Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vifo ajali ya basi la Shabiby, lori Iringa vyafikia sita

Muktasari:

  • Idadi ya vifo imeongezeka hadi sita huku familia mbalimbali zinaendelea na taratibu za kuwasafirisha wapendwa wao waliofariki dunia.

Iringa. Idadi ya vifo katika ajali ya barabarani iliyohusisha basi la Kampuni ya Shabiby na lori la vinywaji baridi katika mteremko hatari wa Tanangozi, imeongezeka na kufika sita baada ya majeruhi mwingine raia wa India kufariki njiani wakati akisafirishwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matubabi zaidi.

Pia, ajali hiyo ajali hiyo iliyotokea alfajiri Mei 8, 2026 katika Barabara ya Tanzania-Zambia eneo la Tanangozi, Kata ya Maseke mkoani Iringa imesababisha vifo vya madereva wawili, kondakta na utingo.

Waliofariki dunia ni dereva na utingo wa lori na dereva na kondakta wa basi la Kampuni ya Shabiby.

Ajali hiyo iliyohusisha basi la Shabiby aina ya Youtong lililokuwa likitokea Dodoma kuelekea Mbeya  na lori aina ya Faw lenye tera lililokuwa limebeba vinywaji kutoka Mbeya kwenda Dodoma na kusababisha vifo vitano na majeruhi 28.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 9, 2026, Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela amesema kuwa miili ya watu watatu imechukuliwa na ndugu zao.

Mwakalebela amesema kati ya waliofariki dunia, wawili walikuwa ndugu, ambao ni dereva na utingo wa Lori lililopata ajali.

Amesema majeruhi wa tatu aliyefariki dunia imeelezwa kuwa alikuwa rafiki yao (dereva na utingo), ingawa hadi sasa bado haijafahamika alikuwa akielekea wapi wala sababu ya safari yake.

“Maiti tatu zimehukuliwa na wenyeji wa Tanga pamoja na ndugu zao na wawili ni ndugu ambao ni dereva na kondakta, na mmoja ni rafiki yao ambaye haijafamika alikuwa anaenda wapi na kwa ajili gani sasa sijuhi walimchukua kwamba rafiki yao pia akatembee tembee au laa ,” amesema Dk Mwakalebela.

Pia, Mwakalebela amesema idadi ya vifo imeongezeka kutoka watano hadi sita baada ya mmoja wa majeruhi, raia mwenye asili ya India, kufariki dunia akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Raia huyo wa India alikuwa nchini kwa shughuli za kikazi katika moja ya kampuni za Dar es Salaam. Wenzake wa karibu walimtambua kwa shida kutokana na mwili wake kuathirika vibaya kutokana na nguvu ya mgongano kwenye ajali.

 “Kinachoniuma zaidi ni namna mfumo wa tiketi za mabasi bado hauwasaidii watu kutambulika kirahisi na watu wanaposafiri taarifa zao nyingi hazihifadhiwi vizuri, hivyo ajali zinapotokea familia hupata shida sana,” amesema Zaini Mukadam maarufu kama Kazaroho, ambaye ni Matanzania mwenye asilia ya Asia anayeishi Iringa.

“Nilipigiwa simu na watu kutoka India wakaniambia niikague maiti hiyo kifuani kwa kuwa alikuwa na alama maalumu. Baada ya ukaguzi ndipo ikathibitika kuwa ni yeye,” ameongeza.

Mukadam amesema tayari wamewasiliana na ubalozi wa India nchini Tanzania kusaidia taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu huyo kurejeshwa nchini India.

“Ni muhimu watu wakaacha taarifa wanaposafiri na kuwaeleza ndugu zao wamepanda gari gani na wanaelekea wapi, kwa sababu ajali haina taarifa,” alisema huku akionekana kuguswa na tukio hilo.

Akizungumzia hali za majeruhi, Mwakalebela amesema kati ya majeruhi 17 waliolazwa siku ya kwanza, sita wameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali zao kuimarika, huku wengine wakiendelea na matibabu chini ya uangalizi maalumu.

Amesema mwanaume mmoja anaendelea kutibiwa tatizo la kifua ambapo madaktari wamemuwekea mpira maalumu wa kutoa maji na usaha, huku mwingine akiwa ameumia vibaya jicho na madaktari wakijitahidi kuokoa uwezo wake wa kuona.

Miongoni mwa majerugi hao ambao wamelazwa wodini ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Beni Lilawola, aliyekuwa akiendelea kupatiwa matibabu ya jicho lake la kulia.

Pia, majeruhi mwingine ni mwalimu wa shule ya sekondari kutoka Songwe, Juma Shaabani, ambaye licha ya kuwa na michubuko usoni, amesema kinachomuumiza zaidi ni kumbukumbu za tukio hilo.

“Tulikuwa usingizini, ghafla nikasikia mlio mkubwa sana. Baada ya hapo sikuelewa tena kilichoendelea,” alisema kwa tabu.

Majeruhi wengine waliolazwa wodini ni Elias Mwakioloma, mfanyakazi wa mgodi kutoka Nyamongo, Tarime, ambaye alisema hajui kilichotokea hadi alipojitambua hospitalini.

“Nimepoteza kila kitu. Sioni laptop yangu wala simu yangu ya iPhone Max, sijui zilipo,” alisema kwa huzuni huku akitazama dirishani.