Prime
VIDEO: Sababu Mchengerwa kupelekwa Tamisemi

Rais Samia Suluhu Hassan, akimuapisha Mohamed Omary Mchengerwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu ndogo Tunguu-Zanzibar leo Septemba Mosi, 2023. Picha na Ikulu
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ametaja sababu ya kumuhamishia Mohammed Mchengerwa katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja sababu za kumhamisha Mohammed Mchengerwa kuwa Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) akisema ni maandalizi kuelekea kivumbi cha mwakani.
Kivumbi hicho, kwa maneno halisi ni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaosimamiwa na Tamisemi.
Uhamisho wa Mchengerwa ulifanyika juzi, akitolewa Wizara ya Maliasili na Utalii aliyohudumu tangu Februari mwaka huu na ni miongoni mwa mawaziri wanne waliobadilishwa wizara.
Pamoja na kusifu utendaji wake katika nafasi alizowahi kumpa, Rais Samia amesema jitihada zake ndizo zilizomfanya ampe nafasi hiyo mpya akiamini anaimudu.
Rais Samia ameyasema hayo Ikulu ndogo ya Zanzibar leo, Septemba 1, 2023 alipohutubia hafla ya uapisho wa viongozi mbalimbali aliowateuwa Agosti 30, mwaka huu.
“Mwakani kuna kivumbi na mimi nakujua najua unaweza, kivumbi kile kinafanana na kifua chako najua unaweza, kwa hiyo nimekupeleka Tamisemi ni kazi kazi ili mwakani tuseme vizuri.
Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi alimeza baadhi ya maneno kuhusu uhamisho huo wa Mchengerwa akisema, “Sitaki kuyachambua hapa wanasema usimwage mtama kwenye ndege wengi,” amesema.
Ameeleza mengine watazungumza zaidi watakapokuwa kwenye kikao kazi kati yake na mawaziri.
Akisifu utendaji wa Mchengerwa, Rais Samia amesema amemtaja kuwa mfano wa mabadiliko akitumia rejea ya alichokifanya kwa mara ya kwanza baada ya kumteuwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
“Tutakapowachambua hapa wengine ni mabingwa wa mabadiliko, nimseme hapa Mchengerwa (Mohammed) kwa mfano, nilipompeleka utumishi mwanzo ninamteuwa, kaingia na kasi kubwa kelele zikawa nyingi.
“Nikasema mmh… labda Waziri wangu kazidi kapandisha mabega, mpeleke michezo, kaenda michezo kazi aliyofanya mnaiona, kaacha kazi nzuri sana, katoka Michezo nimempeleka Utalii.
“Mipango aliyoiweka sekta ile nani anakwenda utalii Angellah, sekta ile ukienda kufuata yaliyowekwa sekta ile mambo yanakwenda kupanda, Hassan (Dk Abbas) yupo pale amefanya kazi nzuri sana wameweka mipango na Waziri kwako ni kusimamia utendaji, yatekelezwe yale yaliyowekwa,” amesema.