VIDEO: Simulizi ya mama alivyoshuhudia wanae pacha wakitenganishwa-1

Hadija Shaban akishukuru Mungu baada ya upasuaji wa kuwatenganisha watoto wake Hussein na Hassan kukamilika salama katika hospitali iliyopo nchini Saudi Arabia. Picha Na Mpigapicha Maalumu
Muktasari:
- Asilimua alivyoshuhudia saa 16 za upasuaji kutenganishwa wanawe, changamoto ya mawasiliano na vyakula.
Dar es Salaam. Ni alfajiri ya Agosti 25, 2021 katika Kijiji cha Kifulumo, Kata ya Sungwizi wilayani Igunga, mkoani Tabora, Hadija Shaban alipohisi uchungu wa kujifungua.
Tofauti na uchungu aliopitia mwaka 2018 alipojifungua mwanaye wa kwanza, Hadija mwenye miaka 24, anasema:
“Nilikuwa na maumivu makali, nikampigia mama kuhusu hali yangu. Walichukua muda mrefu kufika, wakijua nitajifungulia nyumbani.”
Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika Desemba 13, 2024 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hadija anasema mume wake, Amir Jumanne alimpeleka katika Zahanati ya Sungwizi iliyopo kilomita 10 kutoka kijiji wanachoishi kwa usafiri wa pikipiki.
Akiwa zahanati, anaeleza uchungu uliongezeka lakini badala ya tumbo kushuka kuashiria kujifungua, lake lilipanda juu. Kutokana na hali hiyo alipewa rufaa ya kwenda hospitali yenye uwezo zaidi.
Anaeleza mume wake alimfuata mama yake katika Kijiji cha Mzanza kisha wakampeleka Hospitali ya Misheni ya Nkinga, iliyopo umbali wa kilomita 19.7 kutoka Zahanati ya Sungwizi.
“Ninaambiwa nilipoteza fahamu tukiwa njiani, nilikuwa nimechoka sana usiku wa Agosti 26. Nilipozinduka nilitambua kuwa nimefanyiwa upasuaji.
“Sikuona mtoto, kila nikiuliza mtoto wangu yuko wapi naambiwa watoto wako wapo salama. Nikajiuliza watoto? Mbona nilipima mimba kliniki mpaka wakati wa kujifungua sikuambiwa nina mapacha? Muda wote nikawa najiuliza mbona watoto siwaoni au kuna jambo jingine? Nikakaa kimya,” anasema.

Hadija Shabani (katikati) akiwa na watoto wake pacha, Hussein na Hassan katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam wakitokea Saudi Arabia baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha nchini humo. kushoto ni Mkurugenzi huduma za upasuaji Muhimbili, Dk Rachael Mhavile. Picha na Maktaba
Anasimulia: “Nilipouliza tena walisema tutakuonyesha watoto wako, tumewapeleka kule hawapo vizuri sana, nikawaambia sawa. Mama yangu alikuwa anakamua maziwa wanapelekewa, baada ya siku nne wakaniambia leo utawaona watoto.”
Anasimulia kabla ya kwenda kuwaona alijulishwa kuwa wameungana.
“Nilishtuka, lakini nikamshukuru Mungu kwa kuwa ndiye ajuaye kila kitu,” anasema.
Anaeleza walilazwa wodi ya watoto njiti, ambako alikuwa anakwenda kuwanywesha maziwa. Mama yake alimweleza hakumjulisha hali ya wanawe kwa kuwa alizuiwa kutoa taarifa.
“Mama alisema alizuiwa kusema chochote kwa kuwa nilikuwa nimetoka kufanyiwa upasuaji, walisubiri niwe sawa ndipo waniambie,” anasema.
Anasema siku saba tangu alipojulishwa kuwa watoto wameungana alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa Tabora na baadaye ukafanyika utaratibu wa kwenda Muhimbili.
Awali, anasimulia walifika maofisa ustawi wa jamii ndipo baadaye ambulensi lilipofika wakaanza safari ya Muhimbili.
Anasema kwa kipindi hicho chote mumewe alikuwa anajua watoto wao, Hussen na Hassan Amir ambao kwa sasa wana miaka mitatu wameungana.
“Alikuwa anakuja kuwaona na kuondoka lakini tangu nimekuja Dar es Salaam alikata mawasiliano,” anasema Hadija aliyefunga ndoa na Amir Said mwaka 2017.
Anasema tangu alipoondoka Hospitali ya Nkinga, hakuwahi tena kuwasiliana na mume wake na sasa ni miaka mitatu.
Hadija anasema Muhimbili alikaa mwaka mmoja na miezi tisa ndipo wakaondoka kwenda Saudi Arabia alikokaa mwaka mmoja na miezi miwili.
Anasema Muhimbili watoto walikaa ili watimize uzito uliohitajika na kwamba, kuliibuka hali ya sintofahamu kutokana na mmoja kunenepa, huku mwingine akikonda.
“Ilikuwa shida, mmoja anakula mwingine hataki kula, lakini ambaye hataki kula akawa ananenepa, huyu anayekula anakonda. Hata sasa yule aliyekuwa hataki kula ndiye mwenye mwili kuliko mwenzake,” anasimulia.
Maisha Saudi Arabia
Hadija aliyeolewa akiwa na umri wa miaka 18, anasema alipoambiwa safari ya kwenda kuwatenganishwa watoto wake imewadia, aliingiwa woga, lakini alifurahi na kuomba Mungu jambo hilo likamilike salama.
