Prime
Yaliyojificha uchunguzi maiti
Muktasari:
- Asimulia safari yake hadi kuwa daktari bingwa, amesema shahada ya kwanza na ya pili alisoma katika Chuo Kikuu Kishiriki Muhimbili (MUHAS), kisha alienda Norway kusomea magonjwa ya figo.
Dar es Salaam. Mafanikio hutokana na shauku ya kufanikisha jambo. Shauku hiyo huzaa matunda pale inapopewa nguvu na kumwagiliwa kama mmea.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Angela Mwakimonga, daktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa (Pathologist) kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambaye kauli ya baba yake ilimjenga hadi kuwa daktari mbobezi nchini.
Akizungumza na Mwananchi, daktari huyu ameeleza safari yake, mafanikio, changamoto na dhana anazokutana nazo katika kazi yake.
Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa (Pathologist) kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Angela Kipesile akionesha namna ya usomaji na utambuzi wa magonjwa.
“Mimi ni mchunguzi wa magonjwa. Lakini pia tunahusika na uchunguzi wa miili iliyokufa yenye vifo vyenye mashaka. Pathology ndiyo uti wa mgongo wa afya, ndio tunaotambua magonjwa na kutambua mtu amekufa kwa ugonjwa gani.
“Nikiwa mdogo, baba yangu alikuwa ananiambia mimi nitakuwa nesi au mwalimu. Shule ya msingi nilisoma Thornpark Primary School, Lusaka, Zambia. O-level nikasoma Chipembi Girls, ipo Chisamba, Zambia, kisha A-level nikasoma Jitegemee,” amesema.
Akisimulia safari yake hadi kuwa daktari bingwa, amesema shahada ya kwanza na ya pili alisoma katika Chuo Kikuu Kishiriki Muhimbili (MUHAS), kisha baadaye alienda Norway kusomea magonjwa ya figo.
“Wakati nimeenda chuo mwaka wa kwanza, nilikuwa natamani tu kuwa daktari. Nilikuwa napenda sana watoto, lakini nilivyofika mwaka wa pili nikagundua ninapenda kitu kingine ambacho ni pathology.
“Somo la pathology linasomwa mwaka wa pili wa shahada. Mwalimu aliyekuwa ananifundisha alikuwa mwanamke, nilipenda namna alivyokuwa akielezea. Yaani ukiona, mfano ugonjwa wa kansa, anaeleza kitu gani kimekuja nyuma yake mpaka imetokea kansa,” amesema.
Baada ya kuvutiwa na mwalimu huyo, Angela amesema akili yake ilihama kutoka kutamani kuwa daktari wa watoto hadi kujikita kwenye uchunguzi wa magonjwa, na hapo ndipo safari yake ilianza.
Uchunguzi wa maiti ukiwa ni kati ya kazi anazofanya, Angela anasimulia mengi yenye funzo na kusisimua. Twende pamoja.
Siku ya kwanza kuchunguza maiti
Angela ameelezea siku yake ya kwanza katika uchunguzi wa maiti ilivyogeuka kuwa mtihani.
“Unapoanza mwaka wa kwanza wa shahada, lazima ukutane na maiti, kuna somo linaitwa ‘Anatomy’. Tukianza huku masters ndiyo tunakutana na maiti tena.
“Kwa mara ya kwanza nimeingia kukata ule mwili, aisee sikuweza kula chakula. Yaani hata kulala nilipata shida sana. Nilikuwa nashtuka, lakini baadaye unazoea kwa sababu ndiyo kazi uliyoichagua. Nakumbuka ilikuwa mwaka 2014,” amesema Angela.
Licha ya hayo, ameeleza umuhimu wa kufanyia maiti uchunguzi, huku akisema lengo kuu ni kutambua chanzo cha kifo au vifo vyenye mashaka.
Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa (Pathologist) kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Angela Kipesile (kulia), akifanya mahojiano na mwandishi wa habari wa gazeti hili (kushoto).
