Prime
Uteuzi wa Munisi waibua mjadala
Muktasari:
- Baadhi wanautafsiri uteuzi huo kama utekelezaji wa falsafa yake ya 4R na turufu ya kuimarisha mshikamano wa kisiasa nchini
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Evaline Munisi kuwa Naibu Waziri-Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), wadau wa siasa wameibua mitazamo kinzani kuhusu uamuzi huo.
Baadhi wanautafsiri uteuzi huo kama utekelezaji wa falsafa yake ya 4R na turufu ya kuimarisha mshikamano wa kisiasa nchini.
4R hizo ni maridhiano (Reconciliation), mabadiliko(Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya(Rebuilding)
Wengine wanadai ni mbinu ya kujaribu kuihadaa dunia kwa kuonesha dhamira ya maridhiano, huku wakisisitiza haina tija.
Munisi, ambaye awali aliteuliwa kuwa mbunge, ameweka historia mpya tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 kwa kushika wadhifa wa Naibu Waziri.
Hapo awali, viongozi wa upinzani waliteuliwa zaidi katika nafasi za ubunge au ukuu wa mikoa.
Munisi aliteuliwa jana Jumamosi, Aprili 2, 2026 kushika wadhifa huo, akichukua nafasi ya Rahma Riyadh Kisuo, ambaye uteuzi wake umetenguliwa baada ya kuhudumu kwa takribani miezi sita.
Kumekuwa na maswali yanayoulizwa je, mteuliwa kwa maana ya Munisi ambaye katika uchaguzi mkuu mwaka 2025 alikuwa mgombea mwenza wa urais wa NCCR-Mageuzi atahamia CCM, atabaki ndani ya chama chake au itakuwaje?
Leo Jumapili, Mei 3, 2026, Mwananchi imezungumza na wadau mbalimbali akiwamo Munisi, chama chake na kupata mitizamo tofauti juu ya uteuzi huo unaoelezwa ni wa kwanza mpinzani kuteuliwa moja kwa moja kuwa Naibu Waziri.
Hata hivyo, Rais Samia amefanya uteuzi huo akiegemea Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inampa mamlaka hayo.
Ibara ya 36(1) inasema bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba na sheria nyingine, Rais ana mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Tanzania.
Ibara ndogo ya (2) inampa Rais mamlaka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali pamoja na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi.
Katika Ibara hizo, hakuna mahali popote panapompa Rais masharti kwamba asiteua mtu ambaye sio mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na ndio maana hata waliomtangulia waliwahi kuteua watu kutoka upinzani.
Munisi si wa kwanza kuteuliwa na Rais kutoka upinzani, Mei 3, 2012, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alimteua aliyekuwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kuwa mbunge.
Julai 16, 2016 Rais wa awamu ya tano, John Magufuli alimteua Mwenyekiti wa TLP kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole kwa kipindi cha miaka mitatu na 2020 akamteua tena kwenye nafasi hiyo.
Juni 3, 2017, Rais Magufuli ambaye baadaye alifariki dunia, alimteua Anna Mghwira kutoka Chama cha ACT Wazalendo, kuwa Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, baadaye Mghwira (marehemu) alijiunga na CCM.
Mei 15, 2021, Rais Samia akamteua Queen Sendiga, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa ADC na mgombea urais kwa tiketi ya ADC kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na baadaye akamhamishia Manyara.
Kauli ya NCCR-Mageuzi
Akizungumza na Mwananchi, Munisi amesema ameupokea uteuzi huo na bado ni mwanachama halali wa NCCR-Mageuzi, ingawa atazungumza kwa kina baada ya kuapishwa.
“Bado ni mwanachama wa NCCR-Mageuzi, na uteuzi nimeupokea. Nitazungumza zaidi baada ya kuapishwa,” amesema Munisi ambaye ni Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi.
Ndani ya NCCR-Mageuzi, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Joseph Selasini, amesema uteuzi huo hauna dhamira njema, akikitenga chama na nafasi mpya ya Munisi.
“Munisi ni Katibu Mkuu wetu. Ameteuliwa kuingia kwenye Baraza la Mawaziri na atalazimika kusimamia sera za chama kingine, ambacho hatulingani kiitikadi; hivyo hawakilishi upinzani,” amesema.
Amesema uteuzi huo hauna maana yoyote kuelekea maridhiano, na kwamba unaweza kuleta mgawanyiko zaidi ndani ya upinzani.