“Nilijisikia furaha lakini nilikuwa nawaza maisha ya watoto wangu, Mungu awasaidie wapone nilikuwa nawaza lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu alitenda,” anasema.
Anasimulia namna vyakula vilivyompa shida kwa kuwa ni tofauti na vya nyumbani kwao.
Akiwa huko anasema hakuwahi kukosa nyama na mbogamboga lakini hakupata ugali na maharage, vyakula alivyozoea alipokuwa nyumbani.
“Saudi Arabia hakuna ugali, ni wali na vingine kama viazi. Uji hamna, mimi na watoto tulikuwa tunapewa maziwa, wali, nyama, matunda, mbogamboga pia hazikosekani. Watoto walipikiwa supu, wanapewa maziwa freshi na juisi,” anasema.
Mbali ya chakula, anasema mawasiliano yalikuwa kikwazo, hivyo alishindwa kuwasiliana na madaktari, wauguzi na hata wahudumu wa hoteli aliyokuwa akiishi.
Anasema alikuwa akiwasiliana kwa simu na Dk Zaitun Bokhari (daktari bingwa wa upasuaji wa watoto Muhimbili) aliyezungumza na wahusika kisha alimtafsiria.
“Dk Zaituni amenisaidia, sikusoma vidato, ingawaje najua kusoma na kuandika, sijui Kiingereza wala Kiarabu, yeye amekuwa mkalimani wangu.
“Amenisaidia kuongea na wataalamu kule Saudi Arabia wanampa taarifa anarudi kwangu ananiambia wamesema hivi, hata aliporudi Tanzania nilikaa mbali naye, tulikuwa tunafanya hivyo kwa simu,” anasimulia.
Anasema kabla Dk Zaituni hajarudi Tanzania, alimfundisha kutumia Google kutafsiri lugha, hiyo ikamsaidia kuwasiliana.
“Nilikuwa nampigia Dk Zaituni wanaongea naye ananitafsiria, nyakati zingine nilikuwa naona labda nikimpigia simu nitamsumbua labda ni suala dogo, natumia Google inanitafsiria, anaongea inaniletea tafsiri kwa Kiswahili, nasoma naelewa namjibu pia kwa Kiswahili, inamtafsiria kwa Kiarabu au Kiingereza,” anasimulia.
Anasema aliweza pia kujifunza Kiarabu kidogo kwa kuwa alisoma madrasa.
Hadija anasema ilichukua muda wa mwezi mmoja na wiki kadhaa watoto wake kutenganishwa: “Tulikwenda Agosti, ilipofika Oktoba ndipo watoto wakatenganishwa.”
Anasilimua Oktoba 05, 2023 haitaisahau, kwa zaidi ya saa 16 alikaa kwa wasiwasi mwingi na woga, akishindwa kula chochote zaidi ya kuomba dua watoto wake walipokuwa wakitenganishwa.
Upasuaji ulihusisha jopo la madaktari katika mjini wa Riyadh, Saudi Arabia.
Kazi ya kuwatenganisha ilikuwa na hatua tisa zikihusisha timu ya madaktari wabobezi, wataalamu na wauguzi 35 katika Hospitali ya Watoto ya King Abdullah, wakiongozwa na Dk Abdullah Rabeen.
Anasema alishuhudia watoto wake wakitenganishwa kupitia dirisha lenye kioo: “Walivyopelekwa chumba cha upasuaji walitumia saa 16 asubuhi mpaka usiku, maana walikuwa na miguu mitatu, waliungana nyonga, tumbo na viungo vingine.”
“Nilikuwa nawaona kupitia kioo, unaona kila kitu tangu wanakata mpaka wanashona, wanatenganishwa niliona kila kitu. Ilikuwa inanitisha lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu alinipa ujasiri nilishinda.
"Namshukuru Mungu watoto wangu wametenganishwa na wanaendelea vizuri, haikuwa rahisi nilikuwa na wakati mgumu," anasema.
Anasema alifurahi alipoona wanaachanishwa kila mmoja anapelekwa kitanda chake kwa hatua zingine za upasuaji.
Hadija anasema alikaa pembeni kwa muda, kisha akarejea akaona kila mmoja amelazwa kitanda chake na mashine zinaonyesha wapo hai.
Anasema wiki moja baada ya upasuaji mmoja alitoka ICU akabaki mmoja.
“Amerudi chumba cha upasuaji mara kwa mara, yapata mara sita hivi, baadaye akakaa sawa akatoka ICU. Huyu ni Hassan. Hussein alitoka mapema na hajawahi kurudishwa chumba cha upasuaji tangu walipotenganishwa,” anasema.
Baada ya upasuaji wa watoto, anasema walikuwa chini ya uangalizi wa wataalamu naye alikuwa akiishi hotelini.
“Nilipofika nilikuwa nakaa hospitalini, watoto walipofanyiwa upasuaji nikapelekwa hotelini, nilikuwa nakwenda kuwaona narudishwa hotelini. Watoto walipokaa vizuri nilikakaa nao hotelini wakawa wananichukua kwenda hospitali kisha tunarudi tena hotelini,” anasema.
Anasema watoto waliporuhusiwa kula walipewa maziwa, viazi, wali na supu na nyakati zingine juisi na matunda, maisha waliyoishi kwa mwaka mmoja na miezi miwili tangu walipotenganishwa.
Itaendelea kesho…