Prime
Uvamizi miundombinu ya mwendokasi mfupa mgumu

Muktasari:
- Wafanyabiashara waeleza sababu za kuvamia maeneo ya mwendokasi, huku mamlaka zikitaja hatua za kuchukua.
Dar es Salaam. Licha ya kuzuiwa kufanya biashara ndani ya miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (Udart), wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga wameendelea kuvamia vituo na njia za mabasi hayo, wakifanya shughuli zao kama hakuna agizo lililowahi kutolewa.
Katika vituo vilivyopo Barabara za Morogoro, Mbagala na Gongo la Mboto, hali hiyo imekuwa ya kawaida, baadhi ya wafanyabiashara wakiuza bidhaa zikiwamo matunda, karanga, vinywaji baridi na nyingine ndogondogo za nyumbani.
Hatua hiyo si tu inahatarisha usalama wa wanunuzi na wachuuzi wa bidhaa hizo, bali pia ina athari kwa miundombinu.
Miongoni mwa sababu za uvamizi huo zinatajwa kuwa ni kuchelewa kuanza kutumika kwa miundombinu hiyo kwa ajili ya usafirishaji, uchache wa mabasi na kukosekana maeneo rafiki kwa ajili ya machinga kufanyia shughuli zao.
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), chini ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), unatekelezwa katika awamu sita; barabara zilizokamilika ni Morogoro na Mbagala.

Barabara ya Morogoro ni mradi uliotekelezwa katika awamu ya kwanza, inatumika kuanzia mwaka 2016, mabasi yakifanya safari kati ya Mbezi-Kimara hadi Kivukoni, Mbezi-Kimara hadi Gerezani na Kimara hadi Morocco.
Barabara ya Mbagala, kwa mujibu wa mamlaka husika, ujenzi wa miundombinu umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, wiki iliyopita akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26, alisema Serikali inatarajiwa kukamilisha ununuzi wa mtoa huduma kwa njia ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.
Kutokana na uvamizi wa miundombinu hiyo katika maeneo kadhaa yakiwamo ya Mbagala Rangi Tatu, Kariakoo, Mchikichini, Mbezi Luis na Kimara, mara kadhaa mgambo wamekuwa wakiweka kambi kuwadhibiti wafanyabiashara hao.
Katika baadhi ya maeneo, mama lishe wanaendelea na biashara ya chakula huku wakipika, kwa maelezo kuwa baada ya kuondoka kwenye maeneo yao ili kupisha ujenzi, hawana mahali mbadala pa kukaa.
Machinga watoa kauli
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi wamesema matatizo ya kiuchumi yanawasukuma kufanya biashara katika maeneo hayo.
Pia wamesema hawana maeneo rasmi ya kufanyia biashara, na yaliyopo si rafiki; ndiyo sababu hutumia vituo vya mabasi au barabara za mwendokasi kwani ni maeneo yenye watu wengi.
Ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha vinatajwa kwamba huwasukuma kufanya biashara maeneo hayo ili kujipatia kipato kwa haraka.
Mchuuzi wa matunda Gongo la Mboto, Godfrey Okechi, amesema kwa miaka sita amekuwa eneo hilo, lakini baada ya kuanza ujenzi wa barabara ya mwendokasi hana pa kufanyia biashara, hivyo analazimika kuuza matunda kwenye miundombinu ya barabara.

“Serikali iangalie namna ya kututafutia sehemu rasmi ya kufanyia biashara. Kwa sasa kila wakati tunafukuzwa, hivyo kushindwa kuwa na amani,” amesema.
Mkazi wa Mbagala Rangi Tatu, Hussein Maalim, amesema si kwamba wafanyabiashara wanapenda kukimbizana na mgambo kila mara, lakini ni katika kujitafutia riziki.
Amesema machinga hufuata wateja walipo, hivyo Serikali iangalie namna ya kuwasaidia kwani kuwaondoa inaonekana ni kazi ngumu.
Zai Kibwana, amesema kupata nafasi katika masoko yaliyojengwa imekuwa ngumu, hivyo wanaona bora kupanga bidhaa barabarani ili kupata riziki, kwani wana majukumu ya kulea familia.
Watumiaji barabara
Kwa upande wao, watumiaji wa barabara wanaona kwamba mamlaka husika haziwajibiki vya kutosha katika kuchukua hatua kuwadhibiti machinga.
Wanaona kwamba kuna udhaifu wa usimamizi wa miundombinu hiyo, hivyo kuvamiwa kirahisi.
Pia yamekuwapo malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kwamba hawashirikishwi uamuzi unapotolewa, ikiwamo kupangiwa maeneo ya biashara, hali inayosababisha warejee kule wanakofukuzwa.
Julian Maro, mkazi wa jijini Dar es Salaam, amesema kinachoendelea ni kero kwa watumiaji wengine wa barabara.
“Wafanyabiashara naona Serikali imewashinda. Kama imeamua kuwatoa maeneo yasiyo rasmi, hata huku kwenye njia za waenda kwa miguu hawapaswi kuwapo. Mgambo wanaposhughulika kuwaondoa, wahakikishe hadi huku hawakai,” amesema.
Stanley Michael, mkazi wa Kigamboni, amesema kuna hatari ya Serikali kuingia gharama ya kufanya ukarabati kabla ya miundombinu hiyo kutumika, iwapo machinga wataendelea kufanya biashara kwenye miundombinu ya Mbagala.
“Tumeona barabara ya Mbagala Serikali imepiga marufuku magari kupita kwenye miundombinu ya mabasi haya. Huku Mchikichini wanawaacha hawa wenye majiko wanaingia hadi vituoni. Tunaelekea wapi na miradi hii? Au hata hawa wanaotupa hela wakija kuona hali wataondoka na tafsiri gani kama si kuona mamlaka zimeshindwa kusimamia watu wake?” amehoji.
Ziada Athuman, mkazi wa Mbagala Charambe, yeye amesema: “Ukitaka kuja Mbagala Rangi Tatu unajifikiria, hata kama unafuata mahitaji muhimu. Ni lazima upigane vikumbo na watu wanaofanya biashara.”
Mtazamo wa mamlaka
Msemaji wa Dart, William Gatambi, amesema kazi ya kuwaondoa wamachinga wameziachia halmashauri.
Ofisa Mazingira wa Wilaya ya Ubungo, Lawi Mgongo, amesema eneo la Mbezi walinzi wapo muda wote, ili kudhibiti wanaofanya biashara katika miundombinu.
Amesema eneo la Kimara Darajani wafanyabiashara wanakuwapo jioni na hawasababishi mabasi kushindwa kupita.
Diwani wa Gongo la Mboto, Lucas Rutainurwa, amesema shida iliyopo ni kutokuwapo soko, licha ya kuwa ni kituo kikubwa kinachopokea daladala zinazotoka pembezoni, hivyo machinga kufanya biashara kwenye miundombinu ya barabara.
Amesema wamekuwa wakifanya vikao na wafanyabiashara kuwaelimisha kuhusu athari za kufanya biashara katika miundombinu hiyo.
Ameeleza hivi karibuni waliwapanga kwenye maeneo ili kupisha ujenzi wa miundombinu unaoendelea, lakini pia kujiandaa pindi magari yatakapoanza kupita.
Mikakati iliyopo, amesema ni kuwa na soko na mchakato unaendelea kupitia halmashauri.
“Tayari tumepata eneo la kujenga soko katika Mtaa wa Gongo la Mboto. Tunatarajia nyumba zaidi ya 21 zitafidiwa ili kutwaa eneo. Mchakato utachukua muda kwani mpaka tathmini ifanyike,” amesema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke, Jomary Satura, amesema wamekuwa na operesheni za kuwaondoa wafanyabiashara kwenye miundombinu ya mwendokasi, kazi anayosema imegubikwa na changamoto kadhaa.
“Wapo wanaoona ukiwafukuza wafanyabiashara hao unawaharibia kura zao, bila kuangalia athari kwa upande wa jamii,” amesema.
Changamoto nyingine, amesema, ni wananchi kushindwa kutii sheria bila shuruti, akisema hawapendi kukimbizana na wafanyabiashara hao mara kwa mara.

“Kukimbizana na wafanyabiashara barabarani si kusudio letu, na wala hatupendi, isipokuwa ili eneo hilo litumiwe na watu wengine na kufanyika kwa shughuli za kijamii ipasavyo, inabidi tufanye hivyo,” amesema.
Ametoa mfano akisema Barabara ya Kilwa haitumiwi na wakazi wa Mbagala pekee bali na ukanda mkubwa wa Kusini, yakiwamo maeneo ya Mkuranga, Rufiji, Kilwa, Lindi na Mtwara.
“Haiwezekani eti kwa sababu ya foleni, mgonjwa anatoka huko alipotoka lakini anakuja kufia Mbagala, kisa tu watu waliopanga biashara kinyume cha sheria na kusababisha foleni. Hilo hatutalikubali. Tunataka matumizi ya barabara hiyo yafuatwe kama malengo ya kuijengwa yalivyokuwa,” amesema.
Amesema Serikali pia huingia gharama za kuwalipa mgambo ili kuwaondoa wafanyabiashara hao, fedha ambazo zingepelekwa kwenye shughuli nyingine kama vile utengenezaji wa madawati au kununua dawa.
Amesema wanaohitaji maeneo sokoni wasisite kufika ofisi za kanda ili wapatiwe badala ya kupanga bidhaa barabarani.