Ustawi kuanzisha kozi ya makuzi, malezi
Muktasari:
- Taasisi ya Ustawi wa Jamii – Kampasi ya Kisangara iko mbioni kuanzisha kozi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika ngazi ya cheti na stashahada itakaotambulika na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Dar es Salaam. Taasisi ya Ustawi wa Jamii – Kampasi ya Kisangara iko mbioni kuanzisha kozi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika ngazi ya cheti na stashahada itakaotambulika na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Uamuzi huo unakuja mara baada ya hivi karibuni kuzinduliwa kwa Programu ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya mwaka 2021/2022- 2025/2026.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Wazara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis katika Mahafali ya nne ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii – Kampasi ya Kisangara ambapo jumla ya wahitimu 524 wamehitimu.
Mwanaidi amesema suala hilo litasaidia Taasisi kukua kitaaluma na kuongeza idadi ya wataalamu katika fani ya Ustawi wa Jamii pamoja na Wizara kuendelea kutoa huduma bora kwa makundi maalum nchini kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii.
"Wizara kama mlezi wa Taasisi tutaendelea kuiangalia Taasisi hii kwa jicho la kipekee mno. Wizara itaainisha maeneo ya ushirikiano kati yake na Taasisi na kupanga mikakati ya pamoja ya kuwatumia wahitimu katika utoaji wa huduma kwa jamii, tafiti na ushauri wa kitaalamu," amesema Mwanaidy.
Hata hivyo amesema Taasisi kupitia kampasi ya Kisangara inazalisha wataalamu wa fani ya Ustawi wa Jamii na fani ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kada ambayo ni muhimu sana katika utekelezaji wa mipango ya Wizara.
Ameongeza kuwa Wizara pia imeweka miongozo, kanuni na sheria mbalimbali katika kuhakikisha suala la malezi ya mtoto yanatolewa kitaalamu katika nyanja zote za kijamii kuanzia ngazi ya familia hadi kwenye makao na vituo vya kulelea watoto mchana.
“Napongeza mipango ya Taasisi kutaka kuanzisha programu ya shahada ya Ustawi wa Jamii katika mwaka wa masomo 2022/2023. Hakika hii itasaidia Taasisi kukua kitaaluma na kuongeza idadi ya wataalamu katika fani ya Ustawi wa Jamii,” amesema Mwanaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni amesema kuwa Serikali kupitia, Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mwaka huu wa masomo wameletea wanafunzi katika ngazi ya cheti cha msingi katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara.
”Kwetu sisi hili linatuonyesha kuwa Taasisi yetu imeaminiwa kuwa ni sehemu na salama ya kuwasaidia vijana hawa kufikia malengo yao ya kitaaluma,” amesema Dk Joyce.
Nao baadhi ya wahitimu wamesema watakwenda kutumia taaluma walioipata hasa katika Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoa elimu sahihi kwa jamii katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora.