Vijana 50 kulipiwa mahari kupitia Al- Hikma Foundation

Dar es Salaam. Taasisi ya dini ya Kiislamu ya Al- Hikma Foundation imetangaza kuwalipia mahari vijana 50 ambao wapo tayari kuoa.
Akizungumza katika mashindano ya 23 ya kimataifa ya uhifadhi wa Qur’an ambayo yamefanyika leo Jumapili Aprili 9, 2023 katika Uwanja wa Uhuru jijini hapa, Sheikh Nurdin Kishki ambaye ni mwenyekiti wa taasisi hiyo amesisitiza kuwa mahari hiyo haitawahusu wale wanaotaka kuongeza mke wa pili.
Kishki amesema sharti hilo limewekwa kwa asiye na mke kabisa ana haja ya kusaidiwa zaidi ya yule ambaye anataka kuongeza mke.
“Tutafanya ndoa ya pamoja ya watu 50 mahari tutatoa Sisi Al-Hikma Foundation masharti usiwe unaongeza mke wa pili ndoa itafanyika Dar es salaam chini ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir”
Amesema lengo lilikuwa kuozesha vijana 100 hivyo ametoa wito kwa yeyote mwenye kuweza kuunga mkono jambo hilo.
Amesema jambo hilo litafanyika kupitia program maalum iliyoanzishwa na taasisi hiyo ya kurejesha kwa jamii kupitia mashindano hayo na kwa mwaka jana walifanikiwa kulipia gharama za kujifungua kwa wajawazito 100.
Leo vijana 23 kutoka mataifa mbalimbali duniani wamekutana jijini Dar es Salaam kuchuana kwenye mashindano ya kusoma Qur’an.