VIDEO-IGP Wambura afunguka mikakati mitatu, ataja haki
Muktasari:
- Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillius Wambura amekabidhiwa ofisi leo Jumatano na mtangulizi wake, Simon sirro ambaye ameteuliwa na kuapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Dar es Salaam. Saa chache baada ya Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillius Wambura kuapishwa, amefunguka na kutaja mikakati yake mitatu ikiwemo kukomesha uhalifu na kuzingatia haki na maadili.
IGP Wambura ameitaja mikakati hiyo mikubwa ambayo amepanga kuitekeleza katika utendaji wake leo Jumatano, Julai 20, 2022 mara baada ya kuapishwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Ameapishwa kuchukua nafasi ya Simoni Sirro ambaye ameteuliwa na kuapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Mara baada ya kuripoti Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Dodoma akitokea Ikulu ya Chamwino alipoapishiwa, IGP Sirro amesema mikakati hiyo mikubwa atahakikisha inatekelezwa kwa kushirikiana na makamishna walio chini yake na kada mbalimbali za askari pamoja na viongozi waliopo katika Jeshi la Polisi.
“Kwanza ni kuhakikisha suala la uhalifu, mapambano dhidi ya uhalifu yanaimarishwa na suala la uhalifu, wahalifu wasije wakafiriki kwamba ile ni ajira hakuna hiyo na nguvu ambayo tutatumia kupambana na uhalifu ni akili kubwa, nguvu kubwa lakini nguvu ya kisasa," amesema IGP Wambura
“Na tutahakikisha wananchi wanakuwa salama na Serikali inaweza kuendelea na shughuli zake na kutokuwa na fikra za kuona ni namna gani wataanza tena kushughulika na uhalifu na kuweka rasilimali zao pale,” amesema.
IGP Wambura ambaye kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nafasi ambayo sasa imechukuliwa na Ramadhan Kingai, amesema kazi yake kubwa ni kuhakikisha suala la uhalifu linakoma nchini.
Ametaja jambo la pili ni kushughulika na maadili ndani ya Jeshi la Polisi na kwamba nchi haiwezi kuwa na jeshi zuri, jeshi imara, jeshi la kisasa na lenye weledi kama hakuna maadili ndani yake.
Ametaja jambo la tatu linalohitaji kufanyiwa kazi kwa karibu sana ni haki, haki kwa wananchi, haki katika kila eneo kuanzia katika vituo vya Jeshi la Polisi na mitaani ambako askari wanafanya kazi.
“Tunataka kuona watu wanatendewa haki kwa mujibu wa sheria, lakini kwa mujibu wa taratibu ni baadhi ya mikakati ambayo nitahakikisha inafanyiwa utekelezaji na inakua inasimamiwa na kuhakikisha yote itaweza kuleta tija katika jeshi letu la polisi,” amesema IGP Wambura.
Kabla ya nafasi hizo Wambura amewahi kuwa Mkuu wa upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam mwaka 2019, pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni mwaka 2018.