Utaratibu mpya kodi ya majengo

Muktasari:
Wakati mjadala wa makali ya tozo ya miamala ya simu yakisubiri uamuzi wa Serikali, maumivu mapya yanaanza leo baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutangaza itakavyotekeleza utaratibu mpya wa kukusanya kodi ya majengo kupitia ununuzi wa umeme.
Dar/mikoani. Wakati mjadala wa makali ya tozo ya miamala ya simu yakisubiri uamuzi wa Serikali, maumivu mapya yanaanza leo baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutangaza itakavyotekeleza utaratibu mpya wa kukusanya kodi ya majengo kupitia ununuzi wa umeme.
Wakati utaratibu huo ukitangazwa, Serikali imejibu baadhi ya maswali tata ambayo yamekuwa yakiulizwa kuhusu kodi hiyo, ambayo awali ilikuwa inakusanywa na Serikali za Mitaa na baadaye kuhamishiwa TRA.
Tamko la TRA
Taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata imesema kila jengo la kawaida lililopo ndani ya kiwanja litalipiwa Sh12,000 badala ya Sh10,000 ya awali na Sh60,000 kwa kila sakafu ya ghorofa kutoka Sh50,000 ya mwanzo. Kwa halmashauri za wilaya na miji midogo, nyumba za ghorofa zitatozwa Sh60,000.
“Kwa utaratibu huu mpya, kila mnunuzi wa umeme atakatwa Sh1,000 kwa mwezi kwa nyumba ya kawaida na Sh5,000 kwa kila sakafu ya ghorofa. Kwa wale wanaotumia mita za ankara watalipa kodi hii kwa pamoja katika ankara ya mwezi,” alisema.
Kwa wamiliki ambao majengo yao hayana umeme, kamishna mkuu alisema wataendelea kulipa kodi hiyo kwa mfumo uliokuwapo awali, ambao ni kwa simu za mkononi au benki baada ya kupata namba ya kulipia (control number) mpaka watakapoingiziwa umeme.
Wamiliki wa majengo na wananchi watakaokatwa kodi hiyo kimakosa, Kidata amesema watatakiwa kwenda ofisi za TRA zilizo karibu na maeneo yao kushughulikia suala hilo. Utaratibu huu pia unamhusu yeyote atakayekuwa na malalamiko juu ya utaratibu uliowekwa.
Vick Shirima, mkazi wa mjini Moshi alisema ameshtushwa na tangazo la TRA kwa sababu aliposikiliza Bunge la Bajeti ulikuwa mjadala wa utaratibu bora wa kukusanya kodi hiyo si kupandisha kiwango kinachotozwa, sasa hili ongezeko la kutoka Sh10,000 hadi Sh12,000 hakulitarajia.
“Najiuliza kama nyumba ina mita mbili au tatu na ni ya wapangaji nani atawajibika kulipa hiyo kodi na mtu akiomba umsaidie kumnunulia umeme huoni nitamlipia kodi?” alihoji Vicky.
Diwani wa Kata ya Katangara Mrere wilayani Rombo (CCM), Venance Maleli alisema wazo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka kuongeza idadi ya walipa kodi halikuwa na maana ya kulilundikia kundi moja kodi ambazo baadhi si rafiki.
“Kulipa kodi ni uzalendo lakini zinatakiwa ziwe rafiki, mfumo uwe mzuri usiowaumiza wananchi. Wizara ya Fedha itafsiri vizuri kauli ya Rais ya kutengeneza walipa kodi wengi,” alisema Maleli.
Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo alisema kodi ya majengo ni jambo jipya na lenye changamoto, hasa kwa wale wanaoishi nyumba za kupanga ambayo kiuhalisia wanaotakiwa kuilipa ni wamiliki wa majengo.
Serikali, wadau wafafanua
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso alisema walipitisha sheria ili kurahisisha ukusanyaji lakini si kuongeza kiwango.
Kakoso alisema kiwango kinachotakiwa kulipwa ni kilichokuwa kinalipwa awali bila kuongeza, ila anaamini hata waliokuwa hawalipi, sasa watalipa.
“Kama wameongeza hilo si jukumu letu, sisi tunapitisha sheria lakini kanuni huwa zinaandikwa na waziri na hapo ndipo kelele huanzia,” alisema Kakoso.
Mbunge wa Viti Maalumu, Felister Njau alisema mpango wa kulipa kodi kupitia luku ulitokana na mawazo ya wabunge wote, lakini si viwango vya kuwaumiza wananchi.
“Kama utawaumiza wananchi lazima wataipigia kelele sheria hiyo ili irejeshwe tena bungeni,” alisema Felister.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Daniel Baran alisema ongezeko la kodi linatokana na mabadiliko ya utaratibu.
“Kiwango kimeongezeka ni kweli, lakini hilo la mita zaidi ya moja haziwezi kulipwa zote ndugu yangu, tunasajili moja,” alisema Baran.
Kuhusu majengo ya umma, ikiwemo hospitali na shule alisema hayakuingizwa katika mfumo huo unaoanza leo.
Kutokana na malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusu ongezeko la kodi ya majengo, Serikali imefafanua jinsi nyumba zenye luku zaidi ya moja au zenye wapangaji zitakavyolipa.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema kikichobadilika ni mfumo wa ulipaji, badala ya kukusanya nyumba kwa nyumba kama zamani sasa inakusanywa kielektroniki tena kwa awamu.
“Kama nyumba wanaishi wapangaji, wanaweza kuwa na maelewano ama mmiliki awe anatoa hiyo Sh1,000 kwa ajili ya makato ya kodi au wazungumze vinginevyo. Kuna nyumba zina mita nyingi au mita moja inatumiwa na watu wengi, kutakuwa na utaratibu wa kutembelea nyumba kwa nyumba kuangalia kama mpango unaenda vizuri,” alisema Tutuba.
(Imeandikwa na Daniel Mjema, Habel Chidawali na Aurea Simtowe.