“Kwa upande wetu, huyo si mwanachama wetu kwa vitendo tena. Mwanachama lazima asimame na itikadi na sera za chama chake. Huwezi kutekeleza ilani ya chama kingine na bado ukadai uko kwenye chama chako cha awali,” amesema.
Mtazamo wa wasomi
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa George Kahangwa amesema tukio lililotokea ni halali Kikatiba, ingawa limeibua maswali mengi kwa kuwa ni mara ya kwanza kutokea.
"Mtazamo wa pili, ni vigumu kwa vyama viwili kuunda Serikali bila ya kuwepo makubaliano ya awali," amesema huku akihoji kama vyama hivyo vimewahi kufanya makubaliano kama hayo na kama hakuna, basi huu ni wakati muafaka kwa NCCR-Mageuzi kujitathmini upya.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Salbinus David amesema uteuzi huo ni ishara ya nia njema kutoka kwa Serikali.
“Inadhihirisha kiwango fulani cha uwazi na utayari wa kushirikiana zaidi ya mipaka ya vyama vya siasa. Hiyo ni hatua muhimu, hasa katika kipindi ambacho nchi inaelekea katika maridhiano,” amesema.
‘Taifa Kwanza’
Mwenyekiti wa Muungano wa vyama 13 vya upinzani na Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema anauona uteuzi huo kama ishara ya nia njema ya Rais ya kuongoza nchi bila kujali itikadi.
Amesema hatua hiyo inaonesha utayari wa kuvuka mipaka ya vyama kwa kuzingatia masilahi ya Taifa na kwamba inatuma ujumbe kuwa yuko tayari kushirikiana na watu wenye uwezo bila kujali itikadi zao za kisiasa.
“Tusichukulie siasa kama timu za mpira zisizoweza kushirikiana. Kama mtu ana sifa na anaweza kulitumikia Taifa, anapaswa kupewa nafasi,” amesema.
Katika maelezo yake, Mluya ameusifu uteuzi huo akisema ni hatua ya vitendo kuelekea maridhiano, huku akiwahimiza walioteuliwa kuthibitisha uwezo wao na kuhalalisha imani waliyopewa.
Hata hivyo, amekataa madai ya baadhi ya wadau kuwa kupandishwa kwa Munisi kunatokana na mbinu za kisiasa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Yusuf Mirambo amesema uteuzi huo unaweza kuwa hatua chanya kuelekea ushirikishwaji mpana na umoja wa kitaifa.
“Hii ni mara ya kwanza kushuhudia uteuzi wa aina hii katika ngazi hii. Inaashiria kuwa Serikali inaweza kuwa tayari kukumbatia mfumo shirikishi zaidi wa uongozi bila kujali itikadi,” amesema.
Mirambo pia ameutafsiri uteuzi huo kama ishara ya utayari wa Serikali kufanya kazi na watu kutoka pande tofauti za kisiasa, kwa kuzingatia zaidi uwezo kuliko itikadi za vyama.
Ilichokisema Chadema
Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema anaona uteuzi huo kama sehemu ya mkakati mpana wa upotoshaji wa kisiasa badala ya maridhiano ya dhati.
Mnyika amesema hatua hiyo inalenga kuunda taswira ya ushirikishwaji kwa umma wa ndani na wa kimataifa, hasa kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 uliogubikwa na utata.
Amesema uteuzi huo hauoneshi dhamira ya kweli ya mazungumzo au mageuzi, bali ni jaribio la kuhamisha mjadala kutoka kwenye migogoro ya kisiasa ambayo bado haijatatuliwa.
“Hii ni mbinu inayolenga kuionesha dunia kuna maridhiano yanaendelea, jambo ambalo si kweli na linaweza kuchochea hasira kwa wananchi,” amesema.
Mnyika amesema hatua hiyo inaendeleza wasiwasi wa muda mrefu kuhusu uadilifu wa mchakato wa kisiasa, akidai kuwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani wanaweza kuwa wanatumika kimkakati kutimiza malengo fulani ya kisiasa.
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, ACT-Wazalendo Shangwe Ayo, amesema chama hicho kinachukua muda kutafakari hali ya siasa nchini.
“Hatuwezi kutoa maoni kwa sasa. Tunatafakari hali ya siasa nchini na matukio ya Oktoba 29. Ukweli, haki na uwajibikaji ndizo mambo pekee yatakayoponya Taifa letu,” amesema.