Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vifo vya kushtua vyaibua hofu

Muktasari:

  • Uchunguzi unaendelea, huku mazishi ya aliyekuwa mwanafunzi wa IFM yakipangwa kufanyika Jumatano.



Dar es Salaam. Ni kama matukio ya vifo vya kikatili yanaanza kurejea taratibu mkoani Dar es Salaam, baada ya kuripotiwa kwa matukio matatu mfululizo ya miili ya watu kuonekana ikielea majini.

Tofauti na ilivyozoeleka nyakati za mvua, ambapo mito ya Dar es Salaam hubeba magogo na taka mbalimbali, hali ilikuwa tofauti jana Jumapili na leo Jumatatu, Mei 3 na 4, 2026, katika maeneo ya Mto Msimbazi, hususan Kipawa na Daraja la Selander, ambako miili ya watu ilionekana ikielea majini.

Matukio hayo yameibua maswali miongoni mwa wananchi kuhusu chanzo na mazingira ya vifo hivyo, huku wakikumbuka baaadhi ya matukio yaliyotokea miaka ya karibuni.

Akizungumza na Mwananchi leo, Mei 4, 2026 Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACF), Peter Mabusi, amesema walihusika katika uokoaji wa miili miwili katika matukio tofauti.

Amesema tukio la kwanza liliripotiwa eneo la Stakishari, na walipokea taarifa ya uwepo wa mwili wa mwanamke mwenye umri wa takribani miaka 60 ukiwa unaelea mtoni.

Amesema kikosi kilifika eneo la tukio, kuuopoa mwili huo na kuukabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi.

Kwa mujibu wa Mabusi, tukio la pili limetokea leo Jumatatu, Mei 4, 2026, saa tano asubuhi, baada ya kupokea taarifa ya mwili wa kijana mwenye umri unaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 21 hadi 26 uliokuwa ukielea karibu na Daraja la Selander.

Mwili huo uliokotwa na kukabidhiwa polisi, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha vifo hivyo kama ni ajali za maji au matukio yenye viashiria vingine vya uhalifu.

Kamanda Mabusi amesisitiza umuhimu wa wananchi kuchukua tahadhari, hasa katika kipindi hiki cha mvua, akibainisha kuwa mara nyingi miili inayopatikana huwa ya watu waliokumbwa na mafuriko au kusombwa na maji, akitolea mfano wale waliokuwa wakikaa karibu na mito au chini ya makaravati.

Hata hivyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kupitia mkurugenzi wake, Dk Anna Henga, kimelaani matukio hayo na kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka, hususan wa maiti iliyokutwa imekatwa kichwa.

“Matukio haya ni ya kinyama na yanakiuka haki ya msingi ya kuishi. Ni wajibu wa vyombo vya dola kuhakikisha wahusika wanabainika na kufikishwa mbele ya sheria,” amesema Dk Henga.

Kwa upande wake, Wakili Ibrahim Bendera amesema matukio hayo yanahitaji uchunguzi wa hali ya juu ili kubaini wahusika, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa makini na usalama wao binafsi na kutoa taarifa kwa ndugu wanapokuwa safarini au wanapotoka nyumbani.

“Serikali haina askari wengi wa kumlinda kila mwananchi, kwa hiyo wananchi nao wanapaswa kusaidia katika hili ili kulinda usalama wa familia zao,” amesema wakili huyo.

Kikatiba, amesema matukio hayo yanakinzana na Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotambua haki ya kila mtu kuishi.


Maelezo ya matukio

Tukio liliripotiwa leo Mei 4, 2026, katika eneo la Daraja la Selander, na picha na video zilizosambaa mitandaoni zikionesha mwili wa kijana ukiwa unaelea majini.

Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo wala kutambua utambulisho wa marehemu.

Tukio hilo limetanguliwa na lingine la jana Jumapili, Mei 3, 2026, ambapo mwili wa kijana mmoja ulioonekana kukatwa kichwa ulipatikana ukielea juu ya maji.

Kitendo hicho kimeelezwa kuwa cha kikatili, huku kichwa cha marehemu kikiwa hakijulikani.

Baadhi ya watu waliodai kuwa ndugu walimtambua marehemu huyo kwa jina la James Temba, anayedaiwa kuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM).

Hata hivyo, uongozi wa chuo haukuthibitisha taarifa hizo, ingawa baba mzazi wa kijana huyo alithibitisha kuwa mwanawe alikuwa akisoma katika chuo hicho.

Aidha, msanii wa kundi la TMK Wanaume, Amani Temba (maarufu Mheshimiwa Temba), ameeleza masikitiko yake kupitia mtandao wa Instagram, akimtaja marehemu kuwa ni ndugu yake wa karibu.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilitoa taarifa kuwa linachunguza tukio la mwili uliopatikana Aprili 30, 2026, katika Mto Msimbazi eneo la Kipawa, ukiwa hauna kichwa. Uchunguzi wa awali umeashiria kuwa huenda mwili huo ni wa James Temba, mkazi wa Tabata Chang’ombe.

Polisi wamesema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika watakaobainika.


Simulizi ya familia

Baba wa marehemu amesema mwanawe alikuwa mwanafunzi wa kutwa IFM na mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa Jumatano, Aprili 29, 2026, alipomjulisha kuwa amefaulu mitihani yake.

Amesema baada ya hapo, kijana huyo aliondoka nyumbani kuelekea chuoni na hakurejea. Juhudi za kumpigia simu hazikufanikiwa, hali iliyozua wasiwasi kwa familia.

Amesema siku iliyofuata, familia ilianza kumtafuta bila mafanikio hadi walipopata taarifa za kupatikana kwa mwili katika Mto Msimbazi. Baba huyo amesema walipofika katika Hospitali ya Polisi eneo la Kilwa Road, Dar es Salaam, waliutambua mwili huo kupitia alama maalumu za mwilini.

Uchunguzi wa matukio hayo unaendelea, huku wakisubiri majibu ya kina kuhusu chanzo chake na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wahusika.


Chuo cha IFM

Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kimetoa taarifa ya tanzia ikieleza kusikitishwa na taarifa ya kifo cha mwanafunzi James Temba, aliyekuwa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Uchumi na Fedha, na mwili wake kuokotwa Aprili 30, 2026, saa 9 alasiri, ukielea kwenye maji yanayotiririka Mto Msimbazi.

“Uchunguzi wa tukio hili unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho chini ya vyombo vya ulinzi na usalama.

“Taarifa za mazishi zinaendelea nyumbani kwa wazazi wake Tabata, na ibada ya mazishi itafanyika Jumatano, Mei 6, 2026, katika Kanisa la KKKT Tabata,” imeeleza taarifa hiyo na kuongeza;

“Kifo chake kimetuacha na huzuni kubwa kwa uongozi wa chuo, wanafunzi, walimu na jamii ya chuo kwa ujumla.”

Nao uongozi wa wanafunzi wa chuo hicho umetoa salamu za pole kwa wote walioguswa na msiba huo.

“Alikuwa mwanafunzi aliyesajiliwa kwa namba IMC/BEF/2524885 katika Kampasi Kuu ya Dar es Salaam. Marehemu alitoweka na kutoonekana kwa siku nne na baadaye alikutwa amefariki dunia,” imeeleza taarifa hiyo.