Wakazi Kigamboni wahaha kuokoa maeneo yanayovamiwa, Serikali yawajibu

Muktasari:
- Wakazi wa Mtaa wa Kichangani, Kata ya Kibada, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam wanaoishi katika maeneo ya vitalu namba moja hadi sita wamehoji ukimya wa Serikali kwa watu wanaovamia maeneo ya hifadhi katika mradi wa viwanja 20,000 Kigamboni.
Dar es Salaam. Wakazi wa mtaa wa Kichangani (Valley Zone), Kata ya Kibada Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam wameiomba Serikali kuingilia kati sakata la kuvamiwa maeneo ya wazi yaliyotengwa.
Wamesema uvamizi huo katika maeneo ya wazi, bonde na yaliyotengwa kwaajili ya nyumba za ibada pamoja na kupumzika, unafanywa na watu wanaopata vibali vya ujenzi kutoka Manispaa.
Wakazi hao wameiambia Mwananchi kuwa walianza kulalamika serikalini tangu mwaka 2021 ikiwemo kwa Mkurugenzi wa Manispaa, Mkuu wa Wilaya lakini wanadai hakuna kilichofanyika mpaka sasa.
Wamesema wamekuwa wakilalamikia uvamizi wa viwanja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na Kamishna wa ardhi tangu mwaka 2021 kuhusu uvamizi huo wa maeneo ya mabonde ya maji ya mvua lakini hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa kuwadhibiti wavamizi hao.
Waeleza historia ya eneo hilo
Sosthenes Sambua amesema mwaka 2003 eneo hilo lilipimwa na kuanza kumilikishwa ilipofika mwaka 2006 huku mamlaka ikitenga maeneo ya wazi, taasisi za dini, viwanja vya michezo na eneo la bonde kupitisha maji na kwaajili ya hewa, shule na kituo cha Polisi.
"Ilivyofika mwaka 2021 tukashangaa watu kuanza kupima maeneo hayo ya wazi yaliyotengwa kwaajili ya kuanza ujenzi. Tukaanza kupeleka malalamiko Ofisi ya Serikali ya mtaa, kwa Mkurugenzi ili kuzuia jambo hilo lakini baada ya miezi sita hakuna lililofanyika.
"Tukachukua hatua kwenda kwa Mkuu wa Wilaya wa wakati huo akaahidi atashughulikia lakini hadi mwaka 2022 hakukuwa na lolote lililofanyika. Tukaenda kwa Kamishna wa Ardhi kwa maandishi akajibu atashughulikia lakini hadi mwaka 2023 hakukuwa na lolote," ameeleza
Amesema alipokuja mkuu wa wilaya wa sasa akatembela eneo hilo wakamueleza akajibu watashughulikia. Mwisho ikaundwa kamati maalumu kwa maagizo ya mkuu wa mkoa ili kutafuta ufumbuzi wa maeneo ya wazi lakini hadi leo mwaka 2024 hakuna kilichofanyika.
"Tunapiga kelele mwaka wa nne huu na hatusaidiwi tumeshazunguka ofisi mbalimbali tunataka sauti yetu ifike kwa waziri mwenye dhamana. Pia mazingira yanaharibiwa kwani eneo la bonde liko hapa mfano juzi Agosti 18, 2024 mtu mmoja alikuja akazungushia eneo la bonde, akaanza ujenzi akiwa na vibali vya kujenga kutoka Manispaa.”
Daniel Koloseni ambaye ni Mwenyekiti wa wakazi wa eneo hilo amesema wanaiomba Serikali iingilie kati kwa usalama wao wa kimazingira kwani kukikosekana eneo la kupitishia maji mvua zikianza itakuwa hatari kwao.
Amesema waliamua kuweka mabango takribani 20 yenye ujumbe wa kuwapa taarifa wanunuzi kwamba maeneo hayo yamehifadhiwa lakini cha kushangaza watu wanapata vibali kutoka kwa baadhi ya watumishi serikalini wasio waaminifu.
Kwa upande wake, DK Jerome Kessy amefafanua kwamba eneo lolote la makazi ya watu lazima liwe na mpango wa eneo la wazi kwaajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo michezo na matukio ya kijamii.
Amesema ni jambo la kushangaza baadhi ya watu kutaka kujenga katika maeneo hayo. Dk Kessy ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira wa Valley Zone amesema maeneo ya wazi yakichukuliwa hata mpango wa Serikali kuotesha miti hautafanikiwa.
"Tunataka maeneo ya wazi yatumike kama ilivyotakiwa na mabonde yatumike kuotesha miti. Tunaomba Serikali iweze kushirikiana na sisi kutunza mazingira kwaajili ya kizazi chetu na kijacho," amesema.
Naye, Jane Malinga ameomba na kusisitiza mamlaka husika kusimamia suala hilo kwani maeneo ya wazi yanasaidia watoto kucheza na kutenga eneo la kujengea soko.
Serikali yawajibu
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Erasto Kiwale amesema shida iliyopo ni mchakato mzima wa utoaji vibali vya ujenzi.
"Kwanza niombe radhi kwa wananchi kwa usumbufu huo ambao huwa unaojitokeza. Kwenye suala la utolewaji vibali kuna namna vinatolewa kwa haraka bila ya kujiridhisha.
Wakati mwingine kuna suala la uharakishaji na watoaji vibali vya ujenzi wanatoa haraka ili kuwahisha huduma. Maamuzi yanaweza kufanyika wakati mwingine kabla ya kufika eneo la uje nzi."
Lakini niwahakikishie tutaendelea kusimamia sheria kanuni na taratibu ili kumaliza changamoto hiyo. Lakini pia siyo sahihi kusema hakuna hatua zilizokwishachukuliwa. Huwa tunachukua hatua za kusitisha vibali baada ya kupata taarifa."
Jukumu la kulinda maeneo ni la kwetu sote lazima tushiriki hivyo waendelee kutushirikisha. Kuna watu ni matapeli na wengine wasio waaminifu tunaendelea kushughulika nao."
Kwa sababu tunapopata habari inakuwa rahisi kwetu, kingine niwaombe wawe na imani. Sisi kama Serikali kazi yetu ni kuhakikisha tunasimamia sheria, tunatatua na kero," amefafanua.
Kiwale ameomba wananchi hao kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na kuwa na imani nayo pia, ameahidi Manispaa itatoa tamko kuhusiana na mgogoro wa eneo hilo na kwa sasa maofisa ardhi wapo kwa kamishna kujadiliana na suala la uvamizi katika vitalu namba moja hadi sita
Vilevile, Mtendaji wa mtaa huo wa Kichangani Mkukumbi Ferdinand amesema wakazi wamekuwa wakitoa taarifa iliyomfanya kuwasiliana na manispaa kwaajili ya kuzuia watu wanaojenga kwenye bonde.
“Mfano, baada ya kuwasiliana na manispaa wakaja wakamwambia mtu aliyekuwa anataka kujenga kwenye eneo la bonde aache mara moja, huku wakimtaka afuate utaratibu pamoja na kufuatilia amepata wapi vibali na hati,” amesema.