“Kuna umuhimu ili kuondoa ile sintofahamu kwenye jamii. Na pia ili huyu mtu apate haki yake kama anahitajika kupata.
“Uchunguzi mwingine hufanyika kutoka wodini. Madaktari wametibu lakini wanafanya ‘clinical’ ili kujua kitu gani kilikuwa kinamsumbua huyu marehemu,” amesema Angela.
Dhana potofu kuchunguza maiti
Amesema zipo dhana nyingi potofu kwenye jamii kuhusu uchunguzi wa maiti ambazo kiuhalisia hazina ukweli.
“Unajua ukishaongelea maiti kuna vitu vingi ambavyo vinaizunguka. Kwa hiyo, kuna wengine unakuta wanadai tunachukua ubongo. Nilishawahi kuambiwa tunachukua ubongo tukatengeneza Panado.
“Sasa unajiuliza hawa wamejifikiria nini, lakini zipo dhana nyingi sana. Wanasema tunachukua viungo ili tuondoke navyo. Lakini postmortem inahusisha kukata mwili,” amesema.
Angela ameeleza kuwa haiwezekani kufanya uchunguzi wa maiti kwa lengo la kujua sababu ya kifo bila kukata mwili.
“Lazima uangalie viungo, uvilinganishe kawaida na ugonjwa. Sasa mtu anapokuta kuna mpasuko tumekata na tumeshona, anasema wamechukua maini.
“Au labda alipata shida kichwani, tumekata kichwani, wanasema tumechukua ubongo. Lakini kiuhalisia si kweli, aliyefanya uchunguzi amekata ili kujua chanzo cha kifo ni nini,” amesema Angela.
Daktari huyu bingwa amesema dhana hizo potofu huwalazimu kukaa na ndugu wa marehemu kwa ajili ya kuwaelimisha.
“Kuna vitu vingine huwa vinatuwahi hata kabla ndugu hawajatoka humu Muhimbili. Kwa hiyo viongozi huwa wanakaa nao au daktari aliyeko zamu anawaeleza. Wakati mwingine tunalazimika hata kuufungua tena mwili ili waone vitu vyao vipo,” amesema Angela.
Angela amesimulia kisa hiki cha kushangaza katika kazi:
“Tulikutana na kesi kama hiyo moja. Ndugu wa marehemu walikuta tumekata kichwani wakalazimisha kuona, kwa sababu wameambiwa tumechukua ubongo.
“Ikabidi tufungue mwili ili wahakikishe kama upo, na wengine wakapiga hata picha kuwaonesha nyumbani kwamba ubongo upo,” amesimulia.
Jamii inavyomchukulia
Licha ya yote hayo, Angela amesema kwa sasa mwitikio ni mkubwa kwa mabinti kujikita kwenye taaluma hiyo ya pathology.
“Unajua kuna dhana nyingi kwenye jamii. Hata mimi mwenyewe, wakati nakua, sikuwahi kupenda kabisa kutembelea hospitali wala mochwari.
“Achilia mbali mimi, ndugu, yaani watu wanakushangaa na kuna baadhi wanashangaa kwanini uchague kwenda kufanya kazi na maiti, wanauliza mwanamke unafanyaje,” amesema.
Angela ameeleza lengo kuu la kazi yake ni kuisaidia jamii.
“Lakini mwisho wa siku upo pale kwa ajili ya kuwasaidia wale waliofiwa. Uko pale kwa ajili ya kufanya kitu ulichokipenda, hata kama kuna dhana na hofu mbalimbali.
“Kwa sasa tuko wengi wanawake ambao ni mapathologist hapa Muhimbili, wanawake ni wengi kuliko wanaume. Zamani watu wengi walikuwa wanaogopa,” amesema Angela.
Aidha, alipinga madai ya baadhi ya watu kwamba wanaofanya kazi mochwari hujihusisha na ulevi.
“Mochwari kuna kada nyingi. Kada ya kwanza ni ‘specialist’, ambao ndio sisi. Kuna ‘attendant’, ambao wao wanashinda kule mochwari zaidi.
