VIDEO: Samia alia na utekaji, aomba machifu wasaidie

Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na baadhi ya machifu kutoka mikoa mbalimbali nchini, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma Julai 20, 2024.
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amesema vimeibuka vitendo vya uhalifu vya utekaji na mauaji ya watu wenye ualibino, akiwa akiwaomba machifu wasaidie kuyazuia kutoka ngazi ya chini.
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na taarifa za watu kupotea, kutekwa, kujeruhiwa na kuuawa kwa watu wenye ualibino, Rais Samia Suluhu Hassan amewaomba machifu na viongozi wa mila kukemea vitendo hivyo katika ngazi za chini wanakotoka.
Kauli ya Rais Samia wakati kukiwa na taarifa za kutekwa kwa watu wakiwamo watoto na watu wenye ualbino likiwemo tukio la mtoto Asimwe Novath aliyetekwa na hatimaye kuuawa wilayani Muleba Mkoa wa Kagera Juni 17, 2024.
Matukio mengine yamelihusisha Jeshi la Polisi, likiwemo la kukamatwa kwa kada wa Chadema, Kombo Mbwana aliyekamatwa nyumbani kwake Kwamsala wilayani Hadeni Mkoa wa Tanga Juni 15, 2024, lakini Julai 14, 2024, Polisi Tanga walitangaza kumshikilia.
Tukio lingine ni la kutekwa kwa Edgar Mwakabela, maarufu Sativa tangu Juni 23, 2024, ambapo katika maelezo yake kwa vyombo vya habari, alidai alipotekwa alipelekwa kituo cha Polisi Oysterbay na kuwekwa katika karakana ya kituo hicho na kusafirishwa kwenda Arusha na kisha akaenda kutupwa katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi alikookotwa akiwa na majeraha.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari akiwa ziarani Mkoa wa Simiyu Julai 15, 2024, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camilius Wambura alikanusha taarifa zinazolihusisha jeshi hilo na vitendo vya utekaji wa watu.
Akizungumza na machifu nchini katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo 20, 2024, Rais Samia amesema mauaji ya watu wenye ualbino na utekaji yameibuka upya na yanaichafua Tanzania.
“Nadhani tunasikia sasa hivi, kuna vitendo vingi vya uhalifu, tayari kulikuwa kimya sasa hivi unaanza maalbino, mara kakatwa mkono, mara kakatwa kiuongo, mata katolewa nini,” amesema.
Ametoa mfano wa mtoto (hakumtaja) aliyeokotwa jijini Dodoma akiwa wakiwa hana mkono na sehemu za siri.
“Sijui ukisikia huku, watoto wamepotea, sijui ukienda huku, sasa hili wimbi hili linapotokea, lawama kubwa ni kwa Serikali pengine na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Lakini tuna viongozi ngazi ya chini wa Serikali na wa kimila wako kule chini, mambo yanatokea tunayatazama, hatuyazungumzi, hatusemi, hatuhoji.
“Yanatokea tu yanarushwa kwenye vyombo vya habari leo kule kesho kule, lakini Watanzania tupo na viongozi wapo, wa Serikali, wa kidini, viongozi wa mila tupo, viongozi wengine tupo, lakini yanatokea.
“Hii sio Tanzania tunayoitaka, niwaombe machifu wenzangu, tulinde watoto wetu, tulinde kutumia mila na desturi zetu,” amesema.
Amewataka machifu kuwaelimisha watu wenye imani za kishirikina akisema vyeo havipatikani kwa kuua watu.
“Mtoaji madaraka ni Mungu, akitaka kukupa utapata, unaweza ukaua watu 10 na unalotaka usipate,” amesema.
Kuhusu utekaji wa watu amesema kila matukio yanapotokea, lawama zinakwenda kwa Serikali, huku akigusia baadhi ya matukio.
“Utasikia mtoto alijiteka mwenyewe, anapiga simu kwao pesa zitoke, huku mama kamtekesha mwanaye ili baba atoe pesa, mwingine sijui na nani. Yaani vidude vya drama drama tu, lakini vinavyoandikwa kwenye vyombo vya habari na kwenye magazeti, kama Serikali imelala watu wanatekwa hovyo tu.”
Amewataka machifu kukemea mambo hayo yasitokee kwenye maeneo yao.
“Haya mambo yanatokea kwenye maeneo yetu, tukayasemee kule, tuwaonye kule tuwakanye kule ili yasitokee.
