Maboresho ya miundombinu na tahadhari vyahitajika kukabili majanga
Wafanyakazi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiwa katika moja ya banda la kitengo cha Elimu na Sheria katika maonesho ya wiki ya Zimamoto Duniani ambayo inatamatika Mei 4, 2026 katika viwanja vya Mnazimmoja jijini Dar es Salaam
Muktasari:
- Siku ya Zimamoto Duniani huadhimishwa Mei 4 kuwaenzi mashujaa. Tanzania inakabiliwa na changamoto ya miundombinu mibovu na uzembe wa jamii, huku Jeshi la Zimamoto likiendelea kuongezewa vifaa vya kisasa na kutoa elimu ili kupunguza vifo na uharibifu wa mali.
Dar es Salaam. Mei 4 ya kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Zimamoto, maalumu kwa kuwaenzi wazimamoto waliopoteza maisha wakiwa kazini. Maadhimisho hayo huambatana na shamrashamra zinazoanza Aprili 28 hadi kilele chake.
Historia ya siku hii inahusishwa na tukio lililotokea Desemba 2, 1998 katika eneo la Linton, jimbo la Victoria nchini Australia, ambapo wazimamoto watano walipoteza maisha wakipambana na moto mkubwa wa msituni.
Ni tukio hilo lililochochea kuanzishwa kwa siku hii, ikiwa ni njia ya kutambua mchango wa wazimamoto na kutoa heshima kwa wale waliopoteza maisha wakilinda wengine.
Licha ya historia hiyo ya kusikitisha, siku hii pia hutumika kutathmini mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta ya zimamoto duniani.
Katika kuadhimisha siku hiyo, kaulimbiu ya mwaka huu “Tuchukue tahadhari leo, tuokoe maisha na mali kesho” imebaki kuwa mwito muhimu unaosisitiza usalama wa moto si jukumu la Serikali pekee, bali la kila mwananchi.
Kwa ujumla, Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya majanga ya moto, lakini pia inaendelea kupiga hatua kupitia uwekezaji wa vifaa vya kisasa, mafunzo na elimu kwa jamii, hatua inayolenga kupunguza vifo na mali zinazopotea kila mwaka.
Takwimu za mwaka 2025 zinaonesha matukio ya moto 3,091 yaliripotiwa nchini, yakisababisha vifo vya watu 114 na majeruhi 295, huku mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Pwani, Ruvuma, Njombe, Dodoma na Manyara ikitajwa kuathirika zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, maeneo yaliyoathirika zaidi ni nyumba za makazi matukio 1,422, magari 94, ofisi 132 na stoo 117. Uchunguzi umebaini hitilafu za umeme kuwa chanzo kikuu cha moto matukio 781, zikifuatiwa na watoto kuchezea viberiti 215 pamoja na uchomaji wa takataka na maandalizi ya mashamba 479.
Miongoni mwa matukio yaliyotikisa jamii ni kifo cha mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 3–4 aliyefariki katika ajali ya moto eneo la Magomeni Kota, Dar es Salaam, na uchunguzi ulibaini alichezea njiti za kiberiti bila uangalizi.
Aidha, zaidi ya maeneo 69,594 yalikaguliwa, ramani 2,356 za majengo zikapitishwa, huku elimu ya kinga na tahadhari ikifikia zaidi ya maeneo 22,000 kupitia kampeni za moja kwa moja na vyombo vya habari.
Vipindi 1,039 vya redio na televisheni vilitumika kuelimisha wananchi kuhusu usalama wa moto.
Mawakala wa vifaa vya kuzimia moto wakiwa kwenye maonyesho ya wiki ya Zimamoto katika viwanja vya Mnazimmoja jijini Dar es Salaam ambayo yanataratiwa kufikia tamati Mei 4,2026
Sheria na ukaguzi
Akizungumzia udhibiti wa majanga, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kitengo cha sheria, Mathias Manyama, amesema jeshi hilo linafanya kazi kwa utekelezaji wa sheria na ukaguzi wa tahadhari dhidi ya majanga ya moto.
Kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Na. 14 ya mwaka 2007 Sura ya 427, katika kutekeleza majukumu hayo chini ya kifungu cha 5(1), jukumu kubwa la jeshi hilo ni kuokoa maisha na mali, likitekelezwa kupitia ukaguzi wa majengo na maeneo mbalimbali ili kubaini hatari zinazoweza kusababisha majanga.
Amesema majengo marefu yanatakiwa kuwa na vifaa vya kuzimia moto na mifumo ya tahadhari, huku mabwawa yakitakiwa kuwa na wasimamizi waliopata mafunzo pamoja na vifaa vya uokoaji. Aidha, magari yote yanapaswa kuwa na vizimia moto.
“Ukaguzi ukibaini upungufu, tunatoa maelekezo na endapo hautekelezwi, hatua za kisheria huchukuliwa,” amesema Manyama.
Uokoaji na athari zake
Takwimu zinaonesha pia kuanzia Januari hadi Machi 2026, matukio 29 ya majanga yalitokea katika mkoa wa Dodoma, yakiwemo vifo 17 vya watu waliovuka mito yenye maji mengi na wengine 11 waliopoteza maisha kwa kuzama kwenye mabwawa na visima.
Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo, Mrakibu Rehema Menda, Aprili 3, 2026 amesema elimu ya tahadhari bado inahitajika kwa jamii ili kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika.
Changamoto ya miundombinu
Matukio mengine yameonesha changamoto ya miundombinu duni, ikiwemo tukio la Morogoro Julai 31, 2024, na zimamoto walishindwa kufika kwenye tukio kutokana na ukosefu wa barabara na kulazimika kutembea kwa miguu huku gari likibaki mbali.
Aidha, Novemba 19, 2025 Shinyanga, gari la zimamoto lilichelewa kufika baada ya hitilafu ya bomba la upepo, hali iliyozua hasira za baadhi ya wananchi.
Mei 2, 2026 Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema bado kuna maeneo mengi jijini Dar es Salaam yenye miundombinu isiyo rafiki kwa magari ya zimamoto, jambo linalochelewesha operesheni za uokoaji wakati wa majanga.
Amesema atamuomba Mkuu wa Mkoa siku ya kufunga maadhimisho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuzungumzia jambo hilo kwa kushirikiana na wadau wa mipango miji kuhakikisha kila eneo linalojengwa linazingatia uwepo wa njia za dharura ili kupunguza madhara.
“Ni lazima tuangalie ramani zetu za miji, kuna maeneo magari ya zimamoto hayawezi kufika kwa haraka na hii inatugharimu maisha na mali za wananchi,” alisema Mpogolo.
Wadau waeleza
Profesa Gelardine Kikwasi wa Chuo Kikuu cha Ardhi amesema ni vyema mtu anapotaka kujenga kuzingatia ramani ya mipango miji na kuacha nafasi kwa ajili ya gari kupita.
Amesema maeneo mengi wananchi hawafuati ramani za mipango miji, hivyo kunapotokea majanga inakuwa vigumu kufanya uokozi kwa sababu hakuna ukaguzi wa majengo kwa maeneo husika.
“Wanaojenga wanapaswa kufuata ramani za mipango miji, lakini pia kuna Serikali za mitaa ziwasiliane kuona namna gani wataacha njia kwa matumizi mengine ili wakati wa dharura iwe rahisi kufanya uokozi,” amesema Profesa Kikwasi.
Mtaalam wa ramani, Selua Barabara, amesema ramani zote zinatakiwa kupitishwa na mamlaka husika na wanapoanza ujenzi inatakiwa kufanyika ukaguzi kwa ajili ya kufuata alama husika.
“Yanayotokea ni wananchi kujiamulia. Wachora ramani wote wanafuata sheria kwa kuacha eneo la barabara na dharura, lakini baadhi ya wananchi husogeza mawe ya alama na kujikuta wakifunga njia,” amesema Selua.