“Suala la kunywa pombe haliendani na kazi. Hilo linaendana na mtu binafsi. Mfano hapa kwetu, tunaofanya postmortem hakuna anayekunywa pombe,” amesema Angela.
Sababu maiti kufukuliwa kufanyiwa uchunguzi?
Yapo maswali mengi kwa baadhi ya watu, wakihoji inawezekana vipi mwili uliozikwa kufukuliwa kwa ajili ya uchunguzi na kisha kutoa majibu sahihi. Daktari huyu amefafanua hilo.
“Kesi hizo ni chache, lakini zinatokea kwa sababu mwili kabla haujazikwa tunaweka ‘formalin’, ambayo huwezesha kitu kilichoonekana awali kubaki hadi mwili utakapoharibika.
“Uharibifu hutegemeana na sehemu ambayo mwili utapozikwa. Kwa hiyo ukifukuliwa baada ya muda mchache, tunaweza kukuta baadhi ya vitu havijaharibika,” amesema Angela na kuongeza:
“Mara nyingi kesi za DNA unaweza ukatumia nywele ambayo utaikuta, jino au kwenye mikono,” ameeleza.
Amesema wakati mwingine katika uchunguzi hujikuta wakigundua vitu ambavyo awali havikudhaniwa.
“Huwa tunagundua vitu ambavyo hata mtaani hawakujua. Wanaweza kusema mtu kapigwa, lakini ukija kupima unagundua kumbe mtu alikuwa na TB ya ubongo.
“Lakini awali watu walisema amepigwa. Unaweza kukuta hata mtu hadi kawekwa ndani. Kwa hiyo unakuwa umesaidia watu wawili,” amesema Angela.
Wanavyotofautisha vifo
Kupitia njia za kitaalamu, sababu za vifo hutofautiana. Angela anafafanua namna wanavyofanya.
“Wakati tunasoma, pale ndipo tunafundishwa namna ya kutofautisha ili kujua kifo cha kisu, jiwe au sumu. Kwa hiyo kama ni sumu, unachukua baadhi ya vitu kwenye ini kwa sababu lazima sumu itakuwepo, inapelekwa kwa Mkemia Mkuu kupitia polisi.
“Kisha yeye ndio anatuletea majibu kuwa wamekuta viashiria fulani. Na kama kafa kwa risasi, uzuri huwa tunaikuta kisha tunaikabidhi kwa polisi. Wanaenda kuangalia na wanakuja na majibu. Lakini wewe mwenyewe unaweza kuangalia kama kapigwa akiwa mbali au karibu kutokana na viashiria,” amesema.
Upande wa mtu aliyefariki kwa maji, Angela amesema majibu huweza kupatikana kwa kuufungua mwili.
Aidha, Angela amesema zipo familia ambazo hupinga ndugu yao kufanyiwa uchunguzi.
“Familia za hivyo huwa zina sababu zao. Wengine wanasema ndugu yao wanajua ni mlevi alianguka tu mtaani. Wengine wanasema ameshakufa, hata postmortem haitamfufua. Wanakuja na maelezo kutoka polisi na barua kwamba hawatafanya,” amesema Angela.
Hatosahau
Amesema katika uchunguzi wa maiti, kuna tukio alilowahi kukutana nalo lililomuachia funzo.
“Kuna tukio moja la muda kidogo, mdada alikuwa ameletwa, wanasema amepigwa na mume wake, ameumia. Wengine wakasema amechomwa visu.
“Katika uchunguzi, ile kuufungua mwili wake, tukakuta ana TB, mapafu yote yameliwa. Kumbe yule mama alikuwa anaumwa. Ndugu wanasema alikuwa na ugomvi na mumewe, kwa hiyo mumewe ndio atakuwa amemuua,” amesema Angela na kuongeza:
“Yule baba ikabidi aachiwe na marehemu akazikwe, na ndugu wakakubali. Maana kuna wakati inabidi uwaite ndugu uwaeleze na wajionee,” ameeleza.
Tukio hilo amesema limempa funzo kuwa jamii iwe inapambana kujua chanzo cha kifo ili kuepuka baadhi ya migogoro.
“Hakuna marehemu anayekufa bila kuwa na chanzo cha kifo. Kwa hiyo zile ugomvi za mtaani zinatakiwa ziishe kwa kufanya uchunguzi.
“Kuna wengine wanazika tu lakini moyoni wanahisi fulani ndiye kamuua ndugu yao. Lakini wakifanya uchunguzi wanajua kabisa ni kitu gani kilichomuua,” amesema Angela.
Siku 14 uchunguzi hukamilika
Daktari huyo mzaliwa wa Mbeya amesema katika utendaji kazi wao ushirikishanaji ni jambo la msingi.
“Kwenye kesi tata, ukiona wewe umeshindwa, unaita wenzio, tunaweza kufanya hadi kumi. Mnaweza kuwa jopo, na ripoti ikiandikwa majina ya wataalamu wote yanakuwa pale. Kesi tata tukizipata tunaweza hata kuzipangia siku.
“Tunawaomba ndugu wakikubali tunafanya, tunashauriana hadi majibu yanatoka. Mwili kama hatujachukua sampuli kupeleka kwa Mkemia Mkuu au kinyama kwa ajili ya uchunguzi, ni siku 14 unatakiwa kuwa kwa wahusika.”
Amesema kama kuna utata, inakuwa changamoto kwa sababu lazima wasubiri majibu ya Mkemia Mkuu na maabara ya Muhimbili ili watoe uamuzi.
“Majibu yakichelewa yanaweza kwenda mpaka mwezi, lakini haimaanishi kwamba huo muda mnaosubiri ripoti mwili unabaki Muhimbili, hapana.
“Tukimaliza uchunguzi wanaandikiwa kibali cha kufanya mazishi. Hapo tunakuwa tumeshachukua sampuli. Mawasiliano yanabaki kwa polisi na daktari,” amesema.
Amefafanua kuwa polisi ndiye anakuwa katikati ya daktari na ndugu katika mawasiliano, hivyo kama ni kesi ya kwenda mahakamani, daktari atatakiwa kwenda kutoa ushahidi, kwani yeye ni shahidi mtaalamu (expert witness).
Vifo vya ajali za bodaboda vimekithiri
Angela amesema vifo vingi wanavyokutana navyo ni ajali za bodaboda.
“Elimu inatakiwa itolewe kwa jamii, na pia nafikiri bodaboda wengi hawana elimu ya jinsi ya kutembea barabarani. Jamii ambayo ni wapandaji wa usafiri huo tukumbuke kuvaa helmeti, kwa sababu hata vifo vingi ni kuumia kwenye kichwa au ubongo,” amesema Angela.
Miaka 10 darasani
Angela amewataka vijana kuacha uoga wa kuingia kwenye sekta ya afya.
Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa (Pathologist) kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Angela Kipesile (kulia), akifanya mahojiano na mwandishi wa habari wa gazeti hili (kushoto).
“Katika upande wa afya, kila sehemu panatisha. Siyo hapa tu, kwa sababu hata ukimfikiria yule mtu anayefanya upasuaji naye yupo kwenye changamoto. Mtu yupo hai, unatakiwa umpasue arudi kuwa hai.
“Kwa hiyo nashauri kazi ni kazi. Hakuna haja ya kuchagua kazi. Na pathology inavutia sana, tunakutana na magonjwa mengine kwenye ‘microscope’ mpaka tunashangaa. Maana tumeyasoma tu kwenye vitabu, lakini tunayakuta. Kama vijana wanapenda, waje, ni fani nzuri na ina watu wengi,” amesema Angela.
Akizungumzia kuhusu safari ya elimu, amesema imechukua miaka kumi.
“Kusoma digrii ni miaka mitano, masters mitatu. Kama unataka kufanya special unaweza kufanya MSE miaka mitatu au ‘fellowship’ mwaka mmoja, na bado ‘internship’ ni kama miaka kumi hivi,” amesema Angela.
Itaendelea kesho.