Usiyoyajua kuhusu mbege

Muktasari:
Kama ulidhani watu wanakunywa pombe ya asili aina ya mbege ili kulewa utakuwa umekosea sana. Kumbe pombe hii inayopatikana mkoani Kilimanjaro ina matumizi mengi kutokana na madai ya wenyeji wa Mkoa huo.
Moshi. Kama ulidhani watu wanakunywa pombe ya asili aina ya mbege ili kulewa utakuwa umekosea sana. Kumbe pombe hii inayopatikana mkoani Kilimanjaro ina matumizi mengi kutokana na madai ya wenyeji wa Mkoa huo.
Huuzwa zaidi kwenye vilabu vya pombe maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa huo lakini siku za hivi karibuni pombe hiyo imeanza kuuzwa hadi kwenye baa maarufu.
Pia imekuwa ni desturi ya wachaga kutumia mbege kwenye sherehe mbalimbali kama harusi na maeneo mengine muhimu kudumisha mila na tamaduni zao.
Baadhi ya wakazi wa mkoa huo wameeleza namna wanavyotumia mbege kufanya matambiko na kuomba mababu waliofariki dunia mafanikio ya vijana wao.
Akizungumza na Mwananchi Digital mmoja wa wakazi wa Mkoa huo ambaye ni mkazi wa kata ya Uru Kusini, Aloyce Kitali amesema wanaiheshimu mbege kwani kwa imani yao wanaamini bila kuomba wazee kwa kutumia mbege huwezi kufanikiwa.
"Tumezaliwa kwenye mila na desturi kuna mambo ya kimila yanasaidia vijana wetu kusimama kwenye shughuli zao za utafutaji, hivyo pasipo mbege hii kuwaomba wakuu wa mila kijana huwezi kupata mafanikio.”
"Ukiomba wakuu wa mila kwa kutumia hii mbege inaleta mafanikio makubwa na unakuta kijana anakuwa vizuri kwenye shughuli zake na hufanikiwa haraka sana kwa imani zetu za kichaga, mbege ni kitu muhimu sana kwenye mila na desturi zetu," amesema.
Anna Kimambo, mkazi wa Old Moshi anaeleza licha ya mbege kutumika katika mila pia husaidia wanawake waliojifungua kupata maziwa ya mtoto kwa wingi.
"Kiafya mbege ni mzuri kwa mfano mwanamke aliyejifungua na kukosa maziwa ya mtoto huku uchagani unapewa mbege na anapata maziwa vizuri na mtoto ananyonya bila shida kabisa," amesema Anna.