Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Ajira ya Mariam yaleta kicheko kwa watumishi, wanaojifungua

Mariam Mwakabungu akiwa katika majukumu yake kwenye Hospitali ya Rufaa ya Amana.

Dar es Salaam. Mwanamke aliyejitolea kukumbatia watoto njiti, Mariam Mwakabungu (25) amegeuka faraja kwa wanawake wanaojifungua kabla ya wakati, wauguzi na madaktari katika wodi ya watoto hao iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Amana.

Siku chache baada ya kupewa ajira na Serikali, Mariam ameongezewa majukumu, ikiwemo kutunza watoto ambao mama zao wanaumwa, waliofanyiwa upasuaji kwa kuwapa huduma za kuwaogesha, kuwavisha na kuwapa maziwa.

Mafanikio haya yamekuja siku 37 tangu gazeti hili liripoti habari kuhusu Mariam, ambaye alianza kwa kujitolea kukumbatia watoto njiti wanaotupwa na kutelekezwa hospitalini hapo.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu juzi, Ofisa muuguzi mwandamizi na kiongozi wa wodi ya watoto wachanga Hospitali ya Rufaa ya Amana, Mary Machemba aliishukuru Serikali kwa kumwajiri kwa sababu wameongeza ufanisi na kurahisisha kazi kwa wataalamu ndani ya wodi hiyo.

“Mwezi mmoja na nusu tangu ameajiriwa ameongeza nguvu kubwa sana. Kuna hawa watoto ambao wanazaliwa mama zao wanapelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi au bado hawajapata nafuu anawahudumia yeye.

“Wengine bahati mbaya wanafariki, waliokotwa au mama zao wapo ICU hawana uwezo wa kuwahudumia yeye anachukua hiyo nafasi na anajituma kweli kweli, kwa sasa hapa tunao watano, akifika asubuhi anaanza nao, kiukweli tuna furaha sana,” alisema.

Machemba alisema kama wanaumwa au wana tatizo lolote anabaini mapema na kuwashirikisha: “Anasimama kwenye nafasi ya umama, anawaogesha, anawavisha pampers, anawapa huduma ya maziwa na kwa usahihi kila baada ya saa tatu, maana humu wauguzi wanakuwa bize sana,” alisema.

Alisema Mariam amekuwa akisaidia kazi nyingine, zikiwemo kusafisha vyombo, kupanga mafaili, kuwazungukia kinamama wanaponyonyesha na kutoa taarifa akibaini mwenye changamoto.

“Ana juhudi na malengo ya kufika mbali, anasema anahitaji kufanya mitihani ya QT ili ajiendeleze kielimu. Ameshasajiliwa na watu wa British Schools ambao wamempa ufadhili kwenye utaratibu wa kuanza masomo ili apate cheti cha kidato cha nne ili aende akasome uuguzi,” alisema.

Ajira ya Mariam yaleta kicheko kwa watumishi, wanaojifungua

Machemba alitoa wito kwa Serikali kuweka angalau msaidizi mmoja kama Mariam mwenye wito katika wodi za watoto wachanga, kwani anasaidia wakue haraka na kupunguza changamoto zilizopo kwa maana wauguzi ni wachache.

Mariam alisema kuna tofauti kubwa sana ya kabla alipokuwa akijitolea na sasa, kwani imempa heshima na hata kutambulika anafanya kazi licha ya kwamba analipwa mshahara.

“Nilikuwa nipo tu kwa ajili ya kuwabeba kifuani saa 24, kwa sasa ninakuja asubuhi saa 1:30 ninapitishwa kwa watoto wote ambao mama zao hawapo au bado wapo ICU ninawahudumia siku nzima ninawabadili nepi, ninawaogesha na kuwalisha kisha ninawarudisha kwenye joto,” alisema.

Akitaja majukumu yake, alisema akifika lazima ahakikishe sehemu atakayowahudumia watoto iko safi. “Ninabadilisha mashuka ya watoto na vitu vingine ambavyo ninatakiwa kuvifanya nafundishwa kila siku, nilikuwa sijui kufanya vitu vingi sana, lakini kwa sasa naelekezwa, baadhi ya vitu ninavifanya ninafurahi sana, maana ninajifunza vitu vingi ambavyo nilikuwa sivijui.”

Licha ya hivyo, Mariam alisema yupo mbioni kuanza masomo baada ya kupata ufadhili kutoka British Schools.

“Wamejitolea kunisomesha na kwa sasa nilikuwa nasubiri mambo fulani ya kifamilia yakae sawa ili nianze kusoma masomo ya jioni,” alisema.

Mratibu Mkuu wa Shule ya British Schools, Frank Mahamila alithibitisha kutoa ufadhili huo. “Tumempa nafasi ya kusoma kozi ya Kiingereza ili mwakani sasa aanze kusoma sekondari ya miaka miwili aweze kumaliza kidato cha nne.”


Familia

Akizungumzia familia yake kwa sasa, Mariam alisema iko vizuri na kwamba anashirikiana na mumewe vizuri katika kazi yake mpya na kwa sasa ameshapata msaidizi ambaye ni ndugu yake ili kumsaidia watoto.