“Pamoja na kwamba sisi Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama tumesimama kufanya kazi zetu, lakini tunaomba msaada kutoka kwenu ili yale mambo yazuilike kutoka ngazi ya chini,” amesema.
Kauli ya Rais Samia imekuja wakati kukiwa na tahadhari zilizotolewa na baadhi ya shule jijini Dar es Salaam kupitia mitandao ya jamii jana Julai 19, 2024, kwa wazazi na walezi kuwalinda watoto wao waendapo na wanaporudi kutoka shule.
Moja ya taarifa zilizosambaa mitandaoni jana, ilidai kuwepo kwa tukio la kutekwa kwa mtoto aliyekutwa kwenye kwenye kiroba akiwa amefariki dunia na kuwepo kwa mwili wa mtu mzima uliookotwa eneo la Kibada Kigamboni Dar es Salaam.
Hata hivyo, kupitia taarifa iliyotolewa jana Julai 19, 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amewaonya watu wanaotoa taarifa za watu kupotea na kutekwa bila kuwa na uhakika nazo.
“Mwezi huu Julai kumejitokeza wimbi la baadhi ya watu wenye nia ovu ambazo hazikubaliki ambapo wanatengeneza taarifa za uongo kuwa eneo fulani watoto wa shule fulani wamechinjwa, kisha kusambaza kwenye mitandao ya jamii,” amesema.
Ameongeza kuwa tabia hiyo pamoja na kwamba ni kosa la jinai, ni tabia ya kulaani na kukemewa kwa nguvu kubwa na kila mmoja.
Maombi ya Machifu
Akizungumza kwa niaba ya machifu wenzake, Chifu Aron Nyamilonda ameshukuru Serikali kukamilisha maombi yao ya kumiliki nyara hizo ambazo ameeleza ni kama Ibada za jadi na utambulisho na kimila.
“Tumepata taarifa za kukamilika kwa sheria kuhusu umiliki wa nyara ambazo sisi machifu tunazitumia katika shughuli mbalimbali za kimili ikiwemo kama zana ya utambulisho wa cheo cha uchifu pamoja na mapambo rasmi ya kiongozi wa kimila,” amesema.
Chifu huyo amesema sheria hiyo siyo muhimu tu kwa machifu bali pia kwa waganga wa tiba asili na wasanii wa ngoma za asili.
Akielezea kuhusu changamoto zinazowakabili machifu nchini, amesema bado baadhi ya watumishi wanashindwa kutafsiri vyema baadhi ya kanuni na sheria zinazosimamia shughuli za kimila.
Chifu Nyamilonda amezitaja sheria hizo kuwa ni pamoja na sheria ya wanyama pori, sheria ya misitu, sheria ya ardhi pamoja na katiba ya nchi ambayo inampa kila mwananchi haki ya uhuru wa kuabudu, kuamini kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi.
Amesema pia, licha ya Serikali kuweka kitengo cha utamaduni kwa ajili ya urithishaji wa utamaduni, kitengo hicho kina uwezo mdogo wa kibajeti kurithisha na kutekeleza mila na desturi licha ya kuwa kina mchango katika kulinda jamii.
Pia, chifu huyo alizungumzia kupatikana kwa kiwanja cha kujenga ofisi za Umoja wa Machifu Dodoma na kueleza mchakato wa upimaji unaendelea ili kumiliki kiwanja hicho kisheria huku akimuomba Rais Samia, kuwashika mkono kuweza kufanya ujenzi wa ofisi hizo.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema alilofanya Rais Samia kukutana na machifu, lilifanywa mara ya mwisho na Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere.
“Mheshimiwa Rais kwa hiki ulichokifanya, inaonyesha wazi kuwa umedhamiria mila na desturi za Watanzania kuzingatiwa,”amesema Dk Ndumbaro.
Hata hivyo amepongeza ushirikiano ambao wamekuwa wakipata kwa machifu na kuieleza yamesaidia kutekeleza shughuli za kiutamaduni nchini ikiwemo kunakofanyika shughuli za kiutamaduni.
Katika kutambua shughuli za machifu, Waziri Ndumbaro amesema wanaandaa mwongozo kwa ajili ya kutambua viongozi hao katika ngazi mbalimbali.
“Lengo ni kuhakikisha kundi hili linapata heshima kutoka kwa jamii yetu, wakiongozwa na Chifu Mkuu, Chifu Hangaya (Rais Samia Suluhu Hassan),” amesema Waziri Ndumbaro.