Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Aliyeishi kwa kupumulia mashine afariki dunia

Muktasari:

Hamad Awadh, aliyeishi kwa kutegemea mashine ya kumsaidia kupumua amefariki dunia jana jioni Oktoba 17, 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili  -Mloganzila alikokuwa amelazwa.

Dar es Salaam.  Hamad Awadh, aliyeishi kwa kutegemea mashine ya kumsaidia kupumua amefariki dunia jana jioni Oktoba 17, 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila alikokuwa amelazwa.
Awadh ambaye baada ya Mwananchi kuandika habari kuhusu ugonjwa unaomsumbua alianza kupata misaada kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali amefariki dunia wiki mbili tangu alipolazwa hospitalini hapo Oktoba 4, 2019 kutokana na  maradhi ya kushindwa kupumua na shinikizo la damu.

Akizungumza na Mwananchi jana usiku,  Catherine Kulekana ambaye ni mke wa Awadh amesema, "hali yake ilianza kubadilika usiku wa kuamkia leo (Jana)  akawa chini ya uangalizi wa madaktari."
"Ilipofika asubuhi hali yake haikurejea  kawaida na saa 10 jioni alifariki,” amesema Catherine.

SOMA ZAIDI: Anayepumulia mashine alazwa tena Mloganzila
Mmoja wa ndugu wa Awadh  ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake amesema taarifa kuhusu msiba wa ndugu yao watazitoa leo Ijumaa.
Juni 10, 2019 Mloganzila ilimpa msaada wa mashine hiyo ya kumsaidia kupumua yenye thamani ya Sh4 milioni  kutokana na matatizo yake ya afya ambayo yalimlazimu kutumia mashine ya Oksjeni muda wote ili aweze kupumua.
Awadh alifikishwa Mloganzila  Julai 9, 2018 na kuruhusiwa Juni  9, 2019 baada ya afya yake kuimarika.
Licha ya kutakiwa kurejea hospitali kila baada ya muda alishindwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokuwa na usafiri wa kutoka nyumbani kwake Kipawa hadi katika hospitali hiyo umbali wa zaidi ya kilomita 10.

Wadau na taasisi mbalimbali walijitokeza kumsaidia ikiwa ni pamoja na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) lililomfungia umeme katika nyumba aliyokuwa akiishi na kumpatia Sh10 milioni za matibabu. Awadh aliomba msaada Tanesco kutokana na mashine ya kumsaidia kupumua kutumia umeme mwingi.
Septemba 11, 2019 Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)  lilisema lipo tayari kumlipia gharama za usafiri hadi Mumbai, India ikiwa atapangiwa na madaktari kutibiwa katika mji huo.

Pia, hospitali ya Mloganzila ilitoa gari la wagonjwa kwa ajili ya kumpeleka Awadh katika hospitali hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake, mara ya mwisho hali yake ilibadilika na kulazwa hadi umauti ulipomkuta.