Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti mabadiliko tabianchi kuboresha maisha ya wananchi

Wadau mbalimbali wa Mazingira wakiwa kwenye uzinduzi wa Mradi wa Utafiti wa Mabadiliko ya Tabianchi unaofanywa na Chuo Kikuu cha Ardhi katika Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Mradi wa utafiti wa mabadiliko ya tabianchi yanayotarajiwa kufanywa wilaya Kigamboni Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Ardhi unatarajia kuboresha mipango ya maendeleo, uboreshaji wa kilimo na usimamizi wa maliasili.

Dar es Salaam. Kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazoathiri dunia nzima, Chuo Kikuu cha Ardhi kinatarajia kufanya utafiti ili kutoa mwongozo kwa Serikali wa kukabiliana na changamoto hizo na kuboresha maisha ya wananchi.

Utafiti huo unafanywa kupitia Mradi wa Kukuza Maarifa kwa manufaa ya muda mrefu na ustahimilivu wa tabianchi kupitia huduma za tabianchi na suluhisho za msingi wa asili (ALBATROSS) na unalenga kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga ya asili.

Hayo yamesemwa jana Agosti 28, 2024 na mratibu wa mradi huo, Profesa Wilbard Kombe akisema utalenga maeneo yanayokabiliwa na changamoto za mazingira kama vile kupungua kwa mvua, kuongezeka kwa joto, na kuenea kwa mafuriko na dhoruba.

Mbali na Tanzania, amesema mradi huo pia utatekelezwa katika nchi nne za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Tanzania, Madagascar, Afrika Kusini, Ghana, na Kenya.

Amesema kwa Tanzania utafiti huo utafanyika katika Wilaya ya Kigamboni Dar es Salaam na utatoa takwimu sahihi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi katika wilaya hiyo kama vile ongezeko la joto, mabadiliko ya mvua, na kuongezeka kwa kina cha bahari.

"Mradi huu tutakuwa nao kwa miaka mitatu utasaidia kukabiliana na changamoto za majanga, utahusisha wakazi wa Kigamboni katika shughuli za hifadhi ya mazingira, ikiwemo urejeshaji wa mikoko, uhifadhi wa bayoanuwai ya majini na ufugaji wa nyuki," amesema Profesa Kombe.

Mkurugenzi Msaidizi wa Sekta za Uchumi na Uzalishaji, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Enock Nyanda amesema utafiti huo utasaidia  Serikali kupanga vizuri mipango ya maendeleo kama vile ujenzi wa miundombinu ya kudumu, uboreshaji wa kilimo, na usimamizi wa maliasili.

"Utafiti unaofanyika umechagua Kigamboni kwa sababu kuna eneo kubwa ambalo halijaendelezwa na sasa wananchi ndio wanakwenda kuutanua mji hii itatusaidia katika upangaji miji na namna ya kuendeleza bila kupata athari za baadae," amesema Nyanda.

Pia amesema inaweza kuwa chachu ya kuvutia wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama vile nishati safi na miundombinu ya kijani, kwa sababu Kigamboni ina nafasi nzuri ikiwamo ukaribu wake na bahari pamoja na miundombinu inayokua.

Naibu Meya Halmashauri ya Kigamboni, Stephano Warioba amesema changamoto iliyopo ni ukataji wa mikoko wakati wa usiku na siku za karibuni walikamata magunia zaidi ya 200 yakiwa tayari kusafirishwa kupelekwa Zanzibar huku wengine wakivunja wakiweka vifusi ili kujipatia maeneo ya kuishi pembezoni au jirani mwa bahari.

"Kupitia utafiti utakaofanywa utasaidia namna ya kulinda mazingira yetu pia utatoa taswira ya mji unavyokua ambao hautaweza kuleta athari kwa wananchi," amesema Warioba.