Prime
Vifo, kutoweka watumishi sekta ya afya vyaibua hofu

Muktasari:
- Mwishoni mwa wiki, mwili wa aliyekuwa mfamasia katika Kituo cha Afya Isansa wilayani Mbozi, Daudi Kwibuja, pia ulikutwa kando mwa barabara ya Tunduma – Mbeya, eneo la Mlowo ukiwa umejaa majeraha ikidaiwa alifariki dunia Julai 3, 2024.
Arusha/Moshi. Nini kimewapata? Ndilo swali linaloumiza vichwa vya wengi baada ya mwili wa muuguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Meru kuokotwa Mto Nduruma, huku muuguzi mwingine wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC akitoweka.
Itakumbukwa mwishoni mwa wiki, mwili wa aliyekuwa mfamasia katika Kituo cha Afya Isansa wilayani Mbozi, Daudi Kwibuja, ulikutwa kando mwa barabara ya Tunduma – Mbeya, eneo la Mlowo, ukiwa na majeraha ikidaiwa alifariki dunia Julai 3, 2024.
Taarifa ya kamanda wa polisi mkoani humo, Agustino Senga, ilieleza uchunguzi wa awali ulibaini aliuawa usiku wa Julai 3, 2024 kabla ya kuokotwa asubuhi yake.
Alieleza awali ilidhaniwa alikufa kwa ajali ya gari, lakini baada ya mwili kuchunguzwa ulikutwa na majeraha ambayo hayafanani na ajali ya kugongwa na kuahidi kuendelea na uchunguzi.
Mkoani Arusha, mwili wa muuguzi mwandamizi katika Hospitali ya Wilaya ya Meru, Elinsia Japhet Uronu (44) nao umeokotwa katika Mto Nduruma ukiwa umeharibika, ikiwa ni siku saba tangu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Mwili huo ulitambuliwa na muuguzi mwenzake kwa mavazi aliyokuwa amevaa pamoja na nywele alizokuwa amesuka kwa mara ya mwisho.
Elinsia aliyekuwa akihudumia zaidi wagonjwa wa nje, alitoweka Juni 27, 2024 nyumbani kwake, kabla ya mwili wake kukutwa umeharibika Julai 4, 2024 kando mwa Mto Nduruma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema upelelezi unaendelea.
"Tunaendelea na upelelezi ili kujua kifo hicho ni cha kawaida au kuna kitu kimesababisha," amesema Masejo.
Wakati hayo yakijiri, mkoani Kilimanjaro, Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi, leo Jumapili Julai 7, 2024 imetoa taarifa kwa umma kuhusu kupotea kwa muuguzi wa hospitali hiyo, Lenga Ng’hajabu tangu Julai 4, 2024.
Kauli ya rais wa Tanna
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, wakati wakiaga mwili huo leo Jumapili, Julai 7, 2024, Makamu wa rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), Jane Barakuliliza amesema matukio ya vifo vya kutatanisha kwa wauguzi wa Arusha yanaogopesha na kutia mashaka.
"Kwa miaka hii miwili, jumla ya wauguzi watatu wamekufa vifo vya kutatanisha, ikiwemo kufia ndani, kujinyonga na leo mwili huu kukutwa mtoni, zaidi ya kilomita 20 kutoka nyumbani kwake," amesema Bararukuliliza.
Ameiomba Serikali na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuongeza ulinzi kwa wauguzi wa afya pamoja na kuharakisha uchunguzi, ili kujua chanzo cha kifo hicho.
Kwa mujibu wa Barakuliliza, katika tukio hilo kumekuwa na uzembe wa baadhi ya viongozi wa kituo chake cha kazi, kwani walipaswa kuchukua hatua haraka za kumtafuta mara walipobaini haonekani kazini.
"Wafawidhi jueni nyie ni walezi, hivyo muuguzi kutoonekana kituo cha kazi kwa siku moja au mbili ni utovu wa nidhamu, hivyo ingefaa ijulikane na hatua zingechukuliwa mapema si ajabu tungeweza kuokoa maisha yake,” amesema.
Dada, wafanyakazi wenzake wafunguka
Dada wa marehemu, Alice Uronu ameiambia Mwananchi kuwa Julai 3, 2024 alipata taarifa ya dada yake kutoonekana kazini.
Amesema walianza kumsaka kwa ndugu bila mafanikio kabla ya siku iliyofuata kupata taarifa za mwili wake kukutwa kando mwa mto Nduruma. "Dada yangu ameacha watoto wawili aliozaa na mume wake waliyeachana siku nyingi kutokana na kutoelewana na hatujawahi kusikia kama kuna mmoja kati yao anamfuatilia mwenzake," amedai Alice alipozungumza na Mwananchi.
Kwa upande wake, Monica Gwandu aliyekuwa anafanya kazi na marehemu amesema alifanikiwa kumtambua kwa nguo alizokuwa amevaa pamoja na nywele alizosuka siku ya mwisho kuonana naye.
Muuguzi KCMC atoweka
Muuguzi wa afya katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kaskazini ya KCMC, Ng'hajabu anadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, baada ya kutoonekana kazini kwa siku nne mfululizo huku simu zake za mkononi zikiwa hazipatikani.
Ng'hajabu ambaye ni muuguzi katika idara ya masikio, pua na koo katika hospitali hiyo, anadaiwa kutoonekana kazini tangu Julai 4, 2024 na hadi jana alikuwa hajulikani alipo wala kufahamu kilichokuwa kimempata.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Julai 7, 2024, Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Gabriel Chisseo, amesema muuguzi huyo alipokwenda mapumziko ya siku, Julai 2 na 3, hakurejea kazini.
Amesema Julai 4, siku aliyopaswa kurejea kazini, hakuripoti na simu zake zilipopigwa hazikupatikana.
"Alikuwa na mapumziko ya siku mbili na Julai 4 ilitakiwa aripoti kazini, hakutokea hata Julai 5 pia hakuonekana, tukaona hii si kawaida na kilichotushtua zaidi simu zake kila tukipiga hazipatikani," amesema Chisseo.
Hata hivyo, amesema walichukua hatua ya kutafuta eneo alilokuwa anaishi na walipofika walimwomba mwenye nyumba wake awaruhusu kuingia ndani, hawakumkuta japo mlango ulikuwa haujafungwa na funguo.
“Tulikuta vitu vyake vyote vipo, ila wote wanaomzunguka, wakiwemo majirani walisema hawajui alipo," amesema Chisseo katika mahojiano hayo.
Amesema walitoa taarifa Kituo cha Polisi Longuo B wakapatiwa RB namba, wanaendelea kumtafuta.
"Tunamtafuta kwa nia njema kwa sababu anakoishi hayupo, hivyo tunaona tutoe tangazo kwa sababu hata namba ambazo tunazo za ndugu kwenye faili lake la ajira hazipatikani," amesema.
Mmoja wa majirani zake, Robert Mwakalinga, amesema muuguzi huyo aliondoka usiku wa Julai 2, 2024 na hakuaga anakokwenda na mpaka leo hajarejea.
“Hatujui nini kimemtokea kwa sababu si jambo la kawaida,” amesema.