wa Tamisemi alitangaza kuanza kwa mchakato wa uchaguzi huo kuanzia tarehe hiyo mpaka Novemba 27, 2024, siku ya upigaji kura.

Lakini, wanaharakati watatu wanaojitambulisha ni raia wa Tanzania waliosajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga, wamefungua shauri la maombi wakiomba kibali cha Mahakama ifungue shauri la kupinga uchaguzi huo kwa utaratibu wa mapitio ya Mahakama (judicial review).

Shauri hilo limefunguliwa na Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe, mwanahabari mstaafu, Ananilea Nkya na Bubelwa Kaiza na wajibu maombi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri hilo la maombi namba19721/2024 linalosikilizwa na Jaji Wilfred Dyansobera, wanaomba kibali wafungue shauri la kupinga kanuni za uchaguzi huo za mwaka 2024 zilizotungwa na Waziri wa Tamisemi, wakihoji mamlaka yake.

Pia, katika shauri hilo wanaloomba kulifungua wanataka kupinga uchaguzi huo kusimamiwa, kuratibiwa na kuendeshwa na Ofisi ya Rais Tamisemi, badala ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), kwa mujibu wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024.

Lakini, wajibu maombi (Waziri wa Tamisemi na AG) wameweka pingamizi la awali dhidi ya shauri hilo la maombi ya ridhaa ya kufungua shauri la kupinga uchaguzi huo, wakiiomba Mahakama hiyo isiyasikilize maombi hayo kwa madai kuwa na kasoro za kisheria.

Kwa kawaida pale upande mmoja katika shauri au kesi unapoibua pingamizi la awali, pingamizi hilo linapaswa lisikilizwe kwanza na kutolewa uamuzi kabla ya kusikiliza shauri la msingi.

Hata hivyo, wakati mwingine kutegemeana na mazingira, Mahakama inaweza kuamua kusikiliza pingamizi la awali sambamba na shauri la msingi.

Hivyo hata, katika shauri hilo Mahakama iliamua kusikiliza pingamizi la awali sambamba na shauri la msingi la maombi ya ridhaa ya kufungua shauri la kupinga uchaguzi huo.


Hoja za pingamizi

Katika pingamizi hilo, wajibu maombi hao wamebainisha hoja nne ambazo wanadai ni kasoro za kisheria zinazolifanya shauri hilo lisiwe halali na Mahakama isiwe na mamlaka ya kulisikiliza.

Katika pingamizi hilo, hoja ya kwanza wajibu maombi walidai waombaji walikuwa na njia mbadala ambayo wangeitumia kwanza kabla ya kufungua shauri la ridhaa ya kufungua shauri la mapitio ya Mahakama.

Kwa mujibu wa mawakili wa wajibu maombi, waombaji walipaswa kufungua kesi ya kikatiba dhidi ya sheria zinazompa mamlaka Waziri wa Tamisemi kutunga kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambazo pia zinaelekeza kuwa uchaguzi huo husimamiwa na Ofisi ya Rais Tamisemi.

Katika hoja ya pili, wajibu maombi walidai kiapo kinachounga mkono maombi hayo kina kasoro za kisheria kwa kuweka mambo au taarifa zisizohitajika kuwemo.

Katika hoja ya tatu, walidai kiapo kianachounga mkono maombi kina taarifa ambazo hazimo kwenye hati ya maelezo ya shauri na wanadai kiapo hicho hakidhibitishi baadhi ya taarifa zilizomo kwenye hati ya maelezo.

Hata hivyo, mawakili wa waombaji walipinga hoja hizo za pingamizi la wajibu maombi wakidai hazina mashiko, huku wakidai waombaji hawakuwa na njia nyingine mbadala zaidi ya waliyoichukua kuomba ridhaa kufungua shauri la mapitio na si kesi ya Kikatiba.

Pia walidai hoja kuwa kuna kasoro katika kiapo kinachounga mkono maombi hayo hazina mashiko, huku wakidai mambo yote yaliyo kwenye kiapo hicho ni ukweli mtupu na kwamba kiapo hicho kinathibitisha taarifa zilizomo kwenye hati ya maelezo ya shauri.


Matokeo ya uamuzi

Mahakama katika uamuzi wake, kwanza itatoa uamuzi kuhusiana na hoja za pingamizi lililowekwa na wajibu maombi.

Matokeo ya uamuzi wa hoja za pingamizi hilo ndio yatakayoamua shauri hilo liishie hapo au kuifanya Mahakama iende katika hatua ya pili, yaani uamuzi wa hoja za maombi ya msingi.


Uamuzi wa pingamizi

Katika hatua hii, Mahakama itaangalia hoja za pingamizi iwapo zina mashiko au la.

Iwapo Mahakama itakubaliana na hoja za pingamizi la wajibu maombi, basi italitupilia mbali shauri hilo na shauri hilo litaishia hapo.

Hata hivyo, ikiwa Mahakama itatupilia mbali pingamizi hilo la wajibu maombi, waombaji watakuwa wamevuka kigingi cha kwanza na sasa shauri litaingia katika hatua ya pili ya uamuzi, yaani uamuzi wa hoja za shauri la msingi.


Uamuzi wa shauri la msingi

Ili mwombaji apewe kibali cha kufungua shauri la mapitio ya Mahakama, anapaswa kutimiza masharti au vigezo vitatu kisheria.

Kwanza, anapaswa afungue shauri la maombi ya ridhaa kuomba kufungua shauri la mapitio ya Mahakama ndani ya miezi sita tangu kutolewa kwa uamuzi unaokusudiwa kupingwa.

Pili, sharti aonyeshe kuna hoja inayohitaji kujadiliwa inayobishaniwa na tatu aonyeshe ana maslahi katika jambo au uamuzi anaotaka kuupinga.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, waombaji hao kupitia mawakili wao, Mpale Mpoki (kiongozi wa jopo) na Jebra Kambole waliieleza na kuonyesha Mahakama wamekidhi masharti ya kisheria kustahili kupewa kibali cha kufungua kesi kupinga uchaguzi huo.

Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na wajibu maombi kupitia jopo la mawakili wa Serikali lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo wakidai waombaji wameshindwa kuonyesha wamekidhi masharti hayo.

Hivyo, Mahakama katika uamuzi wake itangalia iwapo waombaji wametimiza masharti au vigezo vya kisheria kustahili kupewa kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama, kupinga uchaguzi huo.

Kama itakubaliana na hoja za wajibu maombi kuwa waombaji wameshindwa kukidhi matakwa hayo, yaani kuonyesha wamekidhi vigezo hivyo, basi shauri hilo la maombi yao ya ridhaa ya kufungua shauri la mapitio ya Mahakama kupinga uchaguzi huo yatatupiliwa mbali.

Lakini, kama Mahakama itakubaliana na hoja za waombaji kuwa wamekidhi matakwa hayo ya kisheria kwamba wamethibitisha kukidhi vigezo hivyo vilivyowekwa kisheria, basi Mahakama itawaruhusu kufungua shauri hilo la mapitio ya mahakama.


Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kitakachotolea