Rais Samia atangaza panga, pangua majeshini

Rais Samia Suluhu Hassan akimwapisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Camillus Wambura kuwa Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi (IGP) katika Hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma leo Jumatano Julai 20, 2022. Picha na Ikulu
Muktasari:
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kuanza kupitiwa upya mchakato wa upatikanaji wa watendaji katika vyombo vyote vya dola.
Dar es Salaam. Katika kujenga majeshi yenye sifa na hadhi ya kuisimamia nchi, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema wanakwenda kupitia upya upatikanaji wa watendaji katika vyombo vyote vya ulinzi.
Sambamba na hilo wataangalia njia gani zinazotumiwa katika kuwapandishia vyeo vya kitaaluma na madaraka maofisa mbalimbali ndani ya majeshi hayo.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatano, Julai 20, 2022 mara baada ya kumaliza kuwaapisha viongozi aliowateua akiwemo Camillius Wambura kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).
Wambura aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) amechukua nafasi ya Simon Sirro ambaye naye aliuliwa na kuapishwa leo Jumatano kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Wengine walioapishwa ni, Luteni Jenerali, Mathew Mkingule kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia na Dk Suleiman Haji Suleiman.
Rais Samia amesema ameamua hilo lifanyika kutokana na vitendo vinavyofanyika barabarani na Polisi hudhani kama mtu kahitimu mafunzo ya kufanya kazi hiyo kule chuoni.
“Lakini background wanazoingilia, tukipekua na huko kuna feki nyingi tu chungu mzima, kwa hiyo inawezekana hata uwezo wa mtu anayepelekwa haya mafunzo hakuna lakini husikii kashindwa wote wanakwenda, wanahitimu na wanapangiwa kazi,” alisema
Rais huyo wa sita wa Tanzania alisema,“kwa hiyo tunakwenda kutizama na huko upatikanaji wa watenda kazi ukoje kwa majeshi yote, kama yalishapita lakini huko mbele tutachujana vizuri sana ili kujenga majeshi yenye sifa na hadhi ya kuisimamia nchi hii.”
Wakati kuhusu mifumo ya upadishaji vyeo, Rais Samia alisema,“tunakwenda kuangalia mifumo ya upandishaji vyeo vya taaluma kijeshi na vyeo vya madaraka, katika taasisi hizi mifumo ikoje.”
“Huwa nikitoka, nikipita napokaa Ikulu kuna maaskari wanakaa hapa wanajipanga kuniaga, nikiingia wananipokea.”
“Natazama wa mwanzo na wale wanaonifutia wa mwanzo ana vijiwe jiwe hivi, anayenifuatia, the most senior kuliko mwingine lakini bega tupu kama hao wengine wanaomfuata na ni kote, nimetazama Dar es Salaam, nimetazama hapa Dodoma, nimetazama kila ninapokwenda.”
Katika hilo, Rais Samia alifafanua mtu anakaribia kustaafu yupo miaka 59, miaka 57, lakini bega lipo tupu, hata ule ukoplo hana na kufanana na wale wadogo ambao wameungana nao juzi.
“Nikawa nasema upandishaji vyeo kwa hayo majeshi huko ukoje, nadhani tutakwenda sasa kungalia jinsi mnavyopandishana vyeo huko je wanastahiki,” alisema
“Lakini sio kupandishana vyeo tu, mafunzo, kwa kuwa najua ili apandishwe vyeo lazima aende mafunzo, je mafunzo yanafanyika ipasavyo, tutakwenda kuangalia pia na pengine upungufu wa mafunzo, ndio haya mambo tunayoyaona huko barabarana yanayotendeka au yanayokwenda kutendeka,” alisema Rais